Ukiangalia miji mingi mikubwa, watu wanaoshikilia uchumi wa miji hiyo sio wazawa wa eneo hilo. Hata kwa ngazi ya kitaifa baadhi ya raia wa kigeni wanaoishi kwenye nchi huwa na mafanikio makubwa kuliko raia wa nchi husika. Umewahi kulifikiria hili? Umewahi kujiuliza ni nini kinasababisha haya kutokea?

ondoka

  Chukua mfano wa jiji la Dar es salaam, wazawa wa dar es salaam ni Wazaramo pamoja na makabila madogo kama vile Wandengereko na Wakwere. Dar es salaam kuna biashara nyingi kubwa, viwanda, mahoteli na majengo mengi makubwa, lakini wamiliki wa vitu hivi wachache sana ni wazawa wa dar es salaam.

  Hata ukiangalia majiji na miji mingine mikubwa kama Mwanza, Arusha, Mbeya na Moshi wengi wa wanaoshikilia uchumi wa maeneo hayo sio wazawa na kama ni wenyeji wa mikoa hiyo basi wametoka wilaya za jirani lakini sio hapo hapo wanapofanyia shughuli zao. Kwa mfano moshi utakuta wengi wenye biashara kubwa na vitega uchumi moshi mjini ni warombo, wamachame ama wakibosho. Hawa wote asili yao sio moshi mjini bali ni wilaya za jirani.

  Ukija kwa ngazi ya taifa raia wa kigeni huwa wanakuwa na uchumi bora kuliko sehemu kubwa ya wazawa. Kila siku tunapata habari kuna raia wengi wa kigeni wanaokuja nchini bila ya kuwa na kitu na baada ya muda wanakuwa na mafanikio makubwa. Sio kwa nchi yetu tu ama afrika tu, hata marekani raia wa kigeni waliohamia ama wanaofanya kazi wengi wana mafanikio makubwa kuliko wazawa. Wahindi, wachina na wakorea wanaonekana kuwa tishio sana kwa biashara na shughuli nyingine wanapofika marekani.

 

Kutokana na yote hayo unajifunza nini?

  Kinachoonekana moja kwa moja ni kwamba ni rahisi sana kufanikiwa ukiwa mbali na sehemu uliyozaliwa ama uliyokulia. Na jinsi umbali unavyozidi kuwa mkubwa ndivyo na mafanikio yanavyozidi kuwa makubwa. Aliyeondoka mkoa mmoja kwenda mwingine atafanikiwa ila sio sawa na anaeondoka nchi moja kwenda nyingine huyu atafanikiwa zaidi.

  Sababu kuu inayofanya watu kufanikiwa mbali na nyumbani ni uhuru mkubwa mtu anaoupata anapokuwa mbali na nyumbani. Unapokwenda sehemu ambayo ni ngeni kwako na hujulikani na wengi, unakuwa na uhuru mkubwa wa kufanya mambo mengi tofauti na ungekuwa sehemu ambayo unajulikana. Watu wanapokwenda kwenye maeneo mapya, hawachagui kazi, hawana cha kulalamikia na hawana pa kutegemea endapo mambo yatakwenda vibaya. Hali hii huwafanya kuwa na ari kubwa ya kufanya kazi na kufanikiwa. Kwa kuwa hakuna anaewajua katika maeneo hayo mapya hakuna atakayewaambia hawawezi, hakuna atakaewashangaa wakifanya kazi zinazoonekana sio za kiwango, hawajali wala hawalalamikii urasimu, wao wanachojua ni kimoja tu kusaka mafanikio.

  Gereza kubwa kwenye maisha yako ni nyumbani. Unapokaa nyumbani ama karibu na nyumbani(eneo uliokulia) kuna vitu vingi sana utashindwa kuvifanya kwa sababu ya watu wanaokufahamu na kukuzunguka. Ni rahisi sana kukatishwa tamaa na watu wanaokufahamu na wengi unaheshimu mawazo yao. Unakuwa na historia nyingi za watu wengi walioshindwa hivyo inakuwia vigumu kuanza kitu kipya.

  Ukiweza kuondoka nyumbani unakuwa umeondoka kwenye gereza hilo kubwa.

  Kama unaweza ondoka nyumbani na ukaanze maisha mapya sehemu mpya. Kama huwezi kuondoka basi ishi hapo kama wewe sio mzawa. Kwa kuweza kuwa na mawazo haya kwenye akili yako kunakurahisishia kuweza kukabiliana na changamoto hizo za kukaa nyumbani.

  Tahadhari, ninaposema uondoke nyumbani simaanishi uzamie meli na uende kwenye nchi za watu ukidhani utakwenda kufanikiwa, maisha yatakuwia magumu mno kama utafanya mambo kinyume na sheria zilizowekwa. Na pia kuna wengi waliofanikiwa sana kwa kuwa nyumbani, ila ukiwaangalia kwa karibu utaona uwepo wao nyumbani hawautumii hata kidogo kwenye shughuli zao za kiuchumi. Wengi wako huru sana kufanya chochote bila ya kuangalia wengine wanasema ama wanafanya nini.

  Kuna usemi maarufu unasema NABII HAKUBALIKI KWAO, unaweza kuuhusisha vizuri sana na hayo maelezo hapo juu.

  Nini maoni yako kuhusiana na kufanikiwa na kukaa nyumbani? Tafadhali tushirikishe kwa kuandika maoni hapo chini.