Moja ya tabia kubwa za binadamu ni kujilinganisha na wengine. Kujilinganisha huku huleta kushindana, kuigana na mwishowe kupotezana.
Katika jambo lolote unalofanya kuna watu wengine wengi tu wanaolifanya. Na kutokana na wingi huu wa watu ni rahisi sana kutaka kuwa bora zaidi ya wengine, kitu ambacho ni kizuri sana. Tatizo kubwa linaanzia pale unapotaka kuwa bora kwa kushindana. Kama utaanza mashindano na wenzako wanaofanya unachofanya basi huwezi kuwa bora zaidi yao bali utakuwa mmoja wao. Na kwa bahati mbaya zaidi unaeshindana nae anaweza kuwa ana uzoefu, na nguvu kubwa kuliko wewe. Kwa kushindana na mtu aliekuzidi vitu vingi ni dhahiri utakwenda kupoteza na utakata tamaa haraka sana na mwishowe utaaga mashindano mapema.
Kitu kingine kibaya kwenye kujilinganisha na wengine ni kuiga. Jamii ya sasa imekuwa na wavivu wengi wa kufikiri. Watu sasa wanaiga kila kitu, mtu akifungua biashara yake sehemu ikaonekana inalipa baada ya muda mfupi unakuta watu karibu kumi wanafanya biashara ile ile, kwenye eneo lile lile na kwa mbinu zile zile. Kuiga ni kubaya sana, ni vigumu sana kufanikiwa kwa kuiga. Na unapoiga bila hata ya kubadili kitu kimoja ni kudhalilisha uwezo wako na ubunifu wako.(soma; kila mtu ni mbunifu)
Matokeo ya mwisho ya kushindana na kuigana ni kupotezana. Unapojilinganisha na wengine na hatimaye kushindana nao ama kuiga wanachofanya kuna uwezekano mkubwa sana wa kupotezana. Kwa sababu unaweza kujikuta unafanya vitu visivyo vizuri kwa sababu tu kila mtu anavifanya. Unakuwa unajipa moyo kwamba kwa sababu kila mtu anafanya basi sio vibaya na wewe ukafanya, ni vibaya sana.
Kwa nini ujiumize kwa kujiingiza kwenye mashindano yasiyo ya msingi? Mashindano yoyote kwenye shughuli mbalimbali hayawezi kuwa ya haki na usawa. Kwa sababu kila mtu ana uwezo na vipaji vya pekee ambavyo haviwezi kupatikana kwa mtu mwingine yeyote.(soma; wewe ni wa pekee)
Usiumize hisia zako kwa kushindana na mtu unaetofautiana nae kila kitu. Kwa sababu unaeshindana nae anaweza kuwa ameanza zamani kuliko wewe, ana uzoefu mkubwa kuliko wewe, ana mtandao mkubwa kuliko wewe na pia anaweza kuwa na mtaji mkubwa kuliko wewe.
Kimbia mbio zako mwenyewe, angalia wenzako wanafanya nini kama njia ya kujifunza. Kamwe usijaribu kushindana nao na kama kuna vitu vizuri vya kuiga basi ongeza na ubunifu wako kidogo ili kupata kitu bora.Tumia uwezo wako wa pekee na vipaji ulivyonavyo na kuwa mbunifu kwa unachofanya.
Unapokimbia mbio zako mwenyewe maswali ya msingi kujiuliza ni je ninaelekea mbele? je ninaelekea kwenye malengo yangu? je njia ninayopita itanifikisha ninakotaka kufika?
Kwa kuwa na maswali haya kwenye kichwa chako utaifurahia sana safari yako na utafika kule unakokwenda kwa urahisi zaidi.