Sina uhakika kama itakufaa lakini kila mtu anapenda kuwa na furaha kwenye maisha yake. Vyote tunavyovifanya na malengo tunayoweka na pale tunapoyatimiza huwa tunajisikia furaha.

Furaha yetu inategemea kitu kimoja na kitu hicho ni ubora wa mawazo yetu. Kama tukiwa na mawazo hasi basi itatupelekea kukosa furaha. Na kama tukiwa na mawazo mazuri basi yatapelekea kuwa na furaha.

Mwanafalsa Marcus Aurelius aliwahi kunukuliwa akisema, furaha ya maisha huwa inategemea ubora wa mawazo .

Kumbe basi, kama mawazo yako ni bora, yatapelekea wewe kuwa na furaha ya maisha.

Naye mwanafalsa Confucius anasema, maisha ni rahisi lakini sisi ndiyo tunayafanya kuwa magumu zaidi.

Na ukiangalia ni kweli. Kwa mfano, mahitaji ya msingi ni machache lakini anasa zetu ndiyo inafanya maisha kuwa magumu zaidi.

Tusifanye maisha kuwa magumu kwa kuwa na mawazo hasi ambayo yanafunga akili yako.

Kuwa makini sana na mawazo yako. Yanaweza kufungua au kufunga milango ya baraka.

Kwa sababu unakuwa kile unachofikiria. Kama unataka kuwa na furaha basi hakikisha akili yako inakuwa na mawazo bora. Mawazo bora ndiyo yanapelekea wewe kuwa na furaha.

Ukiona huna furaha jiulize kwani mawazo yangu yakoje?

Akili yako ni ufanguo, unafungua kila kitu. Kuwa na mawazo ambayo yatapelekea wewe kuwa na furaha kubwa kwenye maisha yako.

Hatua ya kuchukua leo; jua ni mawazo gani ukiwaza yataongeza ubora wa furaha yako.

Maisha ni furaha. Kuwa na mawazo bora yatakayokupelekea wewe kuwa na furaha ya maisha.

Kitu kimoja zaidi , fikiria mawazo bora yatakayokupa furaha ya maisha.

Rafiki na Mwanafalsafa mwenzako,
Mstoa Mwl Deogratius Kessy.