Rafiki yangu mpendwa,
Hebu pata picha kama mimea ingekuwa na akili kama ambayo sisi binadamu tunayo.

Kwanza kabisa ingekuwa na mwalimu wa kuifundisha mimea hiyo namna gani inapaswa kuwa.

Kwenye shamba moja ambapo mbuyu na mchicha vimepandwa, mchicha utaanza kuota haraka kuliko mbuyu.

Kila mtu ataanza kuusema vibaya mbuyu, kwamba hauna akili, ni mzembe na mengine mengi.

Kwa nini ukubali kupitwa na mchicha kwenye kuota?

Baadaye mbuyu utaota kwa wakati wake, lakini utakuwa mrefu kuliko mchicha.
Watu wataanza tena kuulaumu mbuyu, kwa nini unakuwa mkubwa kuliko mwenzake mchicha?

Ninachotaka kusema hapa ni nini?
Kwamba kila kiumbe hai kina upekee wake, hakuna namna kinafanana na kiumbe mwingine aliye hai.

Lakini sisi binadamu, kwa akili zetu, tunaacha upekee wetu na kuhangaika kuwa kama wengine.

Unawezaje kuelezea watu wanaofanya kazi au biashara ya aina moja kufanya vitu vinavyofanana, kupata kipato kinachoendana na kuwa na maisha yanayofanana?

Kwamba hawa watu wote wanapata matokeo yanayofanana, kuna kitu kimebadilishwa ndani yao.

Sisi binadamu ndiyo viumbe pekee ambao tuna ubongo wa juu ambao ni mkubwa na ulioendelea sana.
Ubongo huo una uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi.
Na zaidi, ubongo huo una uwezo wa kutengeneza hadithi ambayo mtu akiiamini inakuwa uhalisia kwake.

Ubongo wetu una akili kubwa ambayo inaweza kuumba chochote ambacho mtu anakitaka sana.
Lakini kwa bahati mbaya sana tumekuwa hatujui hilo, hivyo tunaishia kuiga maisha ya wengine na kuzika uwezo wetu mkubwa.

Hivyo ndivyo tumeishia kupata matokeo yanayofanana wakati ndani tunatofautiana sana.
Kwa sababu tumeitumia nguvu ya akili zetu kutudumaza badala ya kutukuza.
Tumefundishwa kutumia nguvu ya akili kuiga kuliko kuwa wa kipekee.

Tushukuru sana viumbe wengine kutokuwa na akili kama zetu maana maisha yangekuwa majanga.
Hebu fikiria samaki angetaka kuwa kama ndege!
Au simba angechagua kuwa kama swala.

Kwa hakika mlinganyo uliopo duniani ungepotea kabisa na hilo lingekuwa na athari kwa viumbe wote hapa duniani.

Ni bahati nzuri kwamba kati yetu binadamu kuna ambao wamekataa kabisa kutumia akili zao vibaya, wamekataa kuwa watu wa kuiga na wamechagua kuishi kile kilicho ndani yao.

Licha ya kupingwa, kukataliwa na kukatishwa tamaa, wachache hao walisikiliza sauti ya ndani yao ambayo iliwaonyesha jinsi walivyo tofauti na kuchagua kuishi utofauti huo.

Walikutana na magumu mengi, il hawakuruhusu yawakatishe tamaa na hatimaye wakaleta matokeo ya tofauti.

Kila kitu tunachokifurahia leo, ni matokeo ya watu wachache ambao walikataa kutumia akili zao kuiga na kuamua kuzitumia kuumba.

Vijana waliokuwa na wazo la kurusha ndege angani waliambiwa wamechanganyikiwa, sayansi inayonyesha hakuna namna kitu kizito kinaweza kuruka angani.
Wangewasikiliza wanasayansi hao, ndege zingechelewa kugunduliwa.

Wakati Henry Ford anawaambia mainjinia wake anataka injini ya V8 walimwambia ni kitu kisichowezekana kifizikia, yeye akawaambia anaitaka na kweli akaipata.

Tunajifunza nini hapa rafiki yangu?

Wewe ni wakipekee kabisa, hajawahi kuwepo mwingine kama wewe na wala hatakuja kuwepo.

Akili yako ina uwezo mkubwa wa kuumba chochote kile unachotaka. Unachopaswa ni kukiamini kweli na kutokukubali kuyumbishwa na chochote.

Jamii inapenda kuhakikisha unakuwa kwenye kundi moja na wengine ili iweze kukutawala vizuri. Itakulinganisha na kukushindanisha na wengine ili tu usiwe wewe.

Njia pekee ya kuacha alama hapa duniani, kufanya makubwa ambayo hayajawahi kufanywa ni kuwa wewe, kuisikiliza sauti yako ya ndani na kufanya kile ambacho una msukumo mkubwa wa kukifanya.

Usijilinganishe au kushindana na mtu mwingine yeyote, kimbia mbio zako mwenyewe, pambana kufikia uwezo wako mkubwa na fanya yaliyo makubwa.

Jifunze kutoka kwenye asili, kila kitu kinakua kwa uwezo ulio ndani yake na siyo kwa kuiga wengine.
Ukipanda mbuyu na mchicha eneo moja, mbuyu utakuwa mkubwa kuliko mchicha, kwa sababu hiyo ndiyo asili yake.

Kadhalika popote pale unapokuwepo, iwe ni kwenye kazi, biashara na hata maisha kwa ujumla, jitambue na uwe wewe badala ya kufuata mkumbo.
Kuwa wewe ndiyo njia pekee ya kufanya makubwa na kuacha alama ya kipekee.

Kujifunza zaidi kuhusu nguvu kubwa ya kutenda miujiza iliyo ndani yako, pata na usome kitabu cha UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA leo, wasiliana na 0752 977 170.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.
http://www.somavitabu.co.tz