2955; Kupendwa au kuheshimiwa?

Rafiki yangu mpendwa,
Wajibu wetu wa kwanza kama viongozi kwenye biashara zetu ni kuwafanya watu wafanye vitu ambavyo hawataki kufanya, lakini vyenye manufaa kwao.

Na hilo halitakuweka kwenye nafasi ya kupendwa sana na watu hao unaowaongoza, kwa sababu utakuwa unawasukuma kuondoka kwenye mazoea.
Hakuna kitu kinachowafanya watu wajisikie vizuri kama kukaa kwenye mazoea.

Sasa kitendo cha wewe kuwasukuma kutoka kwenye mazoea waliyojijengea, hakitapokelewa kwa urahisi.
Kitaonekana ni kigumu, kibaya na kisicho wezekana.
Kama utakachokuwa unataka ni kupendwa na watu unaowaongoza, hutawalazimisha kwenye mabadiliko hayo, kwa sababu hutaki wajisikie vibaya.
Hivyo utawaacha waendelee na mazoea ili wajisikie vizuri na kukupenda.

Njia hiyo inaonekana rahisi na itakayokupa umaarufu kwa sababu ya kupendwa.
Lakini mapenzi ni hisia tu, haitachukua muda kabla watu hao hao wanaokupenda wataanza kukuchukia.
Hapo ni baada ya kuwa wamebaki pale walipo na kushindwa kupiga hatua.

Upande wa pili ni kuheshimiwa.
Kuheshimiwa kunakuja pale unapowawezesha watu kufanya mabadiliko yenye tija kwenye maisha yao.
Awali wanakuwa wabishi kwa sababu hawataki mabadiliko.
Watakuchukia kwa yale utakayokuwa unasimamia.
Lakini mabadiliko watakayoyaona kwenye maisha yao, yatawafanya wakuheshimu sana.

Uzuri wa heshima huwa inadumu muda mrefu. Hata kama mtu hakupendi, akishakuheshimu kwa kile sahihi ulichofanya, ataendelea kukuheshimu kwa muda mrefu.
Heshima ya mtokeo bora unayokuwa umezalisha huwa inadumu kwa muda mrefu. Na hiyo inakupa fursa za kuendelea kufanya makubwa zaidi.

Sisi ni binadamu, inapokuja kati ya kupendwa na kuheshimiwa, huwa ni rahisi kwetu kukimbilia kupendwa.
Hiyo ni kwa sababu tunajali sana wengine wanatuchukuliaje.
Kama unachoangalia ni matokeo ya muda mfupi, utakimbilia kupendwa.
Lakini kama unachoangalia ni matokeo ya muda mrefu, utakimbilia kuheshimiwa.

Ili ukae upande wa kuheshimiwa, unatakiwa kutokujali watu wengine watakuchukuliaje.
Wewe unachopaswa kufanya ni kusimama kwenye yale yaliyo sahihi na kupuuza mengine yote.
Unapaswa kujiwekea viwango vya juu sana, kuwatendea wengine haki na kuzalisha matokeo makubwa.

Watu watakuchukia awali kwa sababu unavuruga mazoea yao.
Lakini watakuheshimu sana baadaye watakapoona matokeo makubwa na tofauti kwao.
Kama utakosa msimamo kwenye yale unayofanya, utakata tamaa haraka kabla hujarika kwenye hatua ya kuheshimika.

Mwanzo wa mabadiliko yoyote yale huwa unachukiwa na wote wanaohusika nayo.
Ni pale matokeo makubwa na mazuri yanapopatikana ndiyo heshima kubwa inapojengeka.
Hilo halitakuwa rahisi, kwa sababu utalazimika kuwasukuma sana watu kutoka kwenye mazoea yao.
Kutakuwa na upinzani mkubwa sana, wapo watakaokukimbia, wengine watasema mambo mengi mabaya kuhusu wewe.
Lakini hupaswi kuruhusu yote hayo yawe na athari kwako.
Hupaswi kuyafanya yakuondoe kwenye njia sahihi.

Kipaumbele chako kama kiongozi siyo kumfurahisha kila mtu, unajua hilo haliwezekani.
Kipaumbele chako ni kuleta mabadiliko chanya, kitu kinachoweza kujidhihirisha, lakini kwa nguvu na gharama kubwa.

Kama kiongozi, wajibu wako ni kuchochea moto kila wakati bila kuchoka.
Hata kama umechoka kiasi gani, hupaswi kuonyesha hilo kwa unaowaongoza.
Hata kama una wasiwasi juu ya jambo lolote, hupaswi kudhihirisha wasiwasi huo.
Wewe ni sura ya mbele ya kile unachosimamia, hivyo unapaswa kuwa kwenye hali sahihi mara zote.
Hili linakupa kazi mara mbili, kitu ambacho siyo kibaya kwa kuangalia matokeo makubwa unayokwenda kuzalisha.

Usihangaike na kupendwa, hizo ni hisia za muda ambazo huwa hazidumu. Maana watu wa kwanza kukuchukia huwa ni wale wale waliokuwa wanakupenda.
Badala yake hangaika na kuheshimiwa, heshima inayotokana na mabadiliko uliyosababisha huwa inadumu milele.

Kama kiongozi unapaswa kusimama kwenye yale yaliyo sahihi, ambayo yanaleta mabadiliko chanya kwenye maisha ya wengine.
Usijali sana wengine wanakuchukuliaje, wewe jua matokeo ya tofauti utakayoyaleta yatakujengea heshima kubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe