3062; Hakuna mjadala.

Rafiki yangu mpendwa,
Fikiria kuna kitu muhimu sana ambacho unataka kununua.
Unaongea na muuzaji wa kitu hicho na anakupa bei.
Mnajadiliana kwenye bei na kufikia muafaka kati yako na muuzaji.

Unaondoka kwenda kuchukua fedha za kulipia kama mlivyokubaliana.
Unarudi ukiwa na kiasi cha fedha kilichokamilika kulingana na makubaliano.
Lakini muuzaji anakuambia hataweza kukuuzia kwa bei hiyo mliyokubaliana, maana amegundua amekupa kwa bei ya chini sana.

Wewe unakitaka sana kitu hicho, ni muhimu mno kwako.
Hivyo mnajadiliana bei mpya ya kukipata.
Unatoka tena mwenda kuongeza fedha.
Unarudi kwa ajili ya kumamilisha mauzo.
Lakini tena muuzaji anakuambia hataweza kukuuzia kwa bei hiyo, ni ndogo sana.

Mpaka hatua hiyo utakuwa tayari utakuwa umepatwa na hasira.
Utaona muuzaji amekosa umakini au hayupo tayari kuuza kile anachouza.
Mwisho kabisa utaamua kuachana naye na kwenda kununua kwa mtu mwingine ambaye amejipanga vizuri.

Utakuwa na haki kabisa ya kumshangaa muuzaji anayebadilika kila wakati, lakini mbona huwa hujishangai wewe mwenyewe?
Kwa sababu tabia aliyokuonyesha muuzaji ya kubadilika badilika kwenye makubaliano, umekuwa unaifanya kwenye maisha yako mwenyewe.
Unaweza kukataa na kujiambia wewe siyo kigeu geu.

Lakini twende tena kwenye mfano ili tuelewane vizuri.
Mara ngapi umejiwekea mpango wa kukamilisha jukumu fulani na kuliwekea kabisa muda wa kulikamilisha.
Lakini wakati wa kukamilisha jukumu hilo unapofika, unabadilika.
Unafungua tena upya mjadala wa iwapo ufanye au usifanye kitu hicho.

Unapoteza muda na nguvu zako nyingi kwenye mijadala isiyo na mwisho.
Kitu pekee ambacho hupati ni matokeo uliyotegemea kwa kufanya kitu hicho.
Hivyo ndivyo umekuwa unaenda kwenye sehemu maeneo mbalimbali ya maisha yako, unapanga vitu vya kufanya, lakini wakati wa kuvifanya unapofika, badala ya kufanya, unafungua upya mjadala.

Ili uweze kufanikiwa, unahitaji kuwa na uwajibikaji wa hali ya juu sana.
Unapopanga kitu cha kufanya, wakati unapofika unapaswa kufanya na siyo kufungua upya mjadala.
Umeshajadiliana na wewe mwenyewe wakati wa kupanga, inapofika wakati wa kutekeleza, tekeleza kama ulivyopanga.

Kamwe usiendekeze mijadala mipya kwenye mipango ambayo tayari umeshaiweka na kukubaliana nayo.
Mara zote fuata mpango wako kama ulivyouweka.
Hata kama unaona kuna maboresho ya kufanya, tekeleza kwanza kama ulivyopanga na utarekebisha baada ya kuwa umeshafanya.

Kuna sababu kwa nini ulipanga jinsi ambavyo umepanga.
Mara nyingi wakati wa kupanga unakuwa na utulivu na akili yako inafikiri vizuri.
Lakini wakati wa utekelezaji unakosa utulivu na hisia zinatawala zaidi akili yako.
Kwa hisia ni rahisi kubadili maamuzi ya awali, lakini mara zote mabadiliko hayo yanakuwa siyo sahihi.

Ukishaweka mipango, kinachofuata ni kuitekeleza kama ulivyopanga.
Hakuna kufanya mabadiliko yoyote kabla hujaanza kufanya.
Heshimu mipango unayojiwekea wewe mwenyewe, utajiheshimu na kuweza kuzalisha matokeo mazuri na makubwa.

Kubadili mipango kila mara, hasa wakati wa utekelezaji ni aina nyingine ya uvivu na uzembe ambayo inakukwamisha sana kupiga hatua.

Panga na kufanya kama ulivyopanga.
Usiruhusu mianya ya kufungua upya mjadala kwenye jambo ambalo umeshaliamulia.
Hata kama unaona maamuzi uliyoweka yana makosa, anza kutekeleza kwanza kabla hujabadili makosa hayo.

Ni muhimu sana ujenge kwanza nidhamu ya kufanya kama ulivyopanga, kwani hiyo itakuwezesha kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

Ukishaamua, tekeleza kama ulivyoamua.
Usikubali kufungua tena mjadala na wewe mwenyewe juu ya maamuzi hayo.
Hisia zako zina nguvu kubwa ya kukudanganya, hasa inapofika wakati wa kuchukua hatua.
Usiendekeze mijadala, kuwa mtu wa kuchukua hatua.
Hata kama utakosea, ni bora ukosee kwa kufanya kuliko kuendelea na mijadala isiyo na ukomo.

Matokeo yanazalishwa kwa kufanya na siyo kwa mijadala.
Kuwa mfanyaji mzuri na utaweza kupiga hatua kubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe