2407; Ni msimamo au kukosa fursa?
Kuna watu ambao hawafanyi vitu fulani, wakidhani kwamba wana msimamo.
Kumbe watu hao hawana msimamo wowote, ni vile tu wamekosa fursa ya kuwawezesha kufanya kitu hicho.
Mfano mtu anaweza kusema hawezi kuiba, kumbe tu hajapata fursa ya kuweza kujipatia kitu kwa wizi bila ya kujulikana.
Au anaweza kusema hawezi kutoa au kupokea rushwa, kumbe tu hajawahi kuwa kwenye mazingira yanayomsukuma kufanya hivyo ili apate asichotaka.
Ni mara ngapi umesikia masikini wakiwashangaa wenye fedha wanavyotumia hovyo fedha zao, halafu na wao wakipata fedha wanaenda kufanya hicho hicho?
Ni mara ngapi mtu asiye kiongozi anawalaumu viongozi halafu anapata nafasi ya uongozi na kufanya yale yale aliyokuwa analaumu?
Watu wenye msimamo wa kweli kwenye jambo huwa ni wachache mno.
Wengi ambao hawafanyi siyo kwa sababu wana msimamo, ila kwa sababu tu hawajapata fursa ya kuwawezesha kufanya.
Hawajakutana na ushawishi mkubwa kwenye kitu hicho na kujua kama wanaweza kuuvuka.
Njia mbili za kutumia hili;
1. Usiamini sana msimamo wa watu ambao hawajapata fursa za kujaribu misimamo yao na wakavuka majaribu hayo.
2. Usijiambie una msimamo kama hujakutana na majaribu ya kutikisha msimamo wako na ukayashinda.
Kocha.
Hiki ni kitu nilichokuwa sikielewi vizuri.
Mara nyingi nimekuwa naona watu wanakuwa na misimamo mikali na kupinga waziwazi yale wanayoyaona siyo sahihi mahali pao pa kazi pindi wanapokuwa hawana vyeo. Lakini inapotokea watu hao hao wakapandishwa cheo na masirahi yao yakaongezeka kidogo basi wanafanya yale yale ambayo walikuwa wanayapinga. Sasa nilikuwa najiuliza hawa watu vyeo ndivyo vinavyo wabailisha au ni jambo gani huwa linawafanya kuacha misimamo yao ya awali? Kumbe ni kokosa fursa ya jambo fulani.
Ahsante sana kocha kwa maarifa haya.
LikeLike
Karibu Datius.
LikeLike