3174; Kitakachokufanya uache.

Rafiki yangu mpendwa,
Hadithi ambazo huwa tunajiambia sisi wenyewe, kuhusu sisi, zina nguvu kubwa sana kwenye maisha yetu.
Na hadithi hizo huwa zinatokana na ushahidi wa yale ambayo huwa tunayafanya, hasa tunapokuwa peke yetu.

Iko hivi rafiki, kitakachoamua mafanikio kwenye maisha yako siyo kile unachofanya mbele ya wengine, bali kile unachofanya ukiwa peke yako.

Watu wengi wanapokuwa mbele ya wengine, huwa wanaigiza kuwa watu wa aina fulani.
Lakini wanapokuwa wao wenyewe, wanakuwa watu wa tofauti kabisa.
Wanadhani wanawadanganya wengine kuhusu wao, kumbe wanajidanganya wao wenyewe.

Hiyo ni kwa sababu hadithi wanayojiambia wao wenyewe, kuhusu wao, inaathiriwa na kile wanachofanya wakiwa peke yao.

Kwa kipindi ambacho nimekaa kwenye hii tasnia ya kuandika, kufundisha na kukochi, nimeona watu wengi ambao walikuwa wakisema wanayataka mafanikio makubwa kwenye maisha yao.
Wanaeleza wazi kwamba wamejitoa hasa kuyapata mafanikio hayo na watapambana mpaka kuyapata.
Wanatoa ahadi na viapo mbalimbali tunavyopeana.
Wanaonekana kweli tupo nao pamoja kwenye hii safari.

Lakini kidogo kidogo unawaona wakipunguza kasi kwenye safari na mchakato mzima.
Halafu ghafla wanaachana kabisa na hiyo safari.

Mwanzo nilikuwa sielewi, inakuwaje huyu mtu ambaye alionekana wazi ni mwenzetu amekuja kuishia njiani?
Ni baada ya kuja kujifunza kwa kina kuhusu saikolojia ya watu ndiyo nilipata majibu.

Na majibu niliyopata ni haya, hadithi ambayo watu wanajiambia wao wenyewe, kuwahusu wao, ndiyo yenye nguvu kubwa kuliko hadithi za nje.
Yale ambayo mtu anafanya akiwa peke yake, ndiyo yanajenga hadithi yake ambayo ndiyo inakuwa na nguvu kubwa.

Wacha nikupe mfano ili tuelewane vizuri.
Tuseme labda umejiambia utaamka saa kumi alfajiri.
Ukaweka alamu kwenye simu yako.
Muda unapofika na alamu kuita, unaizima na kujiambia unalala kwa dakika nyingine chache.
Unakuja kushtuka kumekucha kabisa, jua tayari linawaka.
Unapoulizwa kwa nini hujaonekana kwenye jambo la asubuhi, husemi ukweli kwamba ulizima alamu na kulala.
Bali unasema mtandao ulikusumbua, au ulipata changamoto.
Watu wanakuamini.

Sasa unajua nini kinakuwa kimetokea hapo?
Hadithi unayokuwa umejipa ni kwamba wewe siyo mtu unayejiheshimu, ukipanga mambo yako huwezi kuyatekeleza.
Na hadithi nyingine unayojipa ni wewe ni mtu mwongo, huwa husemi ukweli.
Hadithi hizo zinakuwa na nguvu kubwa sana kwako, kwa sababu zina ushahidi wa wazi kabisa.

Sasa patamu zaidi ni jinsi hadithi hizo zinavyoendelea kufanya kazi.
Siku nyingine tena alamu inaita, lakini sasa una ushahidi, wewe siyo mtu unayejiheshimu, hivyo unaizima na kulala.
Na unaouliza una hadithi kwamba wewe ni mtu mwongo, hivyo unadanganya.
Utaendelea hivyo, huku sababu na visingizio unavyotumia vikiendelea kuisha.
Baada ya sababu na visingizio kuisha, unabaki na kitu kimoja tu; KUACHA.

Na hapo ndipo wengi huja na hadithi ya mwisho kwangu, wakiwa na maelezo yaliyojipanga vizuri kabisa.
Maelezo yanaweza kuwa mengi, lakini yanakuwa na mtiririko huu; Kocha umekuwa mtu wa msaada mkubwa kwangu, nimejifunza mengi kwako, ila kwa sasa naomba nikae pembeni kidogo, nitarudi baada ya kuweka mambo yangu sawa.
Kunaweza kuwa na maelezo mengine mengi ya kunipamba au kujitetea, lakini kwa msingi hadithi inaenda hivyo.
Na huo ndiyo unakuwa msumari wa mwisho kwenye jeneza la kuyaaga mashindano.

Mwanzoni nilikuwa naumia sana mtu anapokuja kwangu na hizo taarifa.
Nilikuwa najiuliza nawezaje kumsaidia mtu zaidi.
Nikikumbuka ahadi nyingi alizotoa kwangu na kwa wengine.
Lakini pia nilikuwa najipa matumaini kwenye hadithi anayonipa mtu, nikijiambia atarudi kama alivyosema.
Lakini nilijifunza kwa ugumu na maumivu kwamba hadithi hizo huwa hazitimii.
Kwamba mtu wa kuacha ni wa kuacha tu.
Na mtu haachi kwa sababu yangu, bali kwa sababu zake binafsi, kutokana na hadithi anayojipa na ushahidi wake binafsi.
Kitu ambacho sina namna yoyote ya kukiathiri, labda kama ningekuwa naambatana naye masaa yote 24 ya siku na kumwambia mbona hapo unafanya tofauti na unavyoahidi au kuripoti?

Hivyo basi, kwa sasa, mtu anapokuja kwangu na hiyo hadithi nzuri ya yeye kuacha, namjibu kwa furaha kabisa; Sawa, kila la kheri.
Nikiwa na uhakika, bila ya shaka yoyote kwamba hadithi yake ya ndani imeshinda.
Haijalishi alikuwa anatuahidi nini, hadithi ya ndani haikuwa inaendana na ahadi alizokuwa anatupa.
Na kwa sababu hadithi ya ndani ndiyo yenye nguvu, huwa inapata ushindi mara zote.

Lakini pia nimekuwa naenda hatua ya ziada kuwasaidia watu kufanya maamuzi pale ninapoona wazi hadithi ya ndani yake haiendani na kile anachotuahidi.
Pale ninapoona mtu anasua sua kwenye mchakato, namsaidia kwa kumwondoa ili asiendelee na mateso anayokuwa anapitia, ya hadithi ya ndani kuwa tofauti na ahadi zake za nje.

Maelezo ni mengi hapa nikijaribu kukufanya uielewe hii dhana, kwa sababu ningeeleza tu kwa juu, wengi msingeelewa.
Lakini ya msingi kabisa ni haya;
1. Kitakachokufanya uache chochote kile ulichoahidi au kuonekana kufanya kwa nje ni hadithi ya ndani yako mwenyewe unayojiambia mwenyewe.
2. Hadithi hiyo inapewa nguvu na ushahidi wa yale ambayo umekuwa unayafanya ukiwa peke yako.
3. Kama unayofanya hadharani (ukiwa mbele ya wengine) ni tofauti na unayofanya faraghani (ukiwa peke yako) yanatofautiana, yatakayoshinda ni yale ya faraghani.

Tukiwa hapo hapo kwenye hatua za watu kuacha, kuna mwenendo ambao nimekuwa nauona ukijirudia rudia kwa wengi.
1. Mtu anaanza akiwa na shauku na hamasa kubwa, anafanya kila anachoambiwa kufanya.
2. Matokeo anayopata yanakuwa ni madogo au hakuna kabisa ukilinganisha na juhudi anazoripoti kuweka.
3. Hamasa na shauku vinaanza kupungua, anaanza kukosekana, huku sababu na visingizio vikiwa vingi.
4. Matokeo yanazidi kuwa madogo au kutokupatikana kabisa.
5. Mwisho wanapotea kabisa.

Kwa nilivyowaangalia wengi, mahali pekee wanapoweza kusimamisha hiyo safari ya kupotea ni kwenye namba mbili.
Pale matokeo yanapokuwa tofauti na juhudi wanazoweka, wanapaswa kujiuliza wapi wanajidanganya wenyewe.
Safari ikishafika namba tatu, ni sawa na gari iliyokatika breki ikiwa kwenye mteremko mkali, hakuna namna upotevu utaweza kuzuiwa.

Ukiwa mtu wa kujitathmini kila mara na kujiambia ukweli, utagundua haraka sana pale unapojikuta namba mbili na kuweza kuchukua hatua.

Ah, mambo ni mengi na nataka utajue yote kwa sababu huenda yatakusaidia.
Nimalizie na moja la mwisho, lawama ambazo watu wamekuwa wananipa.
Zipo mbili kubwa;
1. Kocha watu wanakudanganya na wewe unakubali. Hii huwa nacheka mwenyewe, kwa sababu ninachojua hakuna mtu anayeweza kumdanganya mtu mwingine, watu huwa wanajidanganya wengine. Na pale ninapogundua mtu ananidanganya huwa nafurahi sana, maana huwa nalichukulia kama jaribio, kuona mtu ataenda na huo uongo wake mpaka wapi. Na majibu ya hayo majaribio ndiyo nimewapa hapa leo, mtu akishaanza tu kudanganya, jua ameuanza mwisho wa safari.
2. Kocha umekuwa unawatoa watu bila hata kuwapa nafasi ya kujirekebisha. Hapo huwa nacheka pia, kwa sababu wengi wanaoeleza hayo kuna taarifa za ndani za mtu wanakuwa hawazijui, ambazo mimi nazijua na kwa huu mtiririko niliowashirikisha hapa, najua amefika mahali pa mateso, anataka kuturidhisha kwa nje, wakati kwa ndani anateseka zaidi. Namsaidia kufanya maamuzi ambayo angalau yatamwacha na amani fulani.

Yote kwa yote, ufanye nini basi ili kuepukana na haya yote?
Kuwa mtu wa aina moja, hadharani na faraghani.
Ukichagua kuwa mtu wa aina mbili tofauti, hadharani na faraghani, jua kwa uhakika kabisa mtu wa faraghani ndiye atakayeshinda.

Hii kurasa ya leo ni kama haitaki kuisha hivi.
Wacha nimalizie kabisa, kabisa, kabisa.
Kuna wengi mtasoma hapa, mtafurahi na kuweka maoni mazuri hapa.
Halafu haitachukua muda mrefu mtayaaga mashindano.
Na hakuna namna tunaweza kuzuia hilo.
Kwa sababu hakuna kinachoweza kuishinda nafsi yako ya faraghani.
Tuishie hapo, lakini tunza huu ukurasa, utakusaidia kwenye maisha yako kuliko kitu kingine chochote.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe