3087; Ni vita kubwa.

Rafiki yangu mpendwa,
Msimu wa HAPANA ambao tupo ni moja ya misimu migumu sana kwenye maisha yetu.
Hiyo ni kwa sababu kupanga kusema HAPANA ni rahisi, lakini kumwangalia mtu usoni na kumwambia HAPANA ni zoezi gumu sana, ambalo wengi wanalishindwa.

Watu wengi wanakwama kwenye kusema HAPANA kwa sababu wanataka wamkatalie mtu kitu lakini wawaache watu hao wakiwa na furaha pia.
Ili kutimiza hilo, wamekuwa wanawaambia watu HAPANA ambazo ni nyepesi, zikiambatana na maelezo mengi yasiyokuwa muhimu.

Kinachotokea ni HAPANA zao zinakosa nyuvu na kujikuta wameshawishika na kukubali kitu ambacho walipanga kukikataa.

Kila mara unaposema NDIYO kwenye jambo ambalo ulipanga kusema HAPANA, unashusha hadhi na thamani yako. Unajidharau na kujiona huna mamlaka juu ya maisha yako. Hilo linafanya HAPANA yako nyingine iwe ngumu zaidi.

Zoezi la kusema HAPANA ni vita kubwa sana.
Kwa sababu unawakatalia watu kitu ambacho tayari walishajipanga kukipata kutoka kwako.
Hawatakubaliana na wewe kirahisi kwenye hilo.

Ili HAPANA yako iwe na nguvu, inapaswa kuelezwa kwa wazi na isiambatane na maelezo mengi.
Hilo linataka uwe tayari kuonekana una roho mbaya na hujali.
Ni vyema uwe tayari kupokea yote ambayo watu watayaleta kwako kwa sababu umewakatalia.

Usigeuze HAPANA yako kuwa NDIYO kwa sababu tu unataka kuwafurahisha watu wengine.
Huwezi kumfurahisha kila mtu na pia siyo wajibu wako kufanya hivyo.
Ni wajibu wa kila mtu kujifurahisha mwenyewe kwenye maisha yake.

Watu wanaokujali na kukuheshimu, watakubaliana na HAPANA yako na kuendelea kushirikiana na wewe kwenye mambo mengine muhimu na yanayoendana na NDIYO zako.
Lakini watu wasiokujali wala kukuheshimu, ambao wanataka kukutumia kwa manufaa yao, watakataa HAPANA zako na kulazimisha wapate kile wanachotaka wao bila kujali kuhusu wewe.

Hapo ndipo ilipo vita niliyokuambia,
Kwa sababu unahitaji kupambana na wote wanaokataa mipaka unayoweka kwenye maisha yako.
Kusema HAPANA ni kuweka mipaka na mtu anayekataa HAPANA zako ni sawa na anafanya uvamizi kwenye mipaka yako, kitu ambacho ni vita kubwa.

Unaposema HAPANA, imaanishe kweli na isimamie. Usijali sana upande wa pili umechukuliaje HAPANA yako, unachohitaji ni kulinda mipaka yako isishambuliwe na matakwa ya wengine.

Acha kutaka kuonekana mwema kwa kila mtu.
Acha kutaka kumfurahisha kila mtu.
Acha kusema NDIYO kwenye mambo ambayo ndani yako unajua yanatakiwa kuwa kwenye HAPANA.
Ukiweza kuishinda vita hii kubwa ambayo silaha yake ni neno HAPANA, utaweza kuweka mipaka sahihi kwenye maisha yako.

Mara zote kumbuka upo kwenye vita ya kulinda muda wako, nguvu zako na umakini wako.
Ukiwa mwepesi mwepesi utaburuzwa sana na wengine kwenye hayo maeneo matatu muhimu.
Matokeo yake ni unajikuta kila siku unachoka sana, lakini ukiangalia hakuna makubwa uliyokamilisha.
Matumizi sahihi ya neno HAPANA yatakuwa mkombozi mkubwa kwako.

Hii vita ingekuwa rahisi, kila mtu angekuwa ameshinda kwenye eneo hilo.
Siyo vita rahisi ndiyo maana wengi wanashindwa na kurudi kwenye maisha yao ya mazoea.
Wewe usikubali kurudi nyuma, songa mbele kama ulivyopanga, tumia neno HAPANA kwa usahihi na msimamo ili uweze kulinda yale muhimu zaidi kwako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe