Kila mtu anatamani kuleta mabadiliko fulani kwenye maisha yake na kwa maisha ya wanaomzunguka. Unaweza kuwa unataka kubadili hali ya maisha, kubadili mazingira ama kuwabadili wale wanaokuzunguka. Ni wachache sana wanaofanikiwa kuleta mabadiliko ya kweli, wengi wanaishia kujaribu kuleta mabadiliko mpaka wanachoka na kuamua kuacha.

mabadiliko4

  Kama wewe ni mmoja wa watu wanaotaka kuleta mabadiliko kwako na kwa dunia kiujumla kuna kitu cha muhimu unachotakiwa kujua kabla hujaanza harakati za kuleta mabadiliko. Kwa kutojua kitu hicho itakuwia vigumu sana kuleta mabadiliko ya kweli.

  Hakuna mabadiliko yoyote yanayoweza kutokea kama wewe hutobadilika. Yaani hakuna kitakacho badilika kabla wewe hujabadilika. Hii ndio sheria kuu ya mabadiliko. mabadiliko3

  Ukijaribu kuleta mabadiliko kabla ya wewe kubadilika itakuwa kazi ngumu sana kwako. Mabadiliko yanaanza na wewe, kuwa mabadiliko unayotaka kuleta.

  Kama unataka kubadili mazingira yanayokuzunguka anza kwanza kubadilika wewe. Anza kubadili mtizamo wako juu ya mazingira unayotaka kubadili ndipo utapoanza kuona mabadiliko yenyewe. Unapobadilika mazingira nayo yanabadilika.

  Kama unataka kuwabadili wanaokuzunguka hasa watu wako wa karibu anza kubadilika wewe. Hakuna kazi ngumu kama kumbadili binadamu, ila wewe unapobadilika unaleta uchocheo wa unayetaka abadilike kuanza kubadilika.

  Mabadiliko yanaambukizwa hivyo kubadilika kwako wewe kutawafanya wanaokuzunguka nao wabadilike. Badilika wewe kabla hujanza kuwabadili wengine.

  Mabadiliko ni kitu kigeni sana kwa binadamu hivyo binadamu yeyote huwa ana asili ya kupinga mabadiliko. Ni rahisi kuondoa kipingamizi hiki cha mabadiliko kama na wewe unayetaka kuleta mabadiliko utakuwa umebadilika.

  Wa kuyabadili maisha yako ni wewe mwenyewe, na utaweza kuyabadili maisha yako kwa wewe mwenyewe utabadilika na kubadili mtizamo wako. Usitegemee mtu yeyote anaweza kuja kuyabadili maisha yako. Hata mtu akikupa chakula, fedha, malazi na kila kitu unachohitaji bado atakuwa hajayabadili maisha yako. Sana sana atakuwa amezidi kuyaharibu.

   Sisi ndio waendeshaji wa maisha yetu na tunalojukumu la kusimamia maisha yetu. Tuwe mabadiliko tunayotaka kuleta kwenye maisha yetu na kwa wanaotuzunguka. Mabadiliko ya kweli yanaanza na sisi wenyewe.

  Tushirikiane kwa pamoja kuleta mabadiliko kwenye jamii yetu na taifa letu kwa kuanza kubadilika sisi wenyewe. Washirikishe marafiki zako ujumbe huu na uwe sehemu ya waleta mabadiliko kwenye jamii yetu.