2407; Ni msimamo au kukosa fursa?

Kuna watu ambao hawafanyi vitu fulani, wakidhani kwamba wana msimamo.

Kumbe watu hao hawana msimamo wowote, ni vile tu wamekosa fursa ya kuwawezesha kufanya kitu hicho.

Mfano mtu anaweza kusema hawezi kuiba, kumbe tu hajapata fursa ya kuweza kujipatia kitu kwa wizi bila ya kujulikana.

Au anaweza kusema hawezi kutoa au kupokea rushwa, kumbe tu hajawahi kuwa kwenye mazingira yanayomsukuma kufanya hivyo ili apate asichotaka.

Ni mara ngapi umesikia masikini wakiwashangaa wenye fedha wanavyotumia hovyo fedha zao, halafu na wao wakipata fedha wanaenda kufanya hicho hicho?

Ni mara ngapi mtu asiye kiongozi anawalaumu viongozi halafu anapata nafasi ya uongozi na kufanya yale yale aliyokuwa analaumu?

Watu wenye msimamo wa kweli kwenye jambo huwa ni wachache mno.
Wengi ambao hawafanyi siyo kwa sababu wana msimamo, ila kwa sababu tu hawajapata fursa ya kuwawezesha kufanya.

Hawajakutana na ushawishi mkubwa kwenye kitu hicho na kujua kama wanaweza kuuvuka.

Njia mbili za kutumia hili;
1. Usiamini sana msimamo wa watu ambao hawajapata fursa za kujaribu misimamo yao na wakavuka majaribu hayo.
2. Usijiambie una msimamo kama hujakutana na majaribu ya kutikisha msimamo wako na ukayashinda.

Kocha.