Kila mtu ana masaa 24 tu kwa siku. Na katika masaa haya 24 kwa siku kuna watu wamefanya mambo makubwa sana duniani na kuna wengine wamekuwa wanalalamika hawana muda wa kutosha. Yawezekana wewe ni mmoja wa watu ambao kila siku unaona muda haukuoshi na unashindwa kuelewa wanaofanya mambo makubwa wanawezaje kutumia muda huu ambao wote tunao sawa.

  Jinsi unavyoishi siku yako kwa mafanikio ndivyo unavyofanikiwa maishani. Hakuna siku moja ambapo mafanikio yataonekana mara moja, bali mafanikio ni mkusanyiko wa siku nyingi ulizoishi kwa mafanikio. Hivyo ili kufanikiwa kwenye maisha ni muhimu sana kufanikiwa kwenye siku moja.(soma; leo ni siku muhimu sana kwako)

saa ya maajabu

  Watu wengi waliofanya mambo makubwa duniani na kufanikiwa sana waliweza/wameweza kuzipanga siku zao vizuri. Na wengi wao wanajua umuhimu wa kutumia saa moja ya maajabu kupanga na kizianza siku zao. Kama na wewe unataka kufikia malengo yako maishani ni vyema ukaanza kutumia saa hii ya maajabu.

  Saa ya maajabu tunayzungumzia hapa ni saa kumi na moja alfajiri mpaka saa kumi na mbili alfajiri/asubuhi. Pia saa hii inaweza kuwa muda wowote asubuhi na mapema ambapo watu wengine wanakuwa bado wamelala.

  Kwa kuweza kuamka muda huo wa mapema asubuhi na kujipatia wewe mwenyew saa moja kwa ajili ya maisha yako, utaianza siku yako ukiwa na malengo ya kutekeleza. Utaianza siku yako ukijua ni kitu gani unakwenda kufanya na hivyo hutopoteza muda. Utakuwa na malengo na mipango ya kutekeleza kwa siku hivyo hutofuata mkumbo kwa kufanya kile ambacho kila mtu anafanya.

  Tenga saa moja asubuhi na mapema(na muda mzuri ni saa kumi na moja mpaka kumi na mbili) na uanze kutengeneza mafanikio ya maisha yako.

asubuhi na mapema

  Ufanye nini katika saa hii moja ili iwe na manufaa kwako?

  Kuna mambo matatu ya msingi sana ya kufanya ndani ya saa hii moja ambayo yataifanya siku yako kuwa ya mafanikio sana.

1. Kufanya mazoezi ya viungo. Ni muhimu sana kufanya mazoezi hasa wakati wa asubuhi maana mazoezi huchangamsha akili na kukuwezesha kufikiri kwa ufasaha zaidi. Pia mazoezi yanaimarisha afya na afya njema ni muhimu sana kwako kufikia malengo yako.

2. Kupitia malengo na mipango ya maisha yako. Katika muda huu wa asubuhi pitia malengo uliyojiwekea maishani na mipango mbalimbali ya kufikia malengo hayo. Pia weka mipango ya siku hiyo na jinsi ya kuitekeleza. Katika saa hii unaweza kuangalia ni kwa kiasi gani umefanikiwa ama umekaribia kuyafikia malengo yako.

 

3. Kujihamasisha. Ni muhimu sana kujihamasisha kabla hujianza siku yako. Hii itakusaidia kuweza kuimiliki siku yako na kuwa na mtizamo chanya juu ya maisha yako na kazi zako. Unaweza kujihamasisha kwa kujisomea kitabu, kusikiliza vitabu vilivyosomwa au kuangalia video mbalimbali za kuhamasisha. Kwa maelezo zaidi ya jinsi ya kujihamasisha asubuhi soma Hiki ndicho unachotakiwa kufanya kila siku asubuhi ili kufanikiwa.

  Kuna faida kubwa sana ya kuianza siku yako saa moja kabla ya ulimwengu mzima haujaamka. Muda huu unakuwa tulivu sana na hivyo unaweza kufikiri bila ya kuingiliwa na mtu yeyote au mazingira. Pia kuweza kuamka na kupanga siku yako asubuhi na mapema kunakupa nguvu kubwa tofauti na watu wengine wanaoanza siku kwa mazoea tu.

  Kama upo tayari kuamka asubuhi na mapema jiunge na mimi na watanzania wengine wanaotumia saa hii moja ya maajabu kwenye maisha yao. Jiunge nasi kwenye kundi la facebook kwa kubonyeza hapa kisha uombe kujiunga. Katika kundi hili tutakuwa tunahamasishana na kushirikishana faida mbalimbali za kuamka asubuhi na mapema na kuzipanga siku zetu.

  Jiunge kwenye kundi hili kama kweli upo tayari kuyabadili maisha yako. Mengi zaidi kuhusiana na kuamka mapema na jinsi ya kufanikiwa kwenye hilo yatapatikana kwenye kundi hilo.