3102; Ni kuwa bora, siyo kufurahia tu.

Rafiki yangu mpendwa,
Hakuna kipindi ambapo maarifa ya mafanikio yamekuwa yanapatikana kwa wingi na urahisi.

Lakini pia ndiyo wakati ambao watu wanaopata mafanikio makubwa wanayoyataka wamekuwa wachache sana.

Ni jambo la kushangaza, iweje maarifa ya mafanikio kupatikana kwa wingi na urahisi, lakini wanaofanikiwa kuwa wachache?

Zipo sababu nyingi, lakini moja kubwa ni mtazamo wa mtu anayejifunza. Watu wengi huwa lengo lao la kujifunza ni kufurahia. Hivyo wanajifunza vile vitu wanavyovitaka tu. Wanapokutana na kitu ambacho kinawataka wabadilike kwa namna fulani, wanaachana nacho.

Watu wachache huwa lengo lao la kujifunza ni kuwa bora. Hawa wanajifunza yote wanayokutana nayo na kuwa tayari kubadilika pale inapohitajika kufanya hivyo.
Ni watu hao wachache ndiyo wanaopata mafanikio makubwa.

Jipime wewe mwenyewe unaingia kwenye kundi lipi kati ya hayo mawili.
Je unajifunza ili kufurahia au kuwa bora?
Ni kujifunza kuwa bora ndiko kwenye fursa ya wewe kupiga hatua zaidi.

Kwenye kujifunza ili kufurahia unaishia kujifunza yale tu ambayo tayari unayajua na kukubaliana nayo. Unakuwa hukutani na ukweli ambao unatikisa mtazamo mzima ulionao.

Kwenye kujifunza ili kuwa bora unajifunza mambo mapya ambayo yanakutaka kubadilika kwa kiasi kikubwa.

Kwa kila unachojifunza, jiulize matokeo ya mwisho yamekuwa nini, umefurahia tu au umekuwa bora?
Anzia hapo ili uweze kufanya makubwa zaidi kwenye maisha yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe