Kwanza nitoe pole sana kwa ndugu zetu na jirani zetu Kenya kwa magumu wanayopitia. Ni jambo la kusikitisha sana kuona binadamu anamuua binadamu mwenzake tena kinyama, inaumiza sana.
Katika viumbe vyote viishivo duniani kuna kiumbe mmoja ni hatari sana na anaweza kuiangamiza dunia nzima.
Kiumbe huyu amepewa uwezo mkubwa sana kuliko viumbe wengine na kupitia uwezo huo mkubwa anaweza kuifanya dunia kuwa sehemu bora sana kwa maisha ama kuwa sehemu mbovu sana kwa maisha.
Kiumbe huyu anaeweza kuijenga ama kuibomoa dunia ni Binadamu. Sisi binadamu ni viumbe hatari sana kwenye hii dunia.Silaha kubwa na za kisasa kabisa zinazotengenezwa kila siku na binadamu ni kwa ajili ya kumuua binadamu mwenzake! Tamaa za baadhi ya binadamu zimesababisha matatizo makubwa sana hapa duniani.
Chanzo kikuu cha matatizo haya yote ni ukosefu wa upendo. Katika makala ya dunia haihitaji vita wala silaha(kama hujaisoma bonyeza hapo kuisoma) tuliona jinsi ambavyo ukosefu wa upendo umesababisha matatizo makubwa duniani.
Hakuna mtu mwenye mamlaka ya kukatisha maisha ya mwenzake kwa sababu yoyote ile. Na hakuna dini yoyote inayotoa mafundisho ya aina hiyo. Tamaa zetu sisi binadamu zimetufanya tutafute njia ya kuhalalisha mambo mabaya kama haya.
Hatusemi tu haya kutokana na mauaji makubwa yanayotokea sehemu mbalimbali duniani. Hata hapa nchini kwetu kuna mambo mengi sana ya kinyama yanaendelea. Wizi, ufisadi, ubakaji, uuaji na mengine mengi ni matendo ambayo binadamu anayafanya kumdhuru binadamu mwenzake.
Dawa ya haya yote ni UPENDO, tupendane kama binadamu. Tofauti ya rangi, kabila, dini na mitazamo mingine haituweki kwenye makundi tofauti ya ubinadamu. Tunaendelea kubaki binadamu licha ya tofauti hizo za kimtizamo.
Tusambaze upendo kwa kuanzia kwenye ngazi ya mtu mmoja mmoja kisha taifa na dunia kiujumla. Tupendane na tuishi pamoja kama ndugu moja ili tuweze kufikia malengo yetu na kufanikiwa.
Yanayotokea kwa wenzetu Kenya na kwingine duniani hata hapa kwetu yanaweza kutokea. Tujihadhari sana na tuzuie mambo haya kutokea. Tunao ushawishi mkubwa kwa binadamu wenzetu hivyo tutumie ushawishi huo kuifanya dunia kuwa sehemu salama kwa maisha.