2551; Jua sheria kabla hujazivunja.

Siyo sheria za nchi, bali zile taratibu mbalimbali za kijamii ambazo zipo na zimezoeleka na kila mtu.

Kuzifuata taratibu hizo ni kuzuru, kunakufanya ueleweke na ukubalike na wengine kwenye jamii.

Lakini huwezi kufikia ubobezi wa hali ya juu na kupata mafanikio makubwa kwa kuendelea kufuata taratibu hizo.
Maana hilo litakuletea matokeo ambayo ni ya mawaida, sawa na ambayo wengine wanayapata.

Kupata matokeo makubwa na ya kipekee, lazima uende kinyume na taratibu na mazoea yaliyopo.
Wengi wanajua hili na hivyo hukimbilia kuvunja taratibu mbalimbali zilizowekwa kwa kuona ni kikwazo kwao.

Wanachokuwa hawajui ni kwamba hata utaratibu uwe wa kijinga kiasi gani, kuna sababu ya kuwepo kwake, kuna manufaa yake.
Hivyo kabla hujakimbilia kuvunja utaratibu huo, jua kwanza una umuhimu gani na una mbadala gani wa kupata umuhimu huo.

Kama hujajua umuhimu na mbadala wa utaratibu wowote, usiuvunje, kwa sababu utaishia kupata madhara kuliko manufaa.

Hatua ya kuchukua;
Kabla hujavunja utararibu na mazoea yoyote yale, jiulize nini manufaa yake na kuwa na njia mbadala ya kupata manufaa hayo.
Kukimbilia kuvunja taratibu na mazoea kabla hujayaelewa kwa undani ni kutengeneza matatizo makubwa.

Tafakari;
Hata saa ambayo ni mbovu, huwa inasema muda sahihi mara mbili kwa siku.
Usione kila kitu ni cha hovyo, jua kina manufaa yake na hivyo yajue na uwe na mbadala wake kabla ya kuondokana na kitu hicho.

Kocha.