3072; Usilale.

Rafiki yangu mpendwa,
Tuna maadui wengi sana ambao wanapambana kwa kila namna kutuzuia tusipate mafanikio makubwa tunayoyataka.

Maadui wanaokuwa na nguvu sana siyo wa nje, bali wale wa ndani yetu.
Hao ni maadui wanaokuwa na nguvu kwa sababu wanatujua kiundani.

Uvivu, uzembe na mazoea ni maadui ambao wengi hawajui madhara yao kwenye mafanikio yao.
Wamekuwa wanafanya kazi kwa chini chini kuhakikisha mtu hapati mafanikio makubwa anayoyataka.

Halafu kuna adui mwingine mkubwa sana ambaye amekuwa kikwazo sana.
Adui huyo ni kulala.
Adui kulala tunayemzungumzia hapa, siyo kule kulala kitandani, bali kulala kurudi nyuma pale mtu anapokuwa ameshapanga kusonga mbele.

Ni mara ngapi umesoma kitabu au kupata mafunzo au wazo lolote na kujiambia kuanzia sasa nakwenda kubadilika?
Unajiambia utaamka mapema, utapangilia muda wako wote na utaweka juhudi kubwa kwenye kazi bila kupoteza muda na kuahirisha mambo.

Siku chache za mwanzoni unatekeleza kama ulivyopanga.
Lakini siku siyo nyingi unakuwa umerudi iwenye mazoea yako ya nyuma.
Hapo ndiyo unakuwa umerudi kulala, baada ya kuwa umeamka kwa muda mrefu.

Leo tunakwenda kujifunza kanuni rahisi sana ambayo itakuzuia usirudi kulala pale unapokuwa umeamka.

Kanuni hiyo ina hatua muhimu tatu za kuzingatia mara zote ili mtu usirudi kulala.

Hatua ya kwanza ni hamasa ambayo ndiyo inakuamsha.
Sisi binadamu ni viumbe wa kihisia na hivyo maamuzi yetu yote huwa tunayafanya kwa kusukumwa na hisia.
Mabadiliko yoyote kwenye maisha yetu huwa yanaanzia kwenye hamasa ambayo mtu unakuwa umepata.
Inaweza kuwa hamasa chanya ya tamaa ya kupata vitu fulani vizuri au hamasa hasi ya hofu ya kukosa au kupoteza vitu vizuri.

Hatua ya pili ni nidhamu ambayo ndiyo inakufanya uendelee kuwa macho.
Baada ya hamasa kukuamsha, nidhamu ndiyo inayokufanya uendelee kukaa kwenye yale uliyopanga kufanya.
Kukosekana kwa nidhamu imekuwa chanzo kikubwa cha watu kurudi kulala muda mfupi baada ya kuamshwa na hamasa.
Wengi hutegemea hamasa ndiyo iwasukume kila wakati, kitu ambacho hakipo.
Hamasa inawasha tu moto, nidhamu ndiyo inauchochea moto huo.
Kukosa nidhamu kumekuwa kikwazo cha wengi kukaa kwenye kitu kwa muda mrefu.

Hatua ya tatu ni kusudi ambalo ndiyo linakuzuia usirudi kulala.
Kusudi linakupa msukumo mkubwa sana wa kuendelea hata pale mambo yanapokuwa magumu na kuonekana kushindwa.
Kadiri kusudi ambalo mtu anakuwa nalo linakuwa kubwa, ndivyo msukumo wa kuendelea kulipambania unavyokuwa mkubwa pia.
Huwa kuna kauli inayosema ukiwa na KWA NINI KUBWA, utaweza kuvumilia chochote ili kuitimiza.
Wengi huwa wanapata hamasa ya kubadilika, ila wanakuwa hawajui kwa nini wanadilike.
Wanakuwa hawajajua kwa nini wateseke na mabadiliko wanayoanzisha.
Hivyo wanapokutana na mateso, huwa wanaacha haraka sana, wanarudi kulala.
Kusudi ni muhimu sana kukuzuia usirudi kwenye uvivu, uzembe na mazoea ya nyuma.

Kwa zama tunazoishi sasa, hakuna uhaba wa hamasa.
Hamasa zinapatikana kwa wingi na kila mahali.
Lakini pamoja na wingi huo wa hamasa, bado watu wengi hawafanikiwi.
Na sababu ni kukosekana kwa vitu hivyo vingine viwili.
Watu wanakosa nidhamu kali sana ya kuamua na kufanya kwa msimamo bila kuacha.
Na zaidi, wanakosa kusudi la kuwasukuma kuendelea na mabadiliko licha ya magumu wanayokabiliana nayo kwenye safari.

Haya yote unayajua, ila huenda hujawahi kuyaunganisha kwa pamoja hivi na ukaona nguvu yake.
Hivyo yalete pamoja na kila siku hakikisha unayafanyia kazi.
Hamasa inakuamsha kutoka kwenye usingizi wa uzembe, uvivu na mazoea.
Nidhamu inakufanya uendelee kuwa macho, kwa wakati wote kuendelea na mabadiliko uliyoanzisha.
Na kusudi linakuzuia usirudi kwenye usingizi wa uzembe, uvivu na mazoea hasa pale unapokutana na magumu na changamoto mbalimbali.

Kama hutaki kulala kwenye hii safari ya mafanikio, hakikisha unatumia HAMASA, NIDHAMU NA KUSUDI kubadilika na kudumu kwenye mabadiliko hayo bila kurudishwa nyuma na kitu chochote.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe