Rafiki yangu mpendwa,
Biashara ndiyo njia ya uhakika ya kuingiza kipato kisichokuwa na ukomo.

Ni njia iliyo wazi kwa kila mmoja na licha ya vikwazo mbalimbali vilivyopo kwenye njia hiyo, bado kila mtu anaweza kuitumia na akafanikiwa sana.

Lakini uhalisia ni tofauti na hilo.
Wengi wanashindwa kuingia kwenye biashara kwa sababu na visingizio mbalimbali.

Na hata wale wanaovuka sababu hizo na kuingia kwenye biashara, wengi zinakufa ndani ya miaka miwili na zile zinazomudu kuvuka kipindi hicho hazikui sana.

Ni biashara chache mno zinazofanikiwa kufika kwenye mafanikio makubwa.

Rafiki, zipo sababu nyingi zinazopelekea matokeo hayo ya kibiashara, lakini kubwa moja ni hii; KUKOSA UWAJIBIKAJI.

Kabla sijaelezea hiyo kwa kina, nikupe mifano miwili.

Ni kawaida kuwasikia wafanyabiashara wadogo wadogo wakilalamikia vitu kama ‘chuma ulete’ kwamba kuna namna fedha zinaondolewa kwenye biashara kimazingara.
Lakini huwezi kusikia benki ikilalamikia kitu kama hicho.
Hivi unadhani huyo chuma ulete angekuwepo kweli angehangaika na visenti vya biashara ndogo na kuacha mabilioni yaliyo benki?

Najua kama wewe ni mwamini wa mambo hayo ya chuma ulete, kwa kusikia mfano huu utajiambia, lakini benki wana madawa makali ya kuzuia chuma ulete.
Na jibu ni ndiyo, wanayo dawa moja kali sana ambayo chuma ulete akiikuta anakimbia, dawa hiyo inaitwa uwajibukaji.
Kila mwisho wa siku lazima fedha zilizoingia na zilizotoka zilingane, lazima kila senti ijulikane ilipo.

Benki ikipotea elfu moja itatafutwa mpaka ipatikane iko wapi. Kwenye biashara ndogo ilipotea elfu moja mtu anajiambia kwani elfu moja kitu gani, isinisumbue. Na hivyo ndivyo chuma ulete anavyokaribishwa.

Nenda kwenye biashara yoyote ndogo na mwambia mwenye biashara akupe namba zake za kibiashara, ataishia kutoa macho tu. Yeye anachojua ni kununua na kuuza, mengine hayana umuhimu kwake.
Nenda kwenye biashara yoyote kubwa, makampuni ambayo yameorodheshwa kwenye soko la hisa na wala huhitaji kuomba namba, zimewekwa wazi mahali panapoonekana au mtandaoni.

Chochote kisichopimwa hakikui, hivyo biashara ambayo namba hazijulikani, hata ifanye nini, haiwezi kukua. Maana hata huko kukua hakujulikani kwa sababu hakuna namba zinazojulikana.
Biashara kubwa zina namba kwa sababu kuna uwajibikaji, biashara ndogo hazina namba kwa sababu hakuna uwajibikaji.

Umuhimu wa uwajibikaji.

Kwa asili, sisi binadamu ni wavivu, wazembe na tunaopenda njia rahisi za kupata kile tunachotaka.
Tunapokutana na ugumu huwa tunaukimbia au kuukwepa.

Kwa kuwa hakuna mafanikio bila ya ugumu, na kwa kuwa hatupendi ugumu, unaweza kuona mwenyewe hapo kwa nini wengi hawafanikiwi.

Nimepata nafasi ya kufanya kazi ya kuwakochi wengi kwenye eneo la biashara na inapofika kwenye namba ndiyo kuna kila aina ya ugumu.
Mtu anakuambia kwa biashara yangu ya reja reja ni vigumu sana kuzijua namba.

Hivi unafikiri Bakhresa anayeuza mandazi, nazi, ice crea na vingine anajipa sababu kama yako? Kwamba ni vigumu kuzijua namba?
Jibu ni hapana, ana uwajibikaji ambao unamsukuma kufuatilia kila kitu na kukiripoti.

Na usiseme yeye anaweza kwa sababu ni kampuni kubwa tayari, amefika hapo kwa sababu alianza kuzingatia hayo mapema.

Unapataje uwajibikaji?

Kwanza kabisa huwezi kujiwajibisha wewe mwenyewe.
Hata uwe na nidhamu kiasi gani, huwezi kujiwajibisha mwenyewe, kuna mahali uvivu na uzembe utakuzidi nguvu na kujikuta tu umeshateleza.

Hivyo uwajibikaji wa kweli unatoka kwa watu wengine, watu ambao unawaambia nini unataka kupata na utafanya nini ili kukipata na kisha kuripoti kwao namna ulivyofanya na matokeo uliyopata.

Makampuni yote makubwa yanawajibika kwa bodi ya wakurugenzi.
Hicho huwa ndiyo chombo cha juu kabisa kinachoisimamia biashara na hata mwanzilishi na mmiliki wa biashara.

Bodi hiyo inakuwa na wajumbe ambao siyo wafanyakazi wala wamiliki wa biashara.
Uwepo wa watu hao unafanya wale wanaoendesha biashara moja kwa moja, iwe ni mwanzilishi mwenyewe (founder) au mkurugenzi mtendaji (CEO) kufanya kazi kwa kujua wanapaswa kuripoti kwenye chombo cha juu zaidi.
Hilo linawasukuma kuchukua hatua ili kufikia malengo waliyojiwekea.

Karibu upate uwajibikaji.

Kwa wale walio kwenye KISIMA CHA MAARIFA, tupo kwenye muongo (2020 – 2030) wa kila mmoja kufika kwenye ubilionea.
Na kila mtu ana malengo na mipango mizuri tu ya kufika huko.

Lakini kinachokosekana ni uwajibikaji, wengi wanakwenda tofauti kabisa na ile mipango ambayo walikuwa wamejiwekea.
Na wengine hawajui kama wanakwenda tofauti, maana uvivu na uzembe wa asili unakuwa umewateka.

Kwa wale waliojitoa kweli kufanya makubwa kwenye huu muongo, tunakwenda kujenga timu za uwajibikaji ambazo zitawasukuma kufikia malengo hayo.

Timu hizo ambazo zitakuwa za watu wasiozidi watano, zitakuwa na manufaa matatu kwa pamoja.

Moja zitakuwa ni Master Mind Group ambapo watu wanakwenda pamoja kwenye safari ya mafanikio.

Mbili zinakuwa ni Bodi ya wakurugenzi ambapo kila mmoja anakuwa mjumbe kwenye biashara ya wenzake na kusukumana kukuza biashara.

Tatu inakuwa ni kikundi cha kibiashara ambacho kinaweza kunufaika kwa njia mbalimbali kama huduma za kifedha na kadhalika.

Bila uwajibikaji, malengo makubwa ambayo mtu unakuwa nayo inakuwa ni njia ya kujifurahisha tu.

Sifa za kupata uwajibikaji.

Kama umeelewa dhana hii ya uwajibikaji na unahitaji kunufaika nayo, unahitaji kuwa na sifa zifuatazo.

1. Mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA na ambaye utaendelea kuwa mwanachama kwa maisha yako yote.

2. Kushiriki SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA kuanzia 2021 na kuendelea.

3. Kuwa na biashara ambayo una malengo ya kuikuza kwa viwango vya juu.

4. Kuwa tayari kushirikiana na wengine hata kama umetingwa sana.

Kama upo tayari kwa hili la uwajibikaji fungua hapa na ujaze fomu; https://bit.ly/kisimainfo

Karibu sana rafiki yangu kwenye mfumo huu wa uwajibikaji ili uweze kufikia malengo yako makubwa.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.
www.somavitabu.co.tz