2556; Mbona huyu mtoto hakui haraka?
Mara kwa mara huwa napata swali la aina hii ninapokuwa natibu wagonjwa.
Mzazi mwenye wasiwasi anauliza mtoto anakaribia mwaka, lakini bado hajaota meno.
Nilimchunguza mtoto vizuri nagundua hana shida yoyote, maendeleo yake yote yako vizuri.
Hapo huwa napenda kudadisi nini kinampa hofu zaidi mzazi.
Na mara nyingi huwa ni vitu viwili;
Moja, anamlinganisha mtoto huyo na watoto wengine ambao amewahi kuwa nao, anakuambia, wenzake kwa umri huu walishafika hatua fulani.
Mbili, wanakuwa wamejazwa hofu na watu wengine, wakiambiwa, wewe mbona mtoto wako amechelewa hatua fulani?
Hapo namweleza vizuri kwamba licha ya watoto kupaswa kupiga hatua fulani kwenye umri fulani, haimaanishi wote watapiga hatua hivyo.
Mara zote wapo ambao huwa wanawahi na wapo ambao huwa wanachelewa.
Hivyo kama mtoto hana shida nyingine yoyote, atakua tu kadiri anavyokwenda.
Maana mtoto hakui kwa kuangalia wengine wanafanyaje, bali anakua kwa kutumia kile kilicho ndani yake.
Hili pia nimekuwa nakutana nalo kwenye huduma ya ukocha.
Mtu anaweka juhudi kubwa kweli kweli, lakini bado matokeo hayaji kama alivyotarajia.
Huku wengine ambao hawaweki juhudi kama yeye, wanapata matokeo makubwa.
Hili ndiyo hupelekea watu kujikuta wanahangaika na mambo mengi kila wakati.
Pamoja na hayo, bado hakuna hatua kubwa wanazopiga.
Hivyo ushauri muhimu kwenye hili ni huu; kama tayari umeshajua kusudi la maisha yako, kama tayari unazo ndoto kubwa, kama tayari unao mchakato unaofanyia kazi kila siku katika kuliishi kusudi na kufikia ndoto zako, basi matokeo yasikuhangaishe sana.
Wewe endelea kupambana na mchakato wako kila siku, matokeo yatakuja kwa wakati wake.
Na kama unaona wengine wanafanikiwa haraka kuliko wewe, tatizo ni hili, hujawa ‘bize’ kwelikweli na mafanikio yako ndiyo maana unapata muda wa kufuatilia mafanikio ya wengine.
Hebu anza kuwa bize na mafanikio yako na wewe utafanikiwa pia.
Hatua ya kuchukua;
Ni kitu gani ambacho umekuwa unajiambia kinachelewa kwako? Hakikisha upo kwenye mchakato sahihi na futa neno kuchelewa, wewe weka mchakato na matokeo yatakuja kwa wakati wake.
Tafakari;
Ukiacha kuangalia na kujilinganisha na wengine, safari yako ya mafanikio itakuwa rahisi sana. Lakini ukishaanza kujilinganisha na wengine, lazima uone unachelewa. Maana mara zote kuna ambao wanapata matokeo ya haraka na makubwa kuliko wewe.
Kocha.
Asante Sana kocha. Nakomaa na mchakato sahihi na matokeo yatakuja yenyewe.
LikeLike
Vizuri Tumaini.
LikeLike
Asante Sana kocha,hebu nipambane na mchakato naimani nitafika ni suala la mda.
LikeLike
Vizuri Beatus.
LikeLike