Katika ufunguzi wa mkutano wa ‘smart dialogue partnership’ uliofanyika mwishoni mwa mwezi juni mwaka huu(2013) dar es salaam, akihutubia Rais Kikwete alisema kwamba yeye anayo simu aina ya iphone 5, na japokuwa ina vitu vingi vya kutumia ila yeye anatumia kupiga na kupokea simu na ujumbe mfupi wa maneno. Niliposikia kauli yake nilijiuliza mara mbili kwa nini watanzania wengi wanapenda kutumia simu za aina hii?

iphone 5

  Simu kama iphone ina vitu vingi sana ambavyo haviwezi kutumika tanzania, kwa mfano kuangalia hali ya hewa, taarifa za soko la hisa, manunuzi kwenye mitandao ya ebay na amazon na kuongoza mitaa kwa kutumia GPS. Hizo ni baadhi ya vitu vinavyoweza kufanyika kwenye simu za aina hiyo ila haviwezi kutumika kwa nchi kama Tanzania. Pamoja na vitu hivyo kutoweza kutumika kwenye nchi zetu hizo bado pia simu za aina hiyo zinauzwa kwa bei kubwa sana. Kuna zenye bei mpaka zaidi ya shilingi milioni moja za kitanzania.

  Sasa kwa nini basi watu wapende kutumia hizi simu za bei ghali na ambazo kazi zake nyingi hazifanyiki kwenye mazingira yetu? Jibu ni moja ufahari na kuonekana. Unaweza kukataa na kusema ni mapenzi tu labda na aina hizo za simu ila kinachosukuma wengi kutumia simu za aina hizo ni kunekana wa hali ya juu, wa kisasa na wenye uelewa mkubwa. Kwa kifupi ni ili kunekana kwa hali hizo.

  Kutaka kuonekana wa daraja fulani kwenye jamii ndio kinakufanya uishi maisha magumu sana. Unaumia sana ili kufikia gharama ambazo ziko nje ya uwezo wako ili tu na wewe uonekane una kitu fulani ambacho jamii inakithamini sana. Usitake kuishi maisha ya kutaka kukubalika na wengine ama ya kutaka kufata wengine wanafanya nini. Ishi maisha yako kutokana na mahitaji yako, nunua vitu vya kiwango na mahitaji unayotaka na sio kwa ajili ya ufahari.

smart phones

  Kwa mfano kwenye iphone 5(na nyingine za aina hiyo), ambayo bei yake ni karibu shilingi milioni moja au zaidi, mtanzania unaitumia kwa kuwasiliana kwa simu na ujumbe, kutumia mtandao na na baadhi ya ‘applications’, vitu hivyo unaweza kuvifanya kwenye simu ya aina nyingine ambayo ni ‘orijino’ na bei yake ni karibu shilingi laki mbili(au chini ya hapo).

  Kama unaweza kununua simu ya shilingi milioni moja na maisha yako yasiathirike kwa chochote basi hakuna tatizo. Ila kama utajikamua ununue simu ya bei hiyo na bado maisha yako ni ya kuungaunga yaani huna uhakika wa kipato kwa miezi kumi na mbili inayokuja basi fikiri mara mbili kabla ya kufanya hayo maamuzi.

  Usinunue kitu chochote kwa sababu watu wengi wanacho ama kila anaenekana wa daraja fulani unalotaka kuwepo anacho. Chochote unachotaka kununua hakikisha kina uhitaji mkubwa kwenye maisha yako kwa sasa, kwamba ukikikosa maisha yatakuwa magumu mno.