Katika dunia ya sasa kujua tu vitu haitoshi kukutoa kimaisha. Zamani ilionekana mtu akijua kitu ama akiwa mtaalamu kwenye kitu fulani basi kila mtu atamfata kupata huduma ambayo inaweza kutolewa na yeye tu.

  Kwa ulimwengu wa sasa karibu kila mtu anajua hicho unachofanya, kila mtu anaweza kufanya kazi unayofanya na kila mtu anaweza kufanya biashara unayofanya. Hata kwenye ajira nyingi wanaweza kumuajiri mtu kwa sababu tu ana shahada ila kazi atakayoifanya haihusiani na alichosoma. Kwa maelekezo ya muda anakuwa ameshaelewa kazi inafanyikaje.

  Kama kila mtu anaweza kufanya je ni nini kinawatenganisha wanaofanikiwa sana na wanaishia kuwa kawaida? Kama kila mtu anaweza kufanya biashara fulani, kwa nini bado kuna wanaofanikiwa sana na wengine kuishiwa kushindwa?

  Pamoja na sababu zingine zinazotofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa kwenye kazi ama biashara zao, MTANDAO ni kichocheo kikubwa. Mtandao wako ni muhimu sana kwa chochote unachofanya. Unaowajua ni muhimu sana kuliko unachokijua.

mtandao2

  Ninaposema wanaokujua ni muhimu kuliko unachokijua simaanishi utumie ndugu ama rushwa kupata kazi ama biashara, bali namaanisha kuwa na mtandao wa watu wanaokujua na wanaojua unachofanya. Watu hao wawe wanajua uwezo wako na vipaji vyako.

  Ukubwa wa mtandao wako ndio ukubwa wa utajiri wako. Kwa maana jinsi ambavyo watu wengi wanakujua na wanajua kazi nzuri unayofanya ndivyo ambavyo watafikisha maneno kwa watu wengine ambao wanaweza kuwa wanahitaji huduma ama bidhaa unazotoa.

mtandao3

  Jitahidi kwa lolote unalofanya kukuza mtandao wako, ongea na watu wengi wanaofanya unachofanya, ongea na wahudumie wateja wako vizuri na onesha uwezo wako na vipaji vyako kila inapotokea nafasi ya kufanya hivyo. Kwa jitihada hizo unajikuta watu wengi wanakufahamu na wanafurahia kazi yako na inakuwa rahisi kwao kukutambulisha kwa watu wengine wanaowajua wao.

  Nguvu ya mtandao ni kubwa sana, kwani kwa kuanza tu jitihana za kuutengeneza mtandao baadae unakua wenyewe.

  Katika dunia ya sasa kila kitu ni watu. Hauwezi kufanikiwa jambo lolote bila ya watu. Binadamu tunategemeana kwa kiasi kikubwa mno kuliko wakati mwingine wewote. Ili upate fedha lazima zitoke kwa watu, ili upate upendo lazima kuwe na watu, ili ufanye kazi lazima kuwe na watu na ili ufanye biashara lazima kuwe na watu. Hivyo watu ndio jiwe kuu la kujenga msingi wako wa mafanikio.

mtandao4

  Jitahidi sana kukuza mtandao wako kwa chochote unachofanya, kama ni kazi basi fanya juhudi za kujuana na waajiri wengi na waoneshe uwezo na vipaji vyako. Pia hakikisha mwajiri wako anaujua uwezo wako na vipaji vyako na jinsi vinavyoweza kusaidia kazi yako. Kama ikitokea kazi yoyote ambayo inahitaji uwezo ama vipaji ulivyo navyo ni rahisi kwa wewe kupata nafasi hiyo.

  Kama unafanya biashara ongeza mtandao wako kwa kujuana na wafanyabiashara wengine wanaofanya biashara unayofanya ama biashara nyingine. Pia weka jitihada kujuana na wateja wengi zaidi kwa kujenga urafiki mzuri ili wateja hao walete wateja wengine zaidi(soma; lengo la biashara sio faida)

  UKUBWA WA MTANDAO WAKO NDIO UKUBWA WA UTAJIRI WAKO. WEKA JUHUDI ZAKO KWENYE KUKUZA MTANDAO WAKO.