Kama tulivyowahi kuona kwenye makala za nyuma mafanikio yanatokana na vitu vidogo vidogo vilivyofanywa kwa kurudiwa rudiwa. Kwa kukusanya mafanikio haya kidogo kidogo mwisho wa siku unajikuta umepiga hatua kubwa sana kimafanikio na umefikia ama kupita malengo uliyojiwekea.

  Kujua kwamba mafanikio yanatokana na hatua ndogo ndogo kwa unachofanya kila siku inakuwa rahisi sana kwako kuweza kufikia malengo yako. Kwa sababu kwa kujua hivyo unakuwa unathamini kila jitihada ndogo unayoifanya kila siku kwenye kazi zako iwe umeajiriwa, umejiajiri ama unafanya biashara.

kuamka

  Katika harakati zako unazofanya kila siku za kufikia malengo yako kuna tendo moja ambalo karibu kila siku unafanikiwa kulifanya na tendo hilo ni muhimu sana kwa mafanikio yako.

  Kwa kufanikiwa kufanya tendo hilo na ukafurahia kulifanya ni mwanzo mzuri sana wa wewe kufikia malengo yako na kuweza kufanikiwa.

  Tendo ninalozungumzia hapa ni kutoka kitandani. Namaanisha kuweza kuamka na kuondoka kitandani kwa furaha huku ukielekea kwenye shughuli zako. Unaweza kufikiri ni kitu rahisi sana kuamka na kuenda kwenye shughuli zako, ila sio rahisi hata kidogo.

  Hebu fikiri ni mara ngapi inafika asubuhi muda wa kuamka lakini hujisikii kabisa kuamka? Mwili hautaki kabisa kutoka kitandani na unatamani kama ingekuwa ni uwezo wako ungeendelea kulala. Na mara nyingi kuna sauti fulani hutuambia tulale japo nusu saa ya ziada ili kupunguza usingizi. Nini kinachotokea unaporudi kulala tena? Mara nyingi siku yako huharibika kabisa, maana unapopanga kulala nusu saa unakuja kushtuka saa nzima imepita.

  Kwa ugumu huu wa kuamka na ushawishi mkubwa wa usingizi ni dhahiri kwamba kuweza kutoka kitandani kwa furaha ni TENDO LA KISHUJAA. Unastahili kujipongeza na kupongezwa kwa kuweza kufanikisha hilo.

kuamka2kuamka3

  KWA NINI TENDO HILI NI MUHIMU SANA KWAKO NA INABIDI KULIENDELEZA?

  Kama tunavyofahamu moja ya gharama tunayotakiwa kulipa ili kupata mafanikio ni KUHUDHURIA. Lazima kila siku ufanye kitu fulani kinachokupeleka kwenye mafanikio. Kuweza kuamka asubuhi na kwenda kwenye shughuli zako ni dalili njema za mafanikio.(soma; hii ndio gharama ya mafanikio unayotakiwa kulipa)

   Kuweza kuamka asubuhi huku ukiwa na mtazamo chanya juu ya maisha yako na kazi zako ni dalili nzuri kwamba mafanikio yako karibu kukufikia, ama wewe kuyafikia. Wanasema nyota njema huonekana asubuhi, vivyo hivyo hata siku yenye mafanikio unaianza asubuhi kwa kuamka ukiwa na furaha. (soma; leo ni siku muhimu sana kwako)

  Ni muhimu sana kwako kuianza siku yako ukiwa na furaha na ari ya juu ya kwenda kufanya shughuli zako. Kama kila siku asubuhi unasumbuka kuamka na kuna ushawishi mwingi unaupata wa kutaka kusogeza majukumu mbele ama kutaka kulala japo dakika tano za ziada basi soma makala hii uweze kubadili hali hiyo.(soma; hili ndilo kosa unalofanya kila siku asubuhi). Pia weka utaratibu wa kupanga siku yako kabla ya kulala hivyo unapoamka unajua ni kitu gani umepanga kufanya.

  Mafanikio yanaanza na wewe kuweza kutoka kitandani kila asubuhi ukiwa na furaha na ari kubwa.

  Kuna usemi maarufu wanasema USINGIZI WAKO NDIO UMASIKINI WAKO. Haimaanishi usilale bali ukiendekeza usingizi mafanikio utayasikia kwa wenzako tu.