Rafiki yangu mpendwa,
Kadiri ninavyojifunza na kuiishi misingi ya kupata mafanikio makubwa kwenye maisha, ndivyo ninavyozidi kuona ukweli ambao huwa hauwekwi wazi.

Nimewahi kusema hakuna siri za mafanikio, mambo yote kuhusu mafanikio yapo wazi kabisa. Kujua kusudi lako, kuwa na ndoto kubwa, kuwa na nidhamu, kujituma sana na mengine kama hayo.

Lakini nimekuja kugundua siri za mafanikio zipo na ni mambo ambayo yako bayana kabisa, ila huwa hayazungumziwi, kwa sababu yanaumiza sana.

Moja ya siri iliyo bayana kuhusu mafanikio ni gharama ambazo mtu unapaswa kulipa ili kupata mafanikio makubwa.

Kadiri mafanikio unayoyataka yanavyokuwa makubwa, ndivyo gharama unazopaswa kulipa zinavyokuwa kubwa zaidi.

Na kwa jinsi gharama hizo zinavyokuwa kubwa, wengi hawawezi kuzimudu.
Wengi wanaotaka mafanikio makubwa hawataweza kuyapata kwa sababu hawawezi kulipa gharama wanazopaswa kulipa.

Sasa karibu ujipime ili uone kama kweli umejitoa kuyapata mafanikio makubwa unayotaka au unajifurahisha tu kujiambia unataka kufanikiwa.

I Kuweka kazi sana.

Mafanikio na kazi ni mapacha ambao hawawezi kutengana.
Popote unapomkuta mmoja, jua na mwingine yupo.
Na siyo tu kazi ya kawaida, bali kazi ya viwango vya juu na inayofanywa kwa muda mrefu.
Hakuna njia za mkato kwenye mafanikio yoyote yale, lakini iangalie jamii na utaona jinsi njia za mkato zinavyouzwa kwa wingi.
Ili ufanikiwe unahitaji kuwa na uvumilivu wa kuweka kazi kwa muda mrefu bila ya kuchoka au kukata tamaa.

Jinsi ya kulipa gharama hii; jitoe kuweka kazi hasa, mtangaze kazi kuwa rafiki yako na epuka njia zozote za mkato.

II Kukosa maisha ya kijamii.

Kwa kuwa mafanikio yanakutaka uweke kazi sana na kwa muda mrefu, na kwa kuwa muda una ukomo, kuna maeneo inabidi yakose muda wako.
Na eneo linaloathirika sana ni mambo ya kijamii.
Shughuli mbalimbali za kijamii ambazo zinachukua muda wako mwingi lazima uwe tayari kutengana nazo.
Mafanikio yako ndiyo yanapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza kwako.
Starehe, mapumziko, sherehe na mambo mengine ya kijamii hutaweza kuyahudumia yote na kuweza kuendelea na safari ya mafanikio.

Jinsi ya kulipa gharama hii; chagua shughuli chache za kijamii ambazo utajihusisha nazo kwa muda mchache ulionao. Nyingine achana nazo na hilo lisikuumize, jua ni gharama unalipa.

III Marafiki wachache.

Kwa kuwa marafiki wengi wanapatikana kwenye shughuli za kijamii ambazo wewe haupo sana.
Na kwa kuwa wengi wanapokutana wanajadili vitu vya kawaida ambavyo wewe hivijali.
Safari ya mafanikio itakupunguzia sana marafiki.
Lazima uwe tayari kwa hili, la sivyo itakuwa vigumu kwako kufanikiwa.

Jinsi ya kulipa gharama hii; tengeneza mahusiano bora na marafiki wachache ambao pia wapo kwenye safari ya mafanikio, hao ndiyo watakuwa na manufaa kwako.

IV Kutokueleweka.

Mafanikio yanakuraka uwe na maono makubwa sana ambayo wengine hawayaoni.
Kufanyia kazi maono hayo lazima uwe tofauti sana na jinsi wengine walivyo.
Hayo yatapelekea watu wengi wasikuelewe.
Na wasipokuelewa watakupa majina mbalimbali, huku wakiyatafsiri maisha na matendo yako kwa namna wanavyoelewa wao.
Wapo watakaosema umechanganyikiwa, huku wengine wakisema unayumia nguvu za giza.
Maneno yatakuwa mengi mpaka wewe mwenyewe utashangaa.

Jinsi ya kulipa gharama hii; jua watu hawatakuelewa kwenye safari yako ya mafanikio. Na wala usihangaike kuwaelewesha, maana kadiri unavyofanya hivyo ndivyo wanazidi kutokukuelewa. Wewe fanyia kazi maono yako makubwa na acha matokeo unayozalisha yaseme yenyewe.

V Kuanguka mara nyingi.

Unapoweka mipango ya mafanikio, unaona matokeo mazuri tu.
Kila hatua inaonekana vyema kabisa na matokeo yake ni mazuri.
Lakini kama wanavyosema, mipango siyo matumizi.
Haijalishi umepanga vizuri kiasi gani, haijalishi umeweka juhudi kubwa kiasi gani.
Inapokuja kwenye kuchukua hatua, matokeo unayopata ni tofauti kabisa na ulivyotegemea.
Kwa kifupi ni utaanguka mara nyingi kabla hujapata kile unachotaka.

Jinsi ya kulipa gharama hii; fanya maamuzi kwamba utapata unachotaka au utakufa ukiwa unakipambania. Kwamba hakuna namna utakata tamaa hata ukutane na nini, badala yake utaendelea na mapambano.

VI Kusimama mwenyewe.

Wakati unaanza safari ya mafanikio, kuna watu wataonekana wako nyuma yako na kukuunga mkono.
Unapoanza kukutana na maanguko, ukigeuka nyuma unajikuta uko peke yako.
Huo ni wakati rahisi sana kukata tamaa na kuona haiwezekani tena.
Lakini hupaswi kufanya hivyo, kwani kusimama peke yako ndiyo gharama unayopaswa kuilipa ili kupata mafanikio makubwa.

Jinsi ya kulipa gharama hii; unapoianza safari ya mafanikio, hakikisha unaweza kusimama mwenyewe pale unapokutana na magumu. Usiwaamini sana wale wanaokuambua wako pamoja na wewe, kumbuka kwenye giza hata kivuli chako mwenyewe kinakukimbia.

VII Kujishuku mwenyewe.

Kutokana na kupitia magumu na kuanguka mara kwa mara.
Ukichanganya na maneno ambayo watu wanasema kuhusu wewe.
Kuna wakati utaanza kujishuku mwenyewe.
Utajiuliza kama kweli njia uliyochagua ni sahihi kwako.
Wakati mwingine unaona kama wanaokupinga na kukukatisha tamaa wako sahihi.
Kuna wakati mpaka unaweza kushuku utimamu wa akili yako, na kuona kama umechanganyikiwa hivi.
Nyakati hizo zitakuwepo kwenye safari yako, muhimu ni kuendelea kuitazama picha kubwa ambayo ni maono unayofanyia kazi.
Chochote kinyume na picha hiyo ni usumbufu kwako, achana nacho.

Jinsi ya kulipa gharama hii; kuwa na KWA NINI kubwa ya mafanikio unayotaka kufikia, kanuni inayohusisha wengine wanavyonufaika pia. Na pale unapoanza kujishuku, rudi kwenye kwa nini yako na utaweza kuondoa mashaka uliyonayo juu yako mwenyewe.

VIII Kutoa kafara.

Kuna vitu vizuri unavyovipenda sana kwenye maisha yako, lakini ni kikwazo kwako kufika kwenye mafanikio makubwa unayoyataka.
Bila ya kuwa tayari kuachana na vitu hivyo, mafanikio hayawezekani kabisa kwako.
Hii ndiyo dhana ya kutoa kafara, kuachana na vitu vizuri na unavyovipenda, tena vinavyokunufaisha, ili upate vilivyo bora zaidi.

Jinsi ya kulipa gharama hii; hakikisha mafanikio unayopigania ndiyo kitu unachopenda na kujali zaidi. Yaani unakuwa hujiulizi mara mbili kuhusu kuacha mengine mazuri ili kufanya hicho ulichochagua. Kama kuna kitu kingine kinaweza kupata kipaumbele kikubwa kuliko mafanikio yako, jua wazi hutaweza kufanikiwa.

IX Kuchukiwa.

Baada ya kupambana sana na ukafanikiwa.
Baada ya kulipa gharama zote hizo kwa kipindi kirefu.
Unaweza kuona sasa ni wakati wa kuyafurahia mafanikio yako.
Unaweza kutegemea dunia ikusifu kwa juhudi ulizoweka mpaka kufanikiwa.
Lakini hicho siyo kinachotokea.
Badala yake unaanza kuchukiwa zaidi na wale ambao hawajafanikiwa.
Watu watachagua kukuchukia tu bila sababu yoyote ya msingi.
Wataona mafanikio yako kama sababu ya wao kushindwa.
Na kwa wengine, mafanikio yako yanakuwa hatari kwao.
Hivyo kadiri unavyofanikiwa, ndivyo utakavyochukiwa na wengi zaidi.

Jinsi ya kulipa gharama hii; ishi maisha halisi na ya kweli kwako, usigafute kupendwa na kila mtu. Hata ufanye mazuri kiasi gani, jua kuna watu watakuchukia tu, kwa sababu wanajichukia wao wenyewe. Usiingie kwenye chuki zao, wewe pambana na mafanikio yako.

X Hakuna kustaafu.

Wakati unaianza safari ya mafanikio, unakiona kilele kimoja cha mafanikio.
Unapambana sana kukifikia kilele hicho ukijua ndiyo kila kitu kwako.
Unakuwa tayari kuteseka kwa kujua ukishafika kwenye kilele hicho, kinachofuata ni raha mustarehe.
Ni mpaka unapofika kwenye kilele hicho ndiyo unagundua kuna vilele vingine vingi ambavyo ulikuwa hujaviona.
Hivyo kila unapofanikiwa, ni kama unaianza upya safari yako ya mafanikio.
Kwa kifupi ni safari ya mafanikio haina kustaafu, kila siku una kitu cha kufanyia kazi mpaka unapoondoka hapa duniani.

Jinsi ya kulipa gharama hii; chagua kufanya kitu ambacho unakipenda, kitu ambacho kwako siyo kazi, ni kama mchezo tu. Na unapoingia kwenye safari ya mafanikio, jua mafanikio ni safari yenyewe na siyo mwisho wa safari. Usiahirishe maisha kwa kujiambia ukifanikiwa ndiyo utafanya hivi au vile, ishi maisha yako kamili sasa, la sivyo utasubiri mpaka siku unaondoka hapa duniani.

Rafiki, je hizo ni gharama ambazo upo tayari kuzilipa?
Kama jibu ni ndiyo basi karibu kwenye safari ya mafanikio na jitoe kweli kweli, ukijua ni safari ya maisha yako yote.
Kama jibu ni hapana pia hakuna ubaya, maana yake kuna mengine unayathamini zaidi kuliko mafanikio, hicho basi yape umakini hayo.

Muhimu ni uchague upande na ukubaliane na yale yanayoambatana na upande huo.
Siyo unachagua upande wa mafanikio halafu watu wanakuambia hueleweki na hilo linakuumiza, unataka uanze kueleweka.
Au unachagua kueleweka halafu unaumia kwamba hupati mafanikio makubwa.

Chagua upande wako na utendee haki upande huo.
Je ni upande upi umechagua na kuwa tayari kulipa gharama ya huo upande?

Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani,
www.somavitabu.co.tz

Ndani yako kuna nguvu ya kuweza kufanya makubwa na kufanikiwa sana. Jua jinsi ya kufikia nguvu hiyo na kuitumia. Soma kitabu cha UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA, kukipata wasiliana na 0752 977 170