2377; Mwenza Wa Uhuru…

Wengi wanapenda sana wawe huru,
Ila wasichojua ni kwamba hakuna uhuru wa bure.
Uhuru huwa unaambatana na mwenza wake ambaye ni wajibu.

Kadiri unavyokuwa na uhuru mkubwa, ndivyo pia unavyokuwa na wajibu mkubwa.

Ukiwa na uhuru wa kifedha unawajibika kuweza kuzalisha, kutunza na kukuza fedha zako zaidi, kitu ambacho wengi hawakiwezi.
Ndiyo maana baadhi wakipata fedha zaidi wanazipoteza, kwa sababu wanakuwa hawajawa tayari kwa wajibu.

Ukiwa na uhuru wa kazi au biashara unawajibika kupanga na kutekeleza mambo yote muhimu na kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri. Kukamilisha haya ni kazi kubwa ambayo wengi hawapo tayari kujitoa kuifanya na ndiyo maana wanakosa uhuru.

Fikiria mhasibu ambaye anaweza kutunza hesabu za mapato na matumizi alipoajiriwa, lakini hawezi kutunza hesabu za fedha zake mwenyewe.

Fikiria daktari ambaye anaweza kumshauri mgonjwa kuhusu ulaji mzuri na vitu vya kuepuka lakini yeye mwenyewe anatumia vitu hivyo.

Fikiria hakimu ambaye anaweza kumhukumu mtu kwa kosa ambalo hata yeye amekuwa analifanya.

Yote hayo siyo tu unafiki, bali pia kushindwa kutumia vizuri uhuru, kwa kutokuwa tayari kuupokea wajibu.

Kabla hujakazana kutaka uhuru, ujue wajibu unaoambatana na uhuru huo na uwe tayari kuutekeleza ili ukipata uhuru usiupoteze.

Kocha.