Mkulima mmoja wa Afrika alikuwa akiishi maisha yake ya furaha kwa kuwa alikuwa na kila alichokitaka. Maisha yake alikuwa ya furaha sana kwa kuwa hakuna alichokikosa, kilimo ndio ilikuwa shughuli yake kuu.
Siku moja mtu mmoja mwerevu alikuja na kumpa habari njema za uvumbuzi wa almasi. Alimwambia kama angeweza kupata almasi ya ukubwa wa kidole angeweza kununua mji, kama angepata ya ukubwa wa mkono angeweza kununua nchi.
Baada ya mtu yule kuondoka mkulima aliingiwa na mawazo mengi sana na ghafla akajikuta hana furaha. Aligundua ni jinsi gani angeweza kuyabadili maisha yake zaidi kama angepata almasi. Siku iliyofuata mkulima alifanya maamuzi ya kuuza mashamba yake yote kuiweka famili yake chini ya usimamizi mzuri na kuanza kuzunguka kutafuta almasi. Alizunguka afrika nzima ila hakupata almasi, alikwenda mpaka ulaya bila kuambulia chochote. Alipofika Uhispania alikuwa ameishiwa na amechoka sana hivyo kujiua kwa kujitupa kwenye mto Barcelona.
Kule nyumbani alikouza shamba, aliyelinunua alikuwa akinywesha mifugo kwenye mfereji unaopita karibu na shamba, aliona jiwe linalong’aa sana, likampendeza na kuamua kulichukua na kuliweka ndani. Yule mtu mwerevu alikuja tena kwenye ile nyumba na kukuta jiwe lile linalongaa, akamuuliza aliyenunua lile shamba kama mmiliki wa mwanzo amerudi. Alimjibu hajarudi na alipotaka kujua kwa nini alimuulizia akamjibu lile jiwe ni almasi na alipoliona alijua ameshapata almasi aliyokwenda kutafuta. Baadae ilikuja kugundulika lile shamba lilikuwa na almasi nyingi mno.
Tunajifunza nini kwenye habari hii?
Kama yule mkulima angelijua almasi inafanana vipi angeipata kwenye shamba lake na maisha yake yangekuwa ya furaha sana.
Maisha yetu ya kila siku yanafanana sana na mfano huo wa almasi. Tunatumia muda mwingi kutafuta fursa sehemu za mbali kabla ya kuchunguza mazingira yetu ya karibu. Tunafikiria kufanya makubwa sana kwa kutumia vitu vingine kabla ya kuujua uwezo mkubwa ulio ndani yetu.
Tunatamani sana kazi za wenzetu ama biashara wanazofanya wenzetu kwa kuona ndizo zenye faida na kushindwa kujua fursa kubwa inayopatikana kwenye kazi zetu na biashara zetu wenyewe.
Wakati unaitamani biashara ama kazi ya wengine kuna mtu anaitamani sana biashara ama kazi unayofanya wewe. Kuna fursa kubwa kwenye kazi ama biashara unayofanya ambayo bado hujaigundua. Kwa kuigundua fursa hiyo unaweza kufanikiwa kwa kiwango kikubwa sana.
Kila biashara na kila kazi inayofanywa na watu ni nzuri na inalipa(soma; hii hapa ndio biashara inayolipa). Kinachotakiwa ni wewe kuzijua fursa zinazopatikana kwenye kazi ama biashara hiyo na jinsi unavyoweza kuzitumia kufikia malengo yako na mafanikio yako.
Usipoteze muda mwingi kuzunguka na kutafuta fursa sehemu za mbali, anza kuutumia uwezo wako binafsi, vipaji, kazi ama biashara unayofanya na mazingira yanayokuzunguka.(soma;wewe ni wa pekee) Kwa kuviangalia vitu hivi kiundani utaona fursa kubwa ambayo kila siku unaipita ama kutoipa thamani kubwa.
HABARI YA ALMASI IMETOLEWA KWENYE KITABU CHA ACRES OF DIAMOND AMBACHO KITATUMWA KWA WANACHAMA WA MTANDAO WA AMKA MTANZANIA BLOG KAMA UTATAKA KUKIPATA NA HUJAJIUNGA JIUNGE HAPA KWA KUANDIKA EMAIL YAKO, BONYEZA HAPA KUJIUNGA