3017; Rudia rudia.

Rafiki yangu mpendwa,
Ni kanuni na sheria ya asili kwa vitu kujirudia rudia kwa muda mrefu bila kuchoka wala kukata tamaa.
Jua huchomoza na kutua kila siku, majira ya mwaka hujirudia kila mwaka.
Na hata kwa miili yetu, kula, kujisafisha na mengine muhimu huwa tunayarudia mara kwa mara.

Lakini sasa, cha kushangaza ni namna tunavyotegemea mambo mengine kwenye maisha yetu yatokee baada ya kufanya tu mara moja.
Tunataka kupata matokeo makubwa kwa kufanya kitu mara moja.
Na hilo halipo kabisa, kitu kinachopelekea watu wengi kukwama kupata kile wanachotaka.

Chochote kile unachosema au kufanya, unapaswa kukirudia rudia mara nyingi bila ya kuchoka.
Ni kupitia marudio yasiyo na ukomo ndiyo unakielewa kitu kwa undani na kuweza kukifanya kwa viwango vya juu kabisa.

Ushindi kwenye jambo lolote lile kwenye maisha yako hauanzii kwenye matokeo unayopata, bali unaanzia kwenye msimamo unaokuwa nao kwenye kurudia rudia kwa muda mrefu bila kuchoka.

Mara nyingi sana matokeo huonekana kuja yenyewe tena bila ya kuweka nguvu kubwa.
Lakini unapochunguza kwa kina, ndiyo unagundua nguvu kubwa ya kurudia rudia inayokuwa kwenye kila jambo.

Kama unataka kuhusianishwa na kitu, kiongelee na kukifanya mara kwa mara.
Kama unataka kujulikana kwa kitu fulani, kizungumzie na kukifanya kila siku.
Na kama unataka kuwa mtu pekee anayejulikana kwa kitu fulani, kizungumzie na kukifanya mara nyingi kwenye kila siku yako.

Tafuta ujumbe wako mkuu na mchakato unaoufuata ili kufika kule unakotaka kufika, kisha rudia mara kwa mara bila kuchoka.
Marudio yana nguvu kubwa ya kuleta matokeo yoyote makubwa ambayo mtu anayataka.
Lakini hayapaswi kuwa marudio ya mazoea, bali marudio ya kuboresha kulingana na matokeo yanayopatikana.

Hakuna mafanikio yanayotokana na kufanya kitu mara moja tu.
Huli mara moja ukashiba milele,
Huogi mara moja ukatakata milele.
Hayo ni mambo unayorudia kuyafanya kila siku bila kuchoka, kwa sababu ni muhimu.

Ili uweze kurudia rudia kitu mara kwa mara lazima ukipende na kukikubali sana.
Lazima kiwe ndiyo kipaumbele cha kwanza kwako, kama ilivyo pumzi.
Lazima uwe tayari kufanya bila kuhesabu umefanya mara ngapi.
Ni lazima uzame kwenye kitu na kitu hicho kiwe sehemu ya maisha yako ndiyo utaweza kukirudia rudia bila kuchoka.

Mara nyingi watu wanashindwa kwenye maisha siyo kwa kushindwa kufanya vitu fulani, bali kwa kushindwa kurudia rudia kufanya kwa wingi bila kuchoka.
Binadamu huwa tunachoshwa haraka na marudio ya vitu vilivyo muhimu, lakini huko ndipo penye nguvu ya kupata matokeo makubwa sana.

Mpango kamili wa mafanikio ni;.
Moja, kujua kwa hakika kile hasa unachotaka kupata.
Mbili kujua mchakato unaopaswa kuutumia kupata hicho unachotaka.
Na tatu kukaa kwenye mchakato huo kwa kurudia rudia bila kuchoka.
Kwa kila matokeo unayoyapata, yatathmini kisha boresha yale unayofanya na endelea kufanya bila kuchoka.

Ugumu wa mafanikio haupo kwenye vitu vikubwa unavyopaswa kufanya.
Bali upo kwenye marudio ya vitu unavyopaswa kuvifanya.
Kuwa tayari kurudia rudia kufanya bila kuchoka ili uweze kuyapata mafanikio unayoyataka.

Kadiri unavyojua hili, kulielewa na kulisimamia, ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi kubwa ya kufanikiwa.
Mpango mzima ni kurudia rudia kufanya mambo yote muhimu kwa mafanikio yako bila kuchoka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe