Ulimwengu wa sasa kila kitu kinawekwa kwenye rekodi. Kuna rekodi nyingi sana zimewekwa na watu kwa mchango wao mkubwa waliofanya duniani. Kuna rekodi zilizowekwa kwa uvumbuzi na ugunduzi wa kisayansi, rekodi za michezo mbalimbali, rekodi za uongozi uliotukuka na rekodi za kupigania amani na kuelimisha watu kaika kuzidai haki zao.

  Popote utapoona jina kama Martin Luther King, Malcom X, Mandela, Mahtma Gandhi, Nyerere, Newton, Albert Einstain, Mohamed Alli, Usain Bolt na mengine mengi kuna kitu fulani kitakujia kwenye akili yako. Kwenye kila jambo lolote lililofanyika duniani kuboresha maisha ya binadamu ama kuwaburudisha basi kuna majina fulani yanahusiana na jambo hilo. Hizi ni rekodi nzuri zilizowekwa na watu wema waliopata kuishi(wengine bado wanaishi) katika dunia hii.

  Kwa upande mwingine kuna rekodi zilizowekwa ambazo sio mifano mizuri kwa dunia na hivyo hutumika kuonya binadamu wasifanye yale yaliyofanywa na watu hao. Unaposikia majina kama Adolf Hitler, Idd Amin na mengine mengi kuna picha fulani ya kutisha itakujia kwenye mawazo yako.

  Pamoja na kuwepo kwa rekodi hizo nyingi, kuna mambo mengi sana yanayofanywa na watu ila hakuna rekodi zilizowahi kuwekwa. Kilichonisukuma kuandika makala hii ni baada ya kuona kuna vitu vingi tunapenda kuvifanya ila havina faida kwetu na pia havijawahi kuwa na faida kwa binadamu kwa kipindi chote ulimwengu umekuwepo.

anza

  Yajue mambo hayo na uache kuyafanya mara moja maana hakuna anaenufaika nayo na hakuna atakaekukumbuka kwa kufanya hivyo. Yako mambo mengi sana ila hapa nitaeleza kwa kifupi sana mambo matano ambayo watu wengi tunapenda kufanya.

1. Kukata tamaa. Hakuna rekodi yoyote umewahi kuwekwa ya wakata tamaa maarufu duniani, ama chochote kimewahi kuboreshwa duniani kutokana na kukata tamaa. Kama una tabia hii ni vyema ukaicha mara moja kwa sababu hakuna itakakokufikisha.

2. Kukosoa na kuwa na mtizamo hasi juu ya wengine. Kuna watu wanapenda kukosoa kila kitu. Watu wanaweza kupinga hata kitu ambacho ni cha manufaa kwao. Kumekuwa na wakosoaji wengi sana kwenye jamii na duniani kwa ujumla ila cha kushangaza haijawahi kujengwa sanamu hata moja ya mkosoaji mkuu.

3. Uvivu. Hii ndio mbaya kabisa, tumekuwa na watu wengi ambao ni wavivu wa kutenda na hata kufikiri. Hakuna kitabu chochote mpaka sasa kilichoandikwa kuwaelezea wavivu wakubwa duniani na mchango wao mkubwa kwenye kuibadili dunia.

4. Kukopi na Kupesti, ama kwa lugha rahisi KUIGA. Kwa wakati wa sasa kumekuwa na utegemezi mkubwa sana wa kuiga kila kitu mtu anachofanya. Wachache wamekuwa wanafikiri ila wengi wanaishia kuiga walichofikiri wengine. Hakuna mtu aliewahi kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kuiga vitu vinavyofanywa na wengine. Ubunifu ni muhimu sana.

5.Kutegemea wengine kwa kila kitu. Kumekuwa na utegemezi mkubwa sana siku hizi, watu wanategemea sana msaada ili waweze kufanikiwa. Hii imefikia mpaka hatua taifa linategemea sana misaada na kuona hio ndio njia ya kujikwamua kutoka hali ngumu. Hakuna maendeleo ya kweli yaliyowahi kupatikana duniani kwa kutegemea misaada ya fedha ama mali zozote. Msaada pekee unaoweza kukusaidia ni msaada wa kukujengea uwezo wa kufikiri na kutumia uwezo na vipaji vyako kuweza kuzikabili changamoto unazokutana nazo kwenye maisha.

  Katika safari ya mafanikio ni vyema kujitathmini na uone kama uko kwenye njia sahihi ama la. Kwa sababu kuweka juhudi kubwa na wakati uko kwenye njia ambayo sio sahihi ni kuzidi kupotea.