Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu kinachoitwa The third door : the wild quest to uncover how the world’s most successful people launched their careers ambacho kimeandikwa na Alex Banayan.

Alex alichagua kuwafuatilia watu waliofanikiwa sana kwenye yale wanayofanya kwa lengo la kujua kule walikoanzia.
Hilo halikuwa zoezi rahisi, ilimtaka kuwa na uvumilivu na ung’ang’anizi wa hali ya juu kitu ambacho kilimsaidia kukutana na wengi.

Ni katika safari hiyo ndiyo Alex anatushirikisha dhana ya mlango wa tatu katika kuyaendea mafanikio.
Karibu tujifunze kupitia uchambuzi wa kitabu hiki.

Utangulizi.
Mafanikio kwenye maisha ni kama kuingia kwenye klabu ya usiku.
Kuna njia tatu za kuweza kuingia.

Kuna mlango wa kwanza; huu ni mlango mkuu unaotumiwa na wote. Mlango huu huwa una foleni ndefu maana asilimia 99 ya watu ndiyo wanautegemea kuingia.

Kuna mlango wa pili; huu ni mlango wa watu mashuhuri (VIP), ambapo wale wenye wadhifa au mafanikio makubwa huwa wanautumia. Mlango huu hutumiwa na wachache.

Ambacho wengi hawajui ni huwa kuna mlango wa tatu. Huu ni mlango ulio nyuma na ambao haujulikani. Kufikia mlango huo ni mpaka uruke ukuta, ugonge mlango kwa nguvu au wakati mwingine kupita dirishani au kupitia jikoni. Kwa vyovyote vile, upo mlango wa tatu ambao wengi hawaujui.

Ni mlango huo wa tatu ambao watu waliofanikiwa sana waliutumia kuanza safari yao ya mafanikio.
Hakuna aliyefanikiwa kwa kufanya yale wengine wanafanya.
Wote waliofanikiwa kuna kitu cha tofauti kabisa walifanya wakati wanaianza safari yao na hilo likawa na manufaa sana kwao.

Kupitia kitabu hiki tunakwenda kujifunza kwa kina dhana hiyo ya mlango wa tatu na umuhimu wake kwenye mafanikio.

Tunakwenda kujifunza jinsi Bill Gates alivyoweza kuishawishi kampuni ya IBM kukodi programu yake badala ya kuinunua moja kwa moja.

Tunakwenda kujifunza jinsi Steve Jobs na Steve Wozniak walivyoweza kukutana na kuanzisha kampuni ya Apple.

Muhimu zaidi tutajifunza kupitia ugumu ambao Alex alikuwa anakutana nao katika kuwapata watu wa kuwahoji na jinsi ung’ang’anizi ulivyoweza kumsaidia, huku pia ukiwa kikwazo kwake wakati mwingine.

Kuna vitabu vingi vinavyoeleza sifa za watu waliofanikiwa, lakini hiki ni cha tofauti kwa sababu tunajifunza mchakato mgumu ambao mtu amepitia katika kupata taarifa hizo za watu waliofanikiwa.

Uchambuzi kamili wa kitabu hiki, pamoja na kitabu chenyewe vinapatikana kwenye channel ya Telegram ya SOMA VITABU TANZANIA.
Jiunge sasa na channel hiyi kwa kufungua http://www.t.me/somavitabutanzania upate chambuzi za vitabu na vitabu vyenyewe.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.