Rafiki yangu mpendwa,
Unajua wajibu mkubwa niliojipa ni wewe.
Yaani kazi yangu kubwa, ambayo inatokana na kusudi nililonalo na ninaloliishi ni kuhakikisha nayafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi kupitia chochote ninachofanya.

Yaani kwa dakika utakazotumia kusoma hapa, uondoke ukiwa bora kuliko ulivyokuwa kabla hujasoma hapa.

Nathamini sana muda wako unaonipa, hakuna chenye thamani kama muda wako.
Muda huu unaotumia kusoma hapa, kuna mambo mengine chungu mzima ungeweza kuwa unayafanya.

Lakini hayo yote umeyaweka pembeni na kuchagua kusoma andika hili. Nathamini sana hilo na ninakazana kuhakikisha kweli unaipata thamani, ili muda wako usipotee, bali uwe umeuwekeza vizuri.

Mwezi januari umeisha, kuna waliofurahia hilo ila kuna wengi ambao wameumaliza kwa huzuni na kukata tamaa.

Wengi usiku wa tarehe 31 disemba na siku nzima ya tarehe 01 januari zilikuwa siku za matumaini makubwa sana.

Zilikuwa siku za kuona wazi kwamba mwaka huu unakwenda kuwa wa tofauti na wanakwenda kufanya makubwa.

Matumaini hayo yakiwasukuma wengi;
Kuanza kufanya mazoezi.
Kuanza kuweka akiba.
Kuanza kusoma vitabu.
Kuanza kuwahi kazini au kwenye biashara.
Kuanza kufanya mambo yao kwa utofauti.

Lakini sasa januari imeisha na yote hayo hayapo tena.
Wengi wamekata tamaa na kupoteza yale matumaini waliyoanza nayo januari.
Wengi wamekata tamaa na kuona hakuna namna wanaweza kubadili maisha yao.

Wameishia kuyakubali maisha yao ya kawaida na kupuuza kabisa ndoto kubwa walizonazo na uwezo wa kipekee ukio ndani yao.

Rafiki, mimi sijakuchoka wewe na wala sitakuacha ukate tamaa.

Ndiyo maana leo ninakutaka ujisamehe kwa yale uliyofanya januari, yakapelekea ukate tamaa na kurudi kwenye mazoea.

Nakusihi ujisamehe kwa sababu ndivyo binadamu tulivyo, tunaendeshwa zaidi na hisia na huwa zinayumbishwa haraka na kwa vitu vidogo.

Huenda kwa hatua ulizoanza kuchukua ulitegemea uwe umeanza kupata matokeo fulani, ila hukuyaona na hapo ukaona hatua hizo hazina maana na ndiyo maana ukaziacha.

Leo nina mbadala kwako, leo nina ushauri wa kitu kizuri kufanya ili usirudi tena kwenye anguko hilo, uendelee na juhudi zako mpaka upate matokeo makubwa unayoyataka.

Kitu hicho hakihitaji uwe na chochote cha ziada, tofauti na vile ulivyonavyo sasa.

Kitu hicho ni kuiishi siku moja kwa ukamilifu wake.

Sahau kuhusu jana na yale uliyishindwa kufanya au uliyofanya na hayakuleta matokeo.

Sahau kuhusu kesho na yale unayotamani kuja kuyafanya au matokeo unayotegemea kuja kuyapata.

Wewe iangalie siku uliyonayo, kisha iishi siku hiyo moja tu kwa ukamilifu mkubwa.

Anza kwa kuandika kabisa, kwamba ili siku iwe ya ukamilifu kwako ni vitu gani unapaswa kuvifanya.

Kama swali hilo halikupi majibu  nenda kwenye hili; kama leo ingekuwa ndiyo siku yako ya mwisho hapa duniani, ni vitu gani ungevifanya?

Kwa lugha nyingine, unapaswa kuiishi kila siku kama vile ndiyo siku yako ya mwisho kuwa hapa duniani.
Hili likubali kutoka ndani yako kabisa kisha weka vipaumbele vyako kwa usahihi kwenye kila siku yako.

Haya siyo maigizo wala kujifanganya, kwani ipo siku ambayo huijui ambayo itakuwa siku yako ya mwisho hapa duniani.
Kwa kuwa siku hiyo inakuja, ila huijui ni lini, kwa nini usiishi kila siku kama ndiyo hiyo?

Utauliza vipi nikipata siku nyingine wakati nimeshaiishi iliyopita kama ya mwisho? Na mimi nitakuuliza vipi unapomaliza kazi yako na kupewa malipo yako, halafu baadaye ukaja kupewa tena ya ziada? Unayakataa? Unachukia?

Majibu ni hapana, unayapokea na kuyafurahia malipo ya ziada.

Kadhalika kwenye siku, unapoiishi siku yako kama ya mwisho, halafu ukaipata siku nyingine ya ziada, unaifurahia na kisha kuiishi hiyo tena kama ya mwisho.

Ni kwa kwenda hivi ndiyo unaweza kujenga maisha ya mafanikio makubwa bila ya kukata tamaa na kuishia njiani.

Kuna rasilimali mbili muhimu sana na kushauri uwe nazo ili uweze kutekeleza haya uliyojifunza hapa.

Ya kwanza ni kitabu cha KANUNI YA SIKU YA MAFANIKIO. Hiki kitakusaidia kuipangilia kila siku yako vizuri, kuwa na vipaumbele sahihi na kuiishi kila siku yako kwa ukamilifu mkubwa.

Rasilimali ya pili ni kitabu cha MWONGOZO WA MAISHA YA MAFANIKIO. Hiki kitakusaidia kujua nini maana ya mafanikio kwako na vitu gani unapaswa kutoa kafara ili kufanikiwa.

Kupata rasilimali hizi wasiliana na 0752 977 170.

Kwa pamoja rasilimali hizi zitakusaidia kuwa wewe na kuyaishi maisha yako, kitu ambacho ni muhimu sana kwa zama tunazoishi sasa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana.
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.