Barua ya X; Kuishi maisha yako.
Rafiki yangu Mstoa,
Umekuwa ni wimbo wa zama hizi kila mtu kutaka kuwa huru kuyaishi maisha yake vile anavyotaka mwenyewe.
Lakini je ni wangapi wanaoweza kweli kuyaishi maisha yao kwa namna hiyo?
Ni wangapi wenye nidhamu ya kuweza kuyaishi maisha yao wenyewe kwa kufuata misingi sahihi?
Japo huwa ni ushauri mzuri kwa watu kuwa huru kuyaishi maisha yao wenyewe, kwa wengi hilo linaweza kuwa hatari kubwa kwao. Kwa kujaribu kuyaishi maisha yao wenyewe, wanaishia kuyaharibu kuliko walivyokuwa wanaishi maisha yao chini ya maelekezo ya wengine.
Tumekuwa tunaona hili kwenye eneo la kuajiriwa na kujiajiri. Wapo watu wengi ambao huona wanakosa uhuru kwenye kuajiriwa na hivyo kuamua kuacha ajira na kwenda kujiajiri. Lakini matokeo yake mambo yanakuwa magumu kiasi cha kulazimika kurudi tena kwenye kuajiriwa.
Hao ni watu waliotumia vibaya nafasi ya kuishi maisha yao, kabla hawajawa na misingi sahihi ya kufanya hivyo.
Mwanafalsafa Seneca aliona changamoto hiyo miaka mingi iliyopita, ya baadhi ya watu kuona wanataka kuwa huru kuyaishi maisha yao wenyewe na mwishowe wanaishia kuyaharibu.
Kwenye barua yake ya 10 aliyomwandikia rafiki yake Lucilius, alieleza kwa kina dhana hiyo, akionyesha wakati gani mtu anaweza kuishi maisha yake mwenyewe na wakati gani hawezi.
Karibu tujifunze hayo kutoka kwenye barua hiyo.
1. Usiweke imani yako kwa mtu yeyote.
Seneca anaanza kwa kumwambia rafiki yake kwamba msimamo wake ni ule ule, kwamba mtu anapaswa kuepuka kundi la wengi, anapaswa kuwaepuka wachache na hata kumwepuka mtu mmoja mmoja.
Lakini pia mtu anapaswa kuwa na tahadhari hata pale anapokuwa peke yake.
Hili ni muhimu sana kuelewa na kuzingatia, kwa sababu tunaweza kuweka imani zetu kwa watu wasio sahihi, hata sisi wenyewe.
Kwa uhakika ni hatupaswi kuweka imani zetu kwa watu bali kwenye misingi sahihi. Na misingi hiyo ndiyo itakayotuwezesha kufanya yaliyo sahihi.
Hatupaswi kujiamini hata sisi wenyewe, kama hatufuati misingi hiyo sahihi.
Hatua ya kuchukua;
Usiweke imani yako kwa watu, bali kwenye misingi. Chagua misingi sahihi itakayokupa kile unachotaka na ifuate hiyo kwa uhakika.
Nukuu;
“I know of no one with whom I should be willing to have you shared.” – Seneca
“Simjui mtu yeyote nitakayekuwa tayari kukuruhusu ushirikiane naye.” – Seneca
2. Nyakati za kuepuka kuwa peke yako.
Imekuwa ikielezwa umuhimu wa mtu kupata muda wa kukaa peke yake na fikra zake ili kuyatafakari maisha yake na kuchukua hatua sahihi.
Lakini siyo mara zote mtu anaweza kuwa salama kuwa peke yake.
Seneca anasema watu walio kwenye majonzi au hofu huwa hawapaswi kukaa peke yao, kwa sababu wanaweza kufikiri na kufanya mambo yasiyokuwa sahihi.
Faida ambayo mtu anaweza kuipata kwa kuwa peke yake, inageuka kuwa hatari pale fikra zake zinapokuwa siyo sahihi.
Hatua ya kuchukua;
Epuka kukaa peke yako pale fikra zako zinapokuwa hazipo sawa. Kama una hali ya majonzi, huzuni, msongo, sonona au hasira, kaa na watu wa karibu ambao wanakuelewa na wanaoweza kukusaidia kuvuka hali hizo.
Nukuu;
“No thoughtless person ought to be left alone; in such cases he only plans folly, and heaps up future dangers for himself or for others.” – Seneca
Mtu asiye na fikra sahihi hapaswi kuachwa peke yake, kwa sababu kwenye hali hiyo ataweka mipango mibaya itakayokuwa hatari kwake na kwa wengine.” – Seneca
3. Mara zote kuwa imara ili uweze kuishi maisha yako.
Baada ya kuona jinsi ambavyo siyo rahisi kuwaamini wengine, na pia ilivyo hatari mtu kukaa peke yake kama fikra zake siyo sahihi, unaweza kujiuliza maisha yataendaje?
Na hapo Seneca anatuelekeza kwamba mara zote tunapaswa kuwa imara, kwa kusimamia misingi sahihi, ili tuweze kujiamini sisi wenyewe na kuyaishi maisha yetu.
Seneca anasisitiza kwamba unapaswa kuyaishi maisha yako kwa namna ambayo wewe mwenyewe ndiye unakuwa mtu sahihi wa kushirikiana naye na kumtegemea.
Hilo litataka muda wote uhakikishe una fikra sahihi.
Na fikra sahihi zinaanzia kwenye misingi sahihi unayokuwa nayo.
Hatua ya kuchukua;
Ishi kwa misingi sahihi ili muda wote uweze kuwa na fikra sahihi, kitu kitakachofanya wewe mwenyewe uwe sahihi kwako.
Nukuu;
“These words did not come from the edge of the lips; these utterances have a solid foundation. This man is not one of the many; he has regard for his real welfare.” – Seneca
“Haya maneno hayajatoka tu kwenye midomo, ni maneno yanayotoka kwenye msingi imara. Huyu mtu siyo mmoja kati ya walio wengi, bali anajali ustawi wake.” – Seneca
4. Omba upate akili sahihi na afya njema.
Seneca anamweleza rafiki yake kwamba anaweza kuwa na maombi mengi kwenye sala anazofanya.
Lakini maombi ya msingi kabisa anayopaswa kuwa nayo ni ya kuwa na akili sahihi na afya njema.
Anasisitiza maombi ambayo mtu anafanya yanapaswa kumjenga kiroho na kimwili.
Na haitishi tu kuomba mara moja, bali unapaswa kuomba kwa kurudia rudia na kwa msimamo.
Na muhimu zaidi, unapaswa kuomba kwa ujasiri, ukijua unachoomba siyo cha mtu mwingine, bali chako mwenyewe.
Hatua ya kuchukua;
Weka juhudi kubwa kuhakikisha akili, roho na mwili wako vipo sawa. Ni usawa kwenye maeneo hayo ndiyo utakufanya uwe mtu sahihi kwako mwenyewe.
Changamoto kwenye eneo lolote katika hayo matatu itafanya uwe mtu hatari kwako mwenyewe na kwa wengine.
Nukuu;
“Pray for a sound mind and for good health, first of soul and then of body. And of course you should offer those prayers frequently.” – Seneca
“Omba kwa ajili ya akili sahihi na afya njema, kwanza ya roho na kisha ya akili. Na hakikisha unaomba mara kwa mara.” – Seneca
5. Omba kile unachoweza kujivunia.
Seneca anamaliza barua hii kwa kumweleza rafiki yake kwamba anapaswa kuomba kile ambacho anajivujia, ambacho hawezi kuwa na aibu nacho kwa wengine.
Seneca anasisitiza ni ujinga pale mtu anaponong’oneza maombi yake na kama mtu mwingine akiyasikia anakaa kimya.
Unapaswa kuomba kile ambacho unajivunia kuwa nacho, ambapo hujali hata kama kuna mtu mwingine anasikia.
Hapaswi kuonea aibu kile unachotaka kwenye maisha yako, kama ndiyo kitu sahihi kwako.
Hatua ya kuchukua;
Kitu chochote kile unachokitaka kwenye maisha yako, jivunie kuwa nacho. Usione aibu kuonekana na wengine unataka kitu hicho. Huwezi kupata kitu ambacho huwezi kujivunia kuwa nacho. Kuwa tayari kueleza wazi kile unachotaka kwa watu wote bila kuogopa wala kuona aibu.
Nukuu;
“Live among men as if God beheld you; speak with God as if men were listening” – Seneca
“Ishi na watu kama vile Mungu anakuoja; ongea na Mungu laka vile watu wanakusikia.” – Seneca
Rafiki yangu Mstoa, tumejifunza mengi kupitia barua hii, ambayo tunapaswa kuyazingatia kwenye kuyaishi maisha yetu.
Jambo la msingi kabisa ni kuwa na misingi sahihi ambayo tunaifuata na mara zote kufanya kile kilicho sahihi.
Kwa kuzingatia hayo, tutakuwa watu sahihi kwetu sisi wenyewe.
Hivyo pia ndivyo tunavyopaswa kuyaishi maisha yetu ya mafanikio.
Kwa mafanikio yoyote tunayoyataka, hatupaswi kuweka imani na matumaini kwa watu au kwetu wenyewe, bali tunapaswa kukaa kwenye misingi sahihi.
Bila misingi sahihi mtu utahangaika sana, lakini utaishia kushindwa.
Lakini unapokuwa na misingi sahihi na kuifuata mara zote, ushindi ni wa uhakika kwako.
Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr Makirita Amani.
Asantee kwa makala NZURI nimejifunza namna ya kuishi kwa kufuata misingi sahihi kwa KWELI nazidi kujifunza sana na kuimariki nitaongzwa na misingi imara sitakubali mtu aniendeshe.asantee.
LikeLike
Safi sana.
LikeLike
Asante kocha nitaomba kile ninachoweza kujivunia.
LikeLike
Vizuri
LikeLike
Asante kocha,Nitaakikisha ninaishi kwenye misingi sahihi na kuifuata mara zote,na ushindi utakuwa wa uhakika kwangu.
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike
Asante Kocha,
Ili nipate mafanikio sitaweka imani na matumaini kwa wengine au kwangu mwenyewe, bali nitakaa kwenye misingi sahihi.
LikeLike
Vizuri
LikeLike
Kitu chochote kile unachokitaka kwenye maisha yako, jivunie kuwa nacho. Usione aibu kuonekana na wengine unataka kitu hicho. Huwezi kupata kitu ambacho huwezi kujivunia kuwa nacho. Kuwa tayari kueleza wazi kile unachotaka kwa watu wote bila kuogopa wala kuona aibu.
LikeLike
Ndiyo
LikeLike
Sitaweka Imani na matumaini kwa wengine ao kwangu mwenyewe nitaishi kwa misingi sahihi pia sitasikia aibu kwa watu kwa kuwaambia kile ninacho kitaka kwa
MBA nataka kuwa Bilionea na najivunia hilo Asante sana kocha
LikeLike
Vizuri
LikeLike