Kuna watu wanaishi kwa taabu sana hapa duniani kwa kutojua kitu kimoja kuhusu maisha yao. Maisha ni kufurahia kuishi na sio kusubiri kufurahishwa na wengine. Furaha ni haki yako ya msingi umezaliwa nayo. Hakuna yeyote mwenye haki ya kukupa wala kukunyima furaha, na kamwe usimpatie mtu yeyote ruhusa hiyo.

  Kwa kutegemea kupewa furaha na wengine baadhi ya watu wameishi maisha magumu na yasiyo na maana. Usitegemee kupata furaha kutoka kwa ndugu, jamaa ama marafiki, wala usitegemee kupewa furaha kutoka kwa mwenza ama mpenzi wako. Hawa watu wapo kwenye maisha yako na ni muhimu kwako katika kushirikiana nao na kufurahia nao maisha ila usiwafanye wao ndio kwamba wanaweza kukupa wewe furaha. Furaha ya kweli inatoka ndani ya nafsi yako.

furaha2

  Utapata furaha ya kweli pale utakapokuwa unafanya unachopenda kufanya na sio kufanya ili watu wakupende kwa unachofanya. Fuata nasfi yako, tumia kipaji chako kufanya kile unachoweza kukifanya kwa utofauti mkubwa na unachofurahia. Moja kwa moja wanaokuzunguka watakupenda wewe kama wewe na kufurahia unachofanya kama unavyofurahia wewe.

  Kama utajaribu kufanya jambo usilopenda kulifanya ili tu kumridhisha mtu ndipo ufurahi basi jua hutoweza kuwa na furaha ya kweli kwenye maisha yako. Wafanye wanakuzunguka wakukubali wewe ulivyo na kwa unayoyafanya.

furaha

  Njia pekee ya watu kukukubali wewe ulivyo ni kwa kufanya kile unachokipenda na kukifurahia.

  Hakuna mwenye mamlaka ya kukupa ama kuchukua furaha yako. Una maamuzi juu ya furaha yako na ni haki yako ya msingi uliyozaliwa nayo.