Barua ya I; Tumia muda wako vizuri.
Rafiki yangu Mstoa,
Muda ni rasilimali muhimu sana kwenye maisha yetu.
Ndiyo rasilimali pekee ambayo ukiipoteza huwezi kuipata tena.
Lakini pamoja na upekee huo wa muda, bado watu wengi hawana udhibiti na muda wao, hivyo kuishia kuupoteza.
Unaweza kudhani changamoto ya muda ni kwa zama tunazoishi sasa.
Zama ambazo zina usumbufu wa kila aina unaotokana na maendeleo ya teknolojia tuliyonayo.
Mfano mzuri ni simu janja tunazokuwa nazo kila mahali, ambazo zina mambo mengi ya kutusumbua.
Lakini ukweli ni changamoto ya muda imekuwepo tangu enzi na enzi.
Wakati wa maisha ya Mwanafalsafa wa Ustoa Seneca, muda ulikuwa ni changamoto kwa wengi.
Watu wengi walipoteza muda kwa mambo yasiyokuwa na tija kabisa.
Ni baada ya kuliona hilo, Seneca aliandika barua kwa rafiki yake aliyeitwa Lucilius akimshauri juu ya matumizi mazuri ya muda wake ili aweze kufanya mambo ya msingi kwenye maisha yake.
Kwenye barua hiyo, Seneca ameshirikisha mambo ya msingi sana kuhusu matumizi ya muda ambayo kama tutayazingatia basi tutaweza kutumia muda wetu vizuri na kufanya makubwa kwenye maisha yetu.
Karibu tujifunze misingi ya kistoa ya kutumia muda vizuri.
1. Unayapoteza maisha kwa kupoteza muda (Unakufa kila siku).
Seneca anaeleza kwamba hasara kubwa kwenye kupoteza muda siyo tu muda unaopotea, bali ni maisha unayapoteza.
Kwa sababu muda unaokuwa umeupoteza ni maisha ambayo hujayaishi.
Seneca anaenda mbali zaidi na kusema tunakufa kila siku, kila siku inayopita unazidi kukisogelea kifo chako. Swali ni je unaweza kuwa na nini cha kujivunia kwenye kila siku unayokuwa umeimaliza, ambayo tayari umeshakufa kwa sehemu fulani?
Kuna muda ambao unapotea nje ya uwezo wetu, pale unapojikuta upo kwenye hali fulani zinazopoteza muda.
Lakini kwa sehemu kubwa, muda tunaoupoteza ni kwa uzembe wetu wenyewe.
Kwa kutambua kwamba tunachopoteza siyo muda pekee bali na maisha pia, tunapaswa kuweka tahadhari kubwa kwenye matumizi ya muda wetu.
Usiruhusu muda upotee kwa mambo yasiyokuwa na tija, jua ni kuchagua kuyapoteza maisha yako.
Hatua ya kuchukua;
Kabla ya kutumia muda kwenye jambo lolote, jiulize kama ungekuwa unakufa siku ya leo bado ungelifanya? Kama jibu ni hapana basi ulisifanye, maana ni kupoteza maisha yako.
Nukuu;
‘While we are postponing, life speeds by.’ – Seneca
‘Wakati tunaahirisha mambo, maisha yanatupita.’ – Seneca
2. Upe muda wako thamani.
Huwa tuna tabia ya kupoteza vitu ambavyo havina thamani kwetu.
Na hilo ndiyo linalopelekea watu wengi kupoteza muda kwenye maisha yao, kwa sababu wanashindwa kuupa thamani.
Kwa kujua kwamba unakufa kila siku, kwa kujua kwamba muda ukishapita hauwezi kurudi tena, tunapaswa kuona jinsi ulivyo na thamani kubwa kwetu.
Na hapo ndipo Seneca anasisitiza kwamba tujue thamani kubwa ya muda na tushikilie vizuri kila saa la muda wetu kwani hatuwezi kumudu kulipoteza.
Kwa kuhakikisha unakamilisha majukumu yako yote ya siku, huwi na wasiwasi kuhusu siku inayokuwa inafuata.
Seneca anasema tunajichanganya sana tunapoangalia kifo kama kitu kinachokuja, wakati kifo ni kitu ambacho kimeshapita.
Muda tuliobaki nao unathamani kubwa sana kwa sababu uliopita umeshapita, hakuna namna tunaweza tena kuutumia.
Hatua ya kuchukua;
Kila siku orodhesha majukumu yako muhimu ya kufanya kisha yafanye hayo kama ulivyopanga bila kupoteza muda kwenye majukumu mengine. Ukikamilisha muhimu ya leo, kesho itakwenda vizuri.
Nukuu;
‘Lay hold of to-day’s task, and you will not need to depend so much upon to-morrow’s.’ – Seneca
‘Shikilia majukumu ya leo na hutajitaji kutegemea sana ya kesho.’ – Seneca
3. Muda ndiyo kitu pekee tunachomiliki.
Huwa tunahangaika na mali nyingi hapa duniani, lakini zote tunaziacha baada ya kufa.
Alama kubwa tunayokuwa tumeiacha hapa duniani ni jinsi ambavyo tumetumia muda wetu.
Asili imewapa watu wote muda sawa, ndiyo kitu pekee ambacho hakuna mtu anaweza kukunyang’anya kama upo hai.
Watu wanaweza kukupotezea muda, lakini hawawezi kukunyang’anya kama wanavyoweza kufanya kwa mali nyingine.
Seneca anasema watu wengi ni wajinga kwa sababu wanapoteza muda wao wa thamani kuhangaika na mali zisizokuwa na thamani sawa na muda wao.
Anaeleza deni la muda ni deni ambalo hakuna mtu yeyote anayeweza kulilipa.
Kwa kujua haya tunapaswa kuupa muda thamani yake kwa kuumiliki vyema na kuutumia kwa tija.
Hatua ya kuchukua;
Miliki muda wako vizuri kwa sababu ndiyo kitu pekee ambacho huwezi kunyang’anywa.
Usipoteza muda wako wa thamani kupata vitu ambavyo haviendani na thamani ya muda huo.
Nukuu;
‘Nothing, Lucilius, is ours, except time.’ – Seneca.
‘Lucilius, muda ndiyo kitu pekee tunachomiliki.’ – Seneca
4. Huwezi kuepuka kupoteza muda kabisa, ila ni vizuri kujua.
Huwa wanasema upumbavu ni kutokujua, ila kudhani unajua. Wakati ujinga ni kutokujua na kujua hujui.
Inapokuja kwenye muda, Seneca anatuambia tatizo siyo kupoteza muda, bali tatizo ni kupoteza muda huku ukiwa hujui kama unapoteza muda.
Seneca anasema hata yeye alikuwa anapoteza muda, ila alijua kabisa kwamba anapoteza muda. Kwa maneno mengine hakuwa anajidanganya au kujifariji.
Upotevu mkubwa wa muda kwenye maisha ni ule ambao mtu hujui kama anapoteza muda.
Anakuwa anajiendea tu na maisha akidhani kila kitu kipo sawa, ni mpaka anapokuwa amechelewa sana ndiyo anakuja kuzinduka kwamba ameshayapoteza maisha yake.
Hatua ya kuchukua;
Pangilia muda wako kwa mambo muhimu na fuata mpango ulioweka.
Na pale inapotokea umepoteza muda, jua wazi kwamba umepoteza muda na hilo litakuumiza na kukufanya uwe makini zaidi na muda uliosalia nao.
Usijidanganye, ona wazi kama unapoteza muda ili uweze kuchukua hatua stahili.
Nukuu;
‘I cannot boast that I waste nothing, but I can at least tell you what I am wasting, and the cause and manner of the loss…’ – Seneca
‘Siwezi kujisifia kwamba sipotezi muda, lakini angalau naweza kukuambia ni kiasi gani cha muda napoteza na ninaupoteza kwa namna gani….’ – Seneca
5. Anza kujali muda wako mapema.
Sote tunajua muda wetu hapa duniani una ukomo, lakini inashangaza jinsi ambavyo watu huwa wanaona bado wana muda mwingi sana.
Watu wakiwa watoto na vijana, wanajiona wana muda mwingi sana.
Ni mpaka wanapofika kwenye uzee ndiyo wanagundua hawana tena muda, huku wakiwa hawajayaishi maisha yako.
Seneca anasema hujachelewa kama bado upo hai, una muda unaoweza kuutumia. Muhimu ni kujua muda ulionao siyo mwingi na hivyo huwezi kumudu kuupoteza.
Anza mara moja kujali muda wako ili uweze kuutumia vizuri kwa mambo yenye tija kwako.
Wakati wowote unapotambua thamani ya muda wako, anza kuutumia vizuri, usijiambie bado ni mapema na muda bado upo.
Hatua ya kuchukua;
Anza sasa kujali na kutumia vizuri muda wako.
Usiangalie huko nyuma umeshapoteza kiasi gani, anza kutumia vizuri muda ulionao sasa.
Usijidanganye bado ni mapema na una muda mwingi, hakuna mwenye uhakika na kesho.
Nukuu;
‘Of that which remains at the bottom, the amount is slight, and the quality is vile.’ – Seneca
‘Kile kinachobaki mwishoni, kiasi huwa ni kidogo na kiwango huwa ni kibaya.’ – Seneca
Tunza na tumia vizuri muda wako, maana hayo ndiyo maisha yako.
Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr. Makirita Amani.
Muda ndiyo maisha, nikiupoteza nimepotezea maisha yangu.
LikeLike
Huo ndiyo ukweli.
LikeLike
Seneca anasema hujachelewa kama bado upo hai, una muda unaoweza kuutumia. Muhimu ni kujua muda ulionao siyo mwingi na hivyo huwezi kumudu kuupoteza.
LikeLike
Hakika
LikeLike
Mtu yeyote anayekupotezea muda anakupotezea sehemu ya maisha yako. Chakushangaza ni kwamba eti kila siku tunakufa kila siku, kila siku inayopita tunazidi kusogelea kifo. Watu wengi hatuelewi.Nitaiishi misingi ya ustoa. Asante sana Kocha.
LikeLike
Vizuri, tuishi kistoa na tutayavuka mengi.
LikeLike
tunakufa kila siku.
swali ni je unaweza kuwa na nini cha kujivunia kwenye kila siku yako ambayo kimsingi unakuwa umesha kufa kwa sehemu fulani.
LikeLike
Hilo ndiyo swali la msingi kabisa kwa kila mtu kulijibu.
LikeLike
Asante kocha juzi nilikutana na taarifa fulani kuhusu nyuki kwamba anaishi takribani siku 40 tu na katika siku hizo 40 anatengeneza kijiko kimoja cha asali.Habari hii ilinitafakarisha sana juu ya matumizi yangu ya muda.Ama kweli muda ni maisha sipaswi kuupoteza.
LikeLike
Asante sana kwa kushirikisha mfano huu wa nyuki, kuna funzo kubwa sana hapo kuhusu maisha na muda.
LikeLike
Muda wangu ndio maisha yangu,nautumia muda wangu vizuri ili niyaishi maisha yangu vizur
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike
Kumbe kuangaika na ambavyo tayari ninavyo ni ujinnga bali kufanya zaidi kupata ambavyo sina ili kutumia uwezo wng wa ndani kwa usahihi na kufanya makubwa.
Natunza muda na kuupa thamani zaidi
Asante mstoa makirita.
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike
Nimeupoteza muda wangu huko nyuma kwa sbabu ya ujinga, hivyo kwa sbabu nimeshajua umuhimu na Tathamni kubwa muda wangu Ulionao, nitajitahidi Kadri ya uwezo wangu kutokuwa mpumbavu wa kutouthamini muda wangu kwa kuendeleza vitu vya kijinga na Visivyo na tija. Kwani muda na maisha ni kitu kimoja
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike
Kuanzia sasa sitapoteza muda wangu tena
LikeLike
Vizuri.
LikeLike
Muda ndiyo kila kitu kwangu, hakika siitaji kupoteza muda wangu, Asante sana kwa makala hii ya ustoa.
LikeLike
Vizuri sana.
LikeLike