3227; Kupigiwa makofi.

Rafiki yangu mpendwa,
Sisi binadamu kama viumbe wa kijamii huwa tunapenda sana kukubalika na wengine kwenye chochote tunachofanya.

Pale wengine wanapotusifia na kutupigia makofi kwenye kile tunachofanya ndiyo tunaona tunafanya kitu sahihi.

Lakini ukweli ni kwamba hakuna yeyote aliyewahi kufanya makubwa ambaye alikubalika na kusifiwa mwanzoni.
Wote walionekana kama wamechanganyikiwa kwa jinsi walivyoonekana kutaka kupata vitu vikubwa ambavyo havikuwa vimezoeleka.

Kama wangekata tamaa kwa sababu ya kutokukubalika mwanzoni, wasingeweza kufanya makubwa.

Wajibu wako mkubwa kwenye maisha ni kuyaendea maisha unayotaka kuyaishi kwa msukumo mkubwa na bila ya aibu wala kuchoka.
Hupaswi kusubiri kukubalika, kusifiwa au kupigiwa makofi.

Utakubalika sana kama utachagua kufanya mambo ya kawaida na yaliyozoeleka.
Utapigiwa makofi mengi kama utafuata mkumbo wa yale ambayo wengine wanafanya.
Lakini njia hiyo haitakufikisha mbali.
Kwani hata wanaokukubali na kukusifia, watafanya hivyo kwa muda tu.

Ukichagua njia ya kufanya makubwa kwenye maisha yako, mwanzo wengi hawatakuelewa.
Watakucheka, watakudharau, watakupinga na kukukatisha tamaa.
Kama utaweza kuyavuka yote hayo na kuendelea mpaka kupata ushindi, wote waliokuwa wanakukataa watakuwa ndiyo wanaokukubali.

Wajibu wako namba moja kwenye maisha siyo kuwaridhisha wengine kwanza, bali kuishi aina ya maisha unayotaka kuishi.
Hivyo ndivyo unavyoweza kupata ushindi mkubwa na unaopelekea ukubalike zaidi.

Ushindi mkuu na sahihi kwako ni kuyaishi maisha yako kwa ukamilifu wake.
Mengine yote yataweza kukaa sawa baada ya hilo kuwa sawa.
Usiyumbishwe na ugumu na kutokukubalika mwanzoni.
Hivyo ndivyo safari ilivyo kwa watu wote.
Haitakuwa tofauti kwako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe