3252; Kabla ya kujifunza kushinda.

Rafiki yangu mpendwa,
Kila mtu anataka kupata ushindi mkubwa kwenye maisha yake.
Lakini wanaopata ushindi huo mkubwa na unaodumu huwa ni wachache.
Wengi huwa wanapata ushindi ambao huwa unawapoteza kabisa.

Ukweli ni kwamba kabla mtu hajajifunza kushinda, lazima kwanza ashindwe.
Ni kupitia kushindwa ndiyo mtu anajifunza mambo mengi ya kuzingatia ili kupata ushindi mkubwa zaidi na wa kudumu.

Ushindi ambao wengi wanaanza nao kwenye kile wanachofanya huwa siyo ushindi unaodumu.
Hiyo ni kwa sababu huwa hawajifunzi vizuri kwenye ushindi kama wanavyojifunza kwenye kushindwa.

Mtu anayeanza na ushindi anaweza kujisahau na kudhani yeye ana uwezo mkubwa kuliko wengine. Hilo linampa kiburi cha kutaka mambo yaende vile anavyotaka, hata kama sivyo kanuni za asili zilivyo.

Mtu anayekutana na kushindwa huwa anapitia hali ya kujifunza ambayo inamfanya aelewe vizuri kanuni za asili zilivyo.
Ni kupitia kanuni hizo ndiyo anaweza kupata ushindi mkubwa wakati mwingine.

Mtu anayeshindwa kujifunza masomo yaliyo nyuma ya kushindwa kwake ataendelea kushindwa kila mara.
Lakini anayejifunza kupitia kila kushindwa, anaendelea kuwa bora zaidi.

Katika kuitathmini biashara yoyote ile kwa haraka, angalia makosa ambayo biashara hiyo imeshapitia.
Kama kuna makosa yamefanyika lakini biashara inaendelea, maana yake kuna funzo kubwa lilipatikana kwenye makosa hayo na kuchangia kwenye ushindi.

Lakini kama unaitathmini biashara na huoni makosa ambayo biashara imeshapitia, kuwa na wasiwasi. Mafanikio yoyote unayokuwa unayaona kwenye biashara ambayo hayatokani na kushindwa, huwa ni hewa.
Kuna namna watu huwa wanavimba kichwa na kusababisha matatizo pale wanapokuwa wanapata ushindi mfululizo.

Unaposhindwa kwenye jambo lolote lile usichukie wala kukata tamaa.
Bali furahia, kwa sababu unapita kwenye darasa la kukuwezesha kupata ushindi mkubwa zaidi.
Kushindwa ni mwalimu mzuri wa kupata ushindi mkubwa zaidi, mtumie vyema.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe