Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Tukikuuliza leo kwa nini unafanya kazi au biashara unayofanya, kwa nini unaishi eneo ambalo unaishi na hata sababu za maamuzi mengine unayofanya, unaweza kutoa majibu yaliyonyooka?

Kwa maana nyingine, unajua kwa nini unafanya yote unayofanya sasa au unafanya kwa sababu ndivyo ulivyozoea kufanya, baada ya kujikuta umefanya?

Pamoja na uzembe unaochangia watu kukosa mafanikio, kikwazo kingine ni watu kupambana sana na bado wasifanikiwe, kwa kutokujua kwa nini wanafanya yote wanayofanya.

Hiyo ni changamoto ambayo imewakwamisha wengi, lakini hawajui jinsi ya kuitatua, hivyo wanatafuta usumbufu wa kuwaondoa kwenye changamoto hiyo. Pale ambapo mtu anakosa maana kwenye maisha yake, anaanza kutafuta maana kwenye vitu, kitu ambacho hakimpi utulivu.

Mambo mengi tunayowaona watu wakihangaika kuyafanya, ili tu waonekane na wengine au wapate umaarufu, ni usumbufu wanaojipa ili wasiuone uhalisia kwamba hakuna cha maana wamefanya na maisha yao.

Inaleta uchungu pale mtu anapokuwa amehangaika kwa maisha yake yote, na yote anayokuwa amefanya anakuwa amefuata tu mkumbo au mazoea. Mtu anakuwa hana chochote ambacho amewahi kufanya kwa sababu kina maana kwake.

Wote tunaanza maisha kwa kujaribu kufanya vitu vyenye maana kwetu, ambavyo vinakuwa havieleweki kwa wengine. Lakini tunakutana na upinzani mkali kwa jamii inayotuzunguka, kitu kinachoturudisha kwenye kufanya kile kinachokubalika kwenye jamii.

Pamoja na jamii kutumia nguvu kubwa kutuweka kwenye hilo gereza la kufanya mambo yasiyokuwa na maana kwetu, siyo hukumu ya maisha, labda kama tukiamua sisi. Tupo huru, kwa wakati wowote ule kuondoka kwenye gereza hilo na kuwa huru kwa namna ambayo tunataka sisi wenyewe.

Barua hii ina lengo la kutuweka huru, kutoka kwenye hilo gereza la kijamii linalotuzuia kuyaishi maisha yenye maana kwetu. Tunakwenda kupata ilani ya kutuongoza, ili na sisi tutengeneze ilani zetu za kutuongoza kuishi kwa uhuru.

1. Ilani Ya Maisha Ya Holstee Iliyoandikwa Mwaka 2009

Kundi la Holstee, liliandika ilani fupi ya maisha kama sehemu ya kazi zao za sanaa. Tangu mwaka huo, ilani hiyo imepata umaarufu mkubwa duniani kwa watu wengi kuona inasema nao moja kwa moja. Hapa tunakwenda kuipata ilani hiyo kwa tafsiri ya Kiswahili, kisha tutapata mwongozo wa kuitumia ilani hiyo kutengeneza ilani binafsi kwetu.

Ilani ya Holstee

Haya ni maisha yako. Fanya unachopenda, na kifanye mara kwa mara.

Kama kuna kitu hukipendi, kibadili. Kama hupendi kazi yako, acha kazi hiyo. Kama huna muda wa kutosha, acha kuangalia TV. Kama unatafuta mpenzi wa maisha yako, acha; watakuwa wanakusubiri pale utakapoanza kufanya vitu unavyopenda.

Acha kuchambua sana mambo, maisha ni rahisi. Hisia zote ni nzuri. Unapokula, furahia kila unachotafuna. Fungua akili yako, mikono yako na moyo wako kwa vitu vipya na watu, tumeunganishwa na tofauti zetu. Muulize kila unayekutana naye anapenda nini, na washirikishe ndoto zako zinazohamasisha.

Safiri mara kwa mara; kupotea kutakusaidia kujipata mwenyewe. Kuna baadhi ya fursa zinakuja mara moja, zichangamkie. Maisha ni kuhusu watu unaokutana nao, na vitu unavyotengeneza nao, hivyo toka nje na anza kutengeneza. Maisha ni mafupi. Ishi ndoto yako na shirikisha vile unavyopenda.

Rafiki, hiyo ndiyo ilani kama ilivyoshirikishwa, na naamini umeona jinsi ambavyo imesema vitu vingi mno kwenye maelezo hayo machache. Sasa tuangalie jinsi tunavyoweza kuitumia kuwa na maisha huru kwetu wenyewe.

2. Maisha Ni Yako, Ni Mafupi, Yapende.

Kitu kimoja ambacho hatujawahi kusisitiziwa na umiliki wa maisha yetu. Tulipokuwa watoto, tulifanyiwa maamuzi yote na wazazi, walezi, walimu na watu wengine waliokuwa na umri mkubwa kuliko sisi.

Tunakua watu wazima, lakini bado tunabaki kufanyiwa maamuzi na watu wengine, kuanzia kwa watu wetu wa karibu na jamii kwa ujumla. Tunajikuta tunafanya mambo siyo kwa sababu tumetaka, bali kwa sababu ya kuwaridhisha wengine.

Na hapo ndipo tunapokwama kwa kiasi kikubwa sana kujenga maisha tunayoyataka na yanayotuweka huru.

Sababu namba moja ya kuwa na ilani ya maisha yako ni kurudisha umiliki wa maisha yako kwako. Tambua na kubali kwamba maisha yako ni yako, wewe ndiye unayewajibika kwa kila kitu kwenye maisha yako.

Wajibu huo hauji tu na mamlaka, unaambatana na uwajibikaji, kitu ambacho wengi wanakikwepa na ndiyo maana hawataki kumiliki maisha yao. Ukishasema wewe ndiye unayemiliki maisha yako, huwezi tena kumlaumu mtu mwingine kwa kukukwamisha kuwa na maisha unayoyataka. Ina maana kila kinachoendelea kwenye maisha yako, wewe ndiye uliyekisababisha.

Ni lazima ukubali hilo, na uachane kabisa na lawama ambazo umekuwa unazitoa kama sababu ya kukwama.

Kitu kingine muhimu ni ufupi wa maisha. Ukiangalia muda ambao dunia imekuwepo, na muda wa sisi kuishi hapa duniani, tuna muda mfupi sana. Hata mtu ukiweza kuishi miaka 100, bado ni muda mfupi sana ukilinganisha na muda ambao dunia imekuwepo na ambao wewe hutakuwepo.

Hilo linatukumbusha umuhimu wa kutumia vizuri muda wetu. Tunapopoteza muda tujue kabisa tunapoteza maisha. Sasa kama kitu ni kifupi na unachagua kukipoteza, hutakuwa na sababu ya kulalamika unapokosa kile unachotaka.

Ili uyamiliki maisha yako na uyatumie kufanya makubwa, ni lazima uyapende. Fikiria tu kwa vitu ambavyo unavipenda kwenye maisha yako, huwa unavichukuliaje. Sasa rudi kwenye maisha yako, kitu pekee ulicho nacho na kwa muda mfupi, unayachukuliaje?

Una wajibu wa kuyapenda sana maisha yako, kuyathamini na kuyatumia kuacha alama kubwa hapa duniani. Unapoyapenda maisha yako ndiyo pia unaweza kuwapenda wengine na ukapenda chochote unachofanya. Mnyororo huo wa upendo ndiyo unaokupa uhuru, furaha na mafanikio makubwa.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha ujifunze mambo mengine matatu ya kuzingatia kwenye ilani ya maisha yako ya mafanikio.

Soma hapa; #BZK079; Ilani Ya Maisha Ya Mafanikio