Mara nyingi tunapofanya jambo na kukawa na watu wanaotuangalia wakati tunafanya jambo hilo basi huwa tunalifanya kwa uangalifu mkubwa. Pia huwa tunalifanya jambo hilo kwa ubunifu na ustadi mkubwa kwa sababu tunajua kuna watu wanatuangalia kila hatua.
  Mara nyingine huwa tunafanya mambo kwa sababu tunajua tunaonekana tunafanya ama tumefanya. Mara nyingi hasa kwenye kazi wengi wetu tunapenda kufanya mambo tuonekane ni sisi tumefanya na tupate sifa kwa tulichokifanya.

  Sio jambo baya kwa wewe kufanya jambo kwa uangalifu mkubwa unapokuwa unaangaliwa na watu. Na pia sio jambo baya kupenda kupata sifa kwa jambo ulilofanya kama haufanyi kwa kujipendekeza. Ni tabia ya binadamu kupenda kuonekana wa muhimu na kuonekana wapekee. Na pia kila binadamu anapenda kusifiwa na kuonekana wa muhimu kwa jambo fulani analofanya.
  Tatizo kubwa linakuja pale tunapofanya mambo yetu binafsi. Kama ungekuwa kila jambo unalolifanya watu wanakuona na kukupa sifa kwa kufanya jambo hilo basi mpaka sasa ungekuwa umefanya mambo makubwa sana na ungekuwa umefanikisha mengi sana.
  Kama kila asubuhi unapoamka na kufanya mambo yako ya kujiendeleza binafsi kungekuwa na mtu anaekuangalia na kukusifia kwa jinsi unavyofanya vizuri basi ungefanya vizuri zaidi na hakuna hata siku moja ungeacha kufanya.
  Kama kila unapopanga malengo yako na mipango ya kuyafikia malengo hayo kungekuwa na mtu anakufuatilia na kukubali jinsi unavyofanya vizuri kwenye malengo yako basi ungekuwa na ari zaidi ya kutaka kufanya zaidi.
  Kama kila unapochukua kitabu na kujisomea ili kujiongezea maarifa ama unaposikiliza vitabu vilivyorekodiwa(audio books) ili kujiendeleza binafsi ungekuwa unaonekana na kila mtu na kusifiwa kwa jambo zuri unalofanya basi hakuna hata siku moja ungeacha kujisomea ama kusikiliza vitabu.
  Tatizo kubwa kwenye jamii yetu ni kwamba hakuna atakaekuona wakati unafanya yote hayo. Hata atakaekuoana kikubwa anachoweza kufanya ni kukukatisha tamaa na kukushawishi unapoteza muda.
 
  Kama hakuna anaetambua juhudi zetu je tufanye nini?
  Japo hakuna anaeona juhudi unazofanya sasa za kuyabadili maisha yako, usikate tamaa. Kusema tu usikate tamaa haiwezi kukusaidia kuvuka wakati huu mgumu. Kitu kikubwa unachoweza kukifanya ili uendelee kufanya unalofanya kwa ari zaidi ni kujiona kama kila unachofanya kila mtu anakuona.
  Fikiria kama kila mtu anakuangalia na anakufuatilia kila unachofanya. Na pia fikiria kila mtu anataka kukusifia ila tu anashindwa kufanya hivyo. Kama kweli utafanya kwa moyo mmoja itakuwia rahisi sana kuvuka wakati mgumu wa kukata tamaa kutokana na kutoonekana.
  Japokuwa hakuna anaekuona na kukusifia kwa juhudi kubwa unazofanya sasa jua kwamba siku moja utafanya mabadiliko makubwa na kila mtu ataona kazi zako na juhudi zako. Hii yote itatokea kama hutokata tamaa kwa kuona hakuna anayejali.