3320; Maamuzi na lawama.
Kutoka mezani kwa Kocha.
Ufanyaji wa maamuzi kwa watu imekuwa ni kitu kigumu sana.
Siyo kwa sababu watu hawana maamuzi ya kufanya.
Karibu kila mtu huwa ana maamuzi kwenye kila jambo linalomhusu.
Wanapokwama wengi ni kwenye kuyafanya maamuzi hayo.
Wengi wanakwepa kufanya maamuzi kwa sababu wanakwepa lawama zinazotokana na maamuzi hayo.
Kwa sababu matokeo yanayotokana na maamuzi, huwa yanapelekwa kwa aliyefanya maamuzi.
Hivyo kama matokeo hayatakuwa mazuri, aliyefanya maamuzi ndiye atakayelaumiwa.

Sasa kwa sababu watu wengi huwa hawapendi lawama, hukwepa kufanya maamuzi ambayo tayari wanayo kabisa.
Huwa wanaona ni bora waendelee na hali wanazokuwa nazo kuliko kufanya maamuzi ambayo watawajibika nayo.
Na pale wanapokuwa wamechoka ile hali ambayo hawataki kuifanyia maamuzi, huwa wanawalazimisha wengine wawafanyie maamuzi.
Watafanya vituko vya kila aina ili wengine wawafanyie maamuzi ambayo wao tayari wanayo, ila hawayafanyi kwa kukwepa lawama.
Kwa mtu kufanya maamuzi mwenyewe, anajua matokeo yoyote yatakayokuja atalaumiwa yeye kwa maamuzi aliyofanya.
Lakini kwa kuwasukuma wengine wawafanyie maamuzi, wanajua lawama zitaenda kwa hao walioyafanya hayo maamuzi.
Huwa tunaona hii mifano kwa wafanyakazi, ambao wanakuwa wameichoka kazi, lakini hawathubutu kufanya maamuzi ya kuiacha. Wanajua kama wataacha kazi wao wenyewe na mambo yakawawia magumu huko mbele, watabeba lawama zao wenyewe kwamba waliacha kazi.
Hivyo wafanyakazi wa aina hiyo wanachofanya ni vituko mbalimbali ili wafukuzwe kazi.
Wakishafukuzwa kazi, wanajua lolote litakalotokea wao siyo wa kulaumiwa, bali wale waliowafukuza kazi.
Wataonyesha jinsi ambavyo maamuzi ya wao kufukuzwa hayakuwa sahihi.
Watahakikisha wao hawana popote wanapoweza kulaumiwa ili matokeo yoyote yanayotokea yasiwahusishe wao.
Hili pia huwa linatokea kwenye mahusiano, ambapo unakuta upande mmoja umeyachoka mahusiano na haupo tayari kuendelea.
Lakini upande huo unakuwa haupo tayari kufanya maamuzi kwa kuepuka lawama ambazo zitatokana na maamuzi hayo.
Hivyo upande huo huanza vituko mbalimbali ili upande wa pili ufanya maamuzi ya kukatisha mahusiano hayo.
Utajua hilo lilikuwa linaendelea kutokana na mrejesho wa maamuzi yanayokuwa yamefanyika.
Upande ambao ulikuwa unachochea maamuzi yafanyika, huwa unayapokea maamuzi hayo kwa furaha kubwa.
Huwa unatoa hotuba ya kishujaa, ukishukuru na kuonyesha kuthamini upande wa pili uliofanya maamuzi.
Hapo unajua kabisa kwamba hiyo hotuba haikuandaliwa hapo kwa hapo, bali ilikuwa imeshaandaliwa muda mrefu.
Kwenye KISIMA CHA MAARIFA, jamii ya tofauti ambayo tunaijenga, tunawasaidia watu kufanya maamuzi haraka sana.
Kwa kuwa jamii inayo miongozo mbalimbali ya kufuata, pale mtu anapoacha kufuata miongozo hiyo, tunajua hayupo tena tayari kuendelea na jamii hiyo.
Pamoja na kuwa hayupo tayari kuendelea, anakuwa hawezi kufanya maamuzi mwenyewe. Kwa sababu hataki lawama kwamba aliondoka yeye mwenyewe.
Hilo ndiyo linamfanya aache kufuata taratibu zilizopo, ili achukuliwe hatua ya kuondolewa.
Anapochukuliwa hatua, anakuwa na nafasi ya kusema aliondolewa, hivyo lawama hazikuwa kwake.
Atakuja na hotuba za kishujaa na maelezo marefu sana kuhusu hatua zilizochukuliwa.
Lakini ni kitu wanachokuwa wamefurahi kufanyiwa maamuzi.
Na kama wakicheleweshwa kufanyiwa maamuzi, hufanya vituko vya kila aina ili tu hatua zichukuliwe.
KISIMA CHA MAARIFA hakitawachelewesha tena watu ambao hawaamini na kuiishi misingi yake bila ya kusubiri.
Kuwa na sababu na visingizio vya kutokuizingatia misingi na taratibu za jamii hii itachukuliwa mara moja kama kiashiria cha kutokutaka na kuepuka lawama za maamuzi.
KISIMA CHA kitawasaidia watu kufanya maamuzi na kuwa tayari kubeba lawama zote zinazotokana na kila maamuzi yanayofanywa.
Kujenga jamii bora na ya mipekee, inayosimamia misingi imara siyo kitu chepesi.
Bila ya uimara wa pande zote zinazohusika, itakuwa ni sawa na kujenga nyumba ya mchanga ufukweni.
Ni swala la mawimbi tu kupita na chochote kilichojengwa kubomoka kabisa.
Ni bora kupitisha kile unachojenga kwenye mitikisiko ili uweze kuona wapi penye madhaifu yanayoweza kuleta uharibifu au anguko.
Ufanyaji wa maamuzi ya haraka ni moja ya mitikisiko muhimu kufanya ili kupima uimara na hata kuimarisha kile unachojenga.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe