Rafiki yangu mpendwa,
Kwa kipindi ambacho nimekuwa natoa huduma hii ya ukocha, nimebahatika kufanya kazi na wengi.

Kitu kimoja ambacho nimekuwa naona kinajirudia kwa wengi ni mtu anapojifunza kuhusu tabia za mafanikio huwa anakuwa na hamasa kubwa sana.

Kwa hamasa hiyo anapanga kubadili maeneo mengi ya maisha yake kwa wakati mmoja. Hamasa anayokuwa nayo inamfanya aone alichelewa sana kupata maarifa hayo.
Hivyo ili kufidia muda aliopoteza, anaona njia pekee ni kubadili kila eneo la maisha yake kwa wakati mmoja.

Kinachotokea kwa watu hawa ni kushindwa vibaya. Licha ya kuwa na hamasa, wanakuwa hawana nguvu ya kutosha kusukuma mabadiliko kwenye maeneo mengi ya maisha yao.

Kila mabadiliko ambayo mtu anafanya kwenye maisha yake huwa yanazalisha changamoto mpya. Hivyo mtu anapobadili maeneo mengi ya maisha yake kwa wakati mmoja, anatengeneza changamoto nyingi ambazo zinamuelemea na kushindwa kuendelea na mabadiliko.

Je hili linamaanisha mabadiliko ni magumu na hayawezekani?
Jibu ni ndiyo mabadiliko ni magumu na hapana, siyo kwamba hayawezekani.
Unapaswa kuwa na mkakati sahihi wa kufanyia kazi ili uweze kuleta mabadiliko unayoyamudu na yenye tija kwenye maisha yako.

Aliyekuwa mchumi wa nchini Italia, Vilfredo Pareto aligundua kwamba asilimia 80 ya matokeo huwa inazalishwa na asilimia 20 ya juhudi.
Kwa lugha rahisi ni kwamba katika juhudi nyingi unazoweka, kuna chache sana zinazozalisha matokeo makubwa na juhudi nyingi zinazozalisha matokeo madogo.

Kwenye kubadili tabia tunaweza kutumia kanuni hii ya Pareto (80/20 rule) na tukaweza kuweka juhudi kwenye machache na kuzalisha matokeo mazuri.

Ili ufanikiwe, huhitaji kuleta mabadiliko 10 kwa wakati mmoja kwenye maisha yako. Bali kuna maeneo mawili tu ambayo ukiweka nguvu zako za kufanya mabadiliko, utayabadili sana maisha yako.

Eneo la kwanza ni MTAZAMO.

Mtazamo wako ndiyo wewe, ndivyo unavyoiona dunia na ndivyo unavyojiona kwenye dunia.
Uko hapo ulipo sasa kwa sababu ya mtazamo ambao umekuwa nao huko nyuma.

Ukitaka kuyabadili maisha yako kwa haraka na kwa viwango vikubwa, anza kwa kubadili mtazamo wako.
Mtazamo ni kama miwani yenye rangi unayotumia kuiangalia dunia.
Kama miwani ina rangi nyeusi, kila kitu utakiona cheusi na kama ina rangi nyekundu kila mahali utaona ni pekundu.

Unaona vitu vikiwa na rangi hiyo, siyo kwa sababu ndiyo rangi ya vitu hivyo, bali kwa sababu ndiyo rangi unayoitumia kuiona dunia.
Hiyo ndiyo nguvu ya mtazamo.

Unavyiona dunia, sivyo ilivyo, bali ndivyo ulivyo.
Dah, hebu rudia tena kusoma hiyo sentensi kwa msisitizo na uone nguvu yake.
Kila unachokiona na namna unavyoichukulia dunia, siyo ilivyo bali wewe ndivyo ulivyo.

Kama umeelewa hapa rafiki yangu, dunia ni yako na mafanikio ni yako. Kwa sababu kitu cha kwanza unachopaswa kufanya ni kubadili namna unavyoiona na kuichukulia dunia na mambo mbalimbali.

Ni mwanasaikolojia William James aliyesema ugunduzi mkubwa wa karne ya 20 ulikuwa ni binadamu ana uwezo wa kuyabadili kabisa maisha yake kwa kubadili mtazamo wake wa kiakili.

Hapa ni mitazamo muhimu unayopaswa kujijengea na kuifanya kuwa sehemu ya maisha yako ili uweze kufanikiwa sana.

1. Kila kitu kinawezekana.
2. Nina uwezo mkubwa ndani yangu.
3. Watu ni wema na wana nia nzuri.
4. Dunia inakwenda kunipa kile ninachotaka.
5. Changamoto ni kiashiria cha ukuaji zaidi.
6. Hakuna kushindwa, kuna kujifunza.
7. Siwezi kueleweka au kukubalika na wote.
8. Naamini kwenye mchakato, njia za mkato ni ndefu na za kupoteza muda.
9. Ninachopata ni sawa sawa na ninachotoa, ili nipate zaidi, napaswa kutoa zaidi.
10. Nitapata ninachotaka au nitakufa nikiwa nakipambania, hakuna njia nyingine.

Amini hayo 10 bila ya shaka yoyote, yafanye kuwa sehemu ya maisha yako na utashangaa jinsi mambo yatabadilika kwako.
Utaanza kuiona dunia kwa namna ya tofauti kabisa.
Utashangaa watu unaojihusisha nao wamebadilika kabisa.
Na utaanza kuziona fursa nzuri kabisa zikija kwako.

Kitendo tu cha kubadili mtazamo wako, kinakuja na mabadiliko makubwa sana kwako.

Eneo la pili ni UJUZI.

Kama MTAZAMO ni jinsi unavyojiona na unavyoiona dunia, UJUZI ni kile unachokifanya, kile unachokitoa kwa dunia.

Ujuzi ni eneo la pili ambalo ukiweka juhudi zako utayabadili mno maisha yako na kuweza kufanikiwa sana.

Na unachohitaji hapa ni kimoja tu, kunijengea ujuzi mpya.
Kama unataka kuyabadili maisha yako,
Kama unataka kutoka hapo ulipo sasa,
Sehemu nzuri ya kuanzia ni kujijengea ujuzi mpya.

Hapa pia pana changamoto kwa sababu watu wamekuwa wakihangaika na mambo mengi ambayo hayana tija kwao.
Wewe usiwe hivyo, chagua ujuzi sahihi wa kunijengea, ambao utaleta matokeo mazuri kwako.

Katika kujijengea ujuzi ambao una manufaa kwako, fuata hatua hizi.
1. Anza  na tatizo au hitaji ambalo watu tayari wanalo. Tatizo linalowaumiza au hitaji linalowasukuma sana kiasi kwamba wapo tayari kutoa fedha zao ili kutatuliwa tatizo lao au kutimiza hitaji hilo.
2. Angalia ni thamani gani inayohitajika ili kutatua tatizo au kutimiza hitaji. Ona kile kinachopaswa kufanyika ili kuleta tija kwa wengine.
3. Jifunze jinsi ya kutengeneza thamani hiyo ambayo inahitajika. Jifunze kuzalisha kitu ambacho kina manufaa kwa wengine, iwe ni bidhaa au huduma.
4. Chagua watu ambao unalenga kuwapatia thamani yako, usimlenge kila mtu, utakuwa unajidanganya na kujipoteza, chagua wachache unaokwenda kuanza nao.
5. Wahudumie vizuri sana wachache unaoanza nao, hakikisha kuna mabadiliko mazuri unayoyeta kwenye maisha yao, wanayoyaona dhahiri.
6. Tengeneza mahusiano bora na wale unaowapa thamani unayozalisha, wasijione tu ni wateja, bali wajione ni sehemu ya familia ya kile unachofanya.
7. Waombe wale ulioanza nao na wakaelewa unachofanya wakuletee wengine zaidi wanaoweza kunufaika na unachofanya. Huku na wewe ukiendelea kuwafikia wapya zaidi.
8. Chukua maoni na mrejesho kutoka kwa unaowalenga na yafanyie kazi ili kuboresha zaidi.
9. Zidi kujijengea ubobezi kwenye kile unachofanya. Jijengee sifa ya utaalamu, uaminifu na kuwa na nidhamu nzuri ya kazi.
10. Kuwa na ndoto na mipango mikubwa kwenye kile unachofanya na kila wakati jisukume kubadilika ili kufika huko, usifanye tu kwa mazoea.

Kwa kuzingatia hatua hizi 10, utajijengea ujuzi ambao utazalisha thamani kubwa kwa wengi na kuwa na manufaa kwako pia.

Tabia mbili muhimu za kitajiri.

Kwenye kitabu cha tabia za kitajiri, nimeshirikisha tabia nyingi ambazo mtu unapaswa kujijengea na kuziishi kila siku ili uweze kujijengea utajiri na mafanikio makubwa.

Lakini zipo tabia kuu mbili ambazo zinabeba tabia nyingine zote.
Ukiweza kujijengea tabia hizo kubwa mbili, ukachanganya na haya mawili uliyojifunza hapa, utakuwa moto wa kuotea mbali.

Kama bado hujapata na kusoma kitabu cha TABIA ZA KITAJIRI, unajichelewesha mno kuyabadili maisha yako.
Pata kitabu hiki leo na uanze kukisoma, utaona jinsi umekuwa unajizuia mwenyewe.
Utayaona maeneo ya kuondoa breki kwenye maisha yako ili uweze kwenda kwa kasi kubwa ya mafanikio.

Kitabu ni nakala tete (softcopy) na kinatumwa kwa email. Kukipata tuma ujumbe wenye maneno KITABU CHA TABIA ZA KITAJIRI kwenda namba 0717 396 253 na utapewa utaratibu wa kukipata.
Chukua hatua sasa, tuma ujumbe ili upate kitabu hicho kinachokwenda kukupa maarifa ya kuyageuza kabisa maisha yako.

Moja ya kanuni muhimu utakayojifunza kwenye kitabu cha TABIA ZA KITAJIRI.

Rafiki, umeshayajua maeneo makuu mawili ya kuweka juhudi zako ili kuleta mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.
Kilichobaki ni wewe kuchukua hatua ili uweze kuyabadili maisha yako.
Usijicheleweshe, anza kuchukua hatua mara moja.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.
www.somavitabu.co.tz