Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Nimekuwa nakusisitiza kuhusu ujenzi, kitu ambacho ni muhimu sana kwako kupata mafanikio makubwa unayoyataka.

Lakini kujenga pekee haitoshi, matunzo endelevu yanahitajika ili mafanikio yapatikane na kuweza kudumu kwa muda mrefu.

Kuna watu wamekuwa wanajenga vitu ambavyo vinawapa mafanikio makubwa. Lakini mafanikio hayo yamekuwa hayadumu kwa sababu matunzo yanakosekana. Baada ya vitu kujengwa, havipati matunzo yanayohitajika na hilo linapelekea vitu hivyo kuharibika na kupotea.

Sisi hatukubali kuteseka kwa ajili ya kujenga vitu ambavyo vitadumu kwa muda mfupi na kisha kupotea. Tumechagua kujenga vitu ambavyo vitadumu kwa muda mrefu, kwa kipindi chote ambacho tupo na kuendelea kuwepo hata baada ya sisi kuondoka.

Ili mafanikio yoyote tunayoyajenga yadumu, kujenga kunahitajika, na kutunza kunahitajika kwa kiwango kikubwa pia.

Changamoto kubwa ambazo tumekuwa nazo kwenye maisha, kuanzia kwa mtu binafsi, familia, jamii, taifa na hata dunia, ni kutunza vizuri vitu vilivyotengenezwa. Chochote tunachoona kimedumu, ni kwa sababu ya matunzo. Na kwa vingi vinavyoshindwa, matatizo yanaanzia kwenye matunzo.

Kwa umuhimu huu wa matunzo kwenye kudumisha mafanikio, ni muhimu kila mmoja wetu kuweka matunzo kwenye kila anachojenga ili kiwe na tija. Hatupaswi tu kuishia kuhamasika na kujenga, tunapaswa pia kuhakikisha tunatunza kwa muda mrefu kile tunachojenga.

Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kujifunza umuhimu wa matunzo kwenye vitu unavyojenga ili upate mafanikio yanayodumu kwa muda mrefu.

1. Kujenga Ni Kuleta Kitu Kipya

Mafunzo na hamasa nyingi ambazo zimekuwa zinatolewa kuhusu mafanikio, zimejikita kwenye kujenga. Kujenga kunahusisha kuleta vitu vipya, ambavyo havijawahi kuwepo kabisa. Kujenga kunabadili vitu, kutoka kwenye hali moja kwenda kwenye hali nyingine.

Kujenga ni hatua muhimu sana ya mafanikio, kwa sababu ndiyo kunahakikisha kile kinachohitajika ili matokeo yapatikane kinakuwepo. Kujenga kunafungua milango na kuondoa ugumu ambao umekuwa unakwamisha matokeo kupatikana.

Kujenga ndiyo kumeleta mabadiliko yote tunayoyaona, kwa sababu vitu vingi vilivyopo sasa huko nyuma havikuwepo. Kujenga kumeongeza thamani kwenye vitu vingi ambavyo havikuwa na thamani hapo kabla.

Dunia inahitaji wajenzi, ambao wanapata maono ya vitu kuwa bora zaidi ya vilivyo na kupambana kuvileta kwenye uhalisia. Maisha yako yanataka wewe uwe mjenzi, ili uweze kubadili yale uliyonayo sasa yakuletee matokeo bora zaidi.

Ujenzi ni hatua muhimu ambayo inapaswa kuwa endelevu kwenye maisha ili mafanikio makubwa yaweze kupatikana. Bila ujenzi maendeleo yanasimama na mazoea kutawala, kitu kinachokwamisha mafanikio makubwa.

2. Kutunza Ni Kufanya Kitu Kiendelee Kuwepo

Kujenga kunapewa kelele nyingi kwa sababu ya kuleta kitu ambacho hakijawahi kuwepo. Japokuwa kujenga kunaleta mafanikio, siyo kila kinachojengwa kinadumu kwa muda mrefu na kuleta matokeo kama inavyotegemewa.

Ili kinachojengwa kiweze kudumu na kuendelea kuleta matokeo, matunzo yanahitajika. Matunzo ndiyo yanafanya kitu kiendelee kuwepo na kuleta matokeo yanayohitajika. Kutunza ndiyo kunadumisha mafanikio yaliyopatikana, kwa kufanya yaendelee kuwepo.

Wakati kujenga kunaweza kuwa kitu cha mara moja, kutunza ni kitu kinachopaswa kufanyika kwa uendelevu. Matunzo hayana mwisho, huwezi kusema umemaliza kutunza kitu. Matunzo ni endelevu, kwa kipindi chote ambacho kitu kipo, kinapaswa kupewa matunzo.

Kujenga kunaweza kuonekana ndiyo hatua muhimu zaidi, lakini matunzo ni hatua muhimu kama ilivyo kujenga. Kujenga bila matunzo ni kupoteza rasilimali nyingi zinazokuwa zimeingia kwenye ujenzi.

Ni muhimu sana kwa kila kinachojengwa, mpango wa matunzo endelevu uwepo na ufanyiwe kazi. Huwa ni rahisi kupuuza matunzo, hasa wakati wa mwanzo baada ya ujenzi, lakini hilo linajenga deni kubwa na linalokuja kugharimu.

Asili huwa ina tabia ya kuharibu kila kitu. Ndiyo maana hata ukiwa na chumba kwenye nyumba yako, ukakisafisha na kukifunga, kwa kuzuia chochote kisiingie, baada ya muda utakuta chumba hicho kina uchafu na hata kuharibika. Huo ni mfano rahisi wa umuhimu wa matunzo kwenye kila kitu.

Kuna miradi mikubwa ya taasisi kubwa na hata serikali ambayo imekuwa inajengwa kwa gharama kubwa na kufurahiwa na kila mtu inapokamilika. Lakini miradi hiyo imekuwa haidumu, kwa sababu ya kukosa matunzo mazuri.

Matunzo ni eneo ambalo linahitaji umakini na kipaumbele cha kutosha ili kuhakikisha mafanikio yanayopatikana yanatunzwa kwa muda mrefu.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK127; Kujenga Pekee Haitoshi, Matunzo Endelevu Yanahitajika Kwenye Mafanikio