
Zawadi jambo au kitu apewacho mtu kwa hiari bila malipo yoyote. Inaweza kuwa ya kitu kinachoshikika moja kwa moja kama nguo, kalamu au daftali lakini pia, inaweza kuwa kitu kisichoshikwa mfano ofa na vitu vingine.
Kiasili sisi binadamu huwa tunapenda zawadi, huwa haijalishi ni ndogo au kubwa kiasi gani, pale tunapopewa kitu ambacho haikuwa wajibu wetu kupewa, huwa tunakithamini sana.
Ni nguvu hiyo ya zawadi ndiyo tunaweza kuitumia kama sehemu ya masoko kwenye biashara zetu na kuwafanya wengi kuijua na kushawishika kuja kununua. Kampuni kubwa kama benki na mitandao ya simu wanatumia mfumo wa zawadi kuwapata wateja wengi.
Biashara inapotoa zawadi kwa wateja wake, kwanza inawafanya warudi tena kwenye biashara. Lakini pia inawafanya wawe tayari kuwaambia wengine kuhusu zawadi walizopata.
Watu huwa hawawezi kutulia na vitu vizuri, hivyo maneno yatasambaa na wengi zaidi watakuja ili nao waweze kupata zawadi zinazotolewa kwenye biashara.
Kuna zawadi nyingi ambazo kila biashara inaweza kutoa kwa wateja na kuwashawishi kununua zaidi. baadhi ya zawadi hizo ni kama ifuatavyo;
- Vitu vya kushikika mfano tisheti, kalamu na vitu vingine kulingana na biashara yako.
- Punguzo la bei.
Hili lipo kwa manunuzi ambayo mtu anafanya. Anapomaliza kufanya malipo anajikuta ameokoa kiasi fulani cha fedha, hali inayofanya apate furaha kubwa. - Nyongeza ya kitu.
Hii ipo pale mtu anapofanya manunuzi ya kiasi fulani. Mfano, mtu akinunua tatu anapata moja bure, au namba nyingine kulingana na aina ya biashara. - Nafasi ya kipekee kwenye biashara kulingana na manunuzi anayokuwa amefanya au muda ambao amekaa kwenye biashara.
Mambo ya kuzingatia kwenye zawadi.
Ili utoaji zawadi uwe na tija kimasoko kwenye biashara, haipaswi kutolewa tu bila ya mpango wowote. Kuna mambo muhimu ya kuzingatia kwenye utoaji zawadi ili iweze kuwa sehemu ya masoko.
- Weka mpango wako wa utoaji wa zawadi. Jua kabisa ni zawadi gani inatolewa na mtu anapaswa kuwa na sifa gani ili kupata zawadi hiyo.
- Tangaza zawadi hiyo kwa kiwango kikubwa, fanya kila mteja na mteja tarajiwa kujua kuna fursa ya kupata zawadi na ajue anapaswa kufanya nini ili kushinda zawadi hiyo.
- Onyesha thamani kubwa ya zawadi ambayo mteja anapata na msisitizo mkubwa uwe hapo kwenye thamani. Hitaji kubwa kwenye zawadi siyo gharama yake kwako, bali thamani ambayo mteja anaipa zawadi hiyo. Kadiri unavyoonyesha thamani kubwa ya zawadi kwa wateja, ndivyo wanavyopata msukumo wa kuipata.
- Wateja wakumbushwe kuhusu zawadi. Hii ifanyike kwa kila mteja anayefika kwenye biashara kununua na nini anapaswa kufanya ili apate zawadi hiyo. Kama kigezo cha zawadi ni kiasi cha manunuzi, aonyeshwe ni kwa namna gani akiongeza kiwango anapata zawadi.
- Mteja anapofikia kigezo cha zawadi mpatie zawadi yake.
Tumia tukio hilo kuwafanya wengine nao wasukumwe kuchukua hatua ili nao wapate zawadi. Hakuna kitu chenye ushawishi kama pale watu wanapoona mwingine akinufaika.
Kwanini zawadi ni muhimu kwa wateja?
Moja; Kuboresha mahusiano
Mfano mzuri angalia mtoto wa kiume na binti anayempenda. Binti anapopewa zawadi hufurahi na kuona anathaminiwa.
Hali hiyo ipo kwa wateja pia.
Mbili; Kuonyesha upendo
Kwa namna moja au nyingine zawadi huonyesha alama ya upendo baina ya watu.
Mteja huona umemjali zaidi ya wataja wengine.
Tatu; Alama ya mawasiliano
Umewahi kupewa zawadi ukajisikia vizuri? Ndiyo maana mtu anapokea zawadi anakukumbuka haraka. Hali inayoleta ukaribu na kuwa tayari kufanya mawasiliano na wewe.
Nne; Kutengeneza deni
Zawadi hujenga mahusiano mazuri na watu. Mtu anapopewa zawadi huchukuliwa kama sehemu ya deni, hujiona kama kuna kitu inabidi akifanye kwako.
Tano; Thamani.
Kutoa zawadi ni njia nzuri ya kuonyesha wateja unawathamini. Pia, huchukuliwa kama sehemu ya shukurani kwa mteja.
Muhimu; Sio kila mteja anaweza kupokea zawadi. Zingatia vigezo maalumu ambavyo mtu akivifikia apate zawadi husika na hapo mtu ataona hajapoteza pesa yake.
Je, biashara yako inatoa zawadi kwa wateja wako?
Share na sisi hapa hapa maoni na ushauri.
Imeandaliwa na Lackius Robert Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Cha tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz.