Kwenye mtaa ninaoishi ndani ya miezi sita iliyopita nimeshuhudia watu watatu wakifilisiwa mali zao baada ya kushindwa kulipa mikopo ya biashara. Na wiki iliyopita maeneo haya haya ulifanyika mnada wa kuuza mali za watu zilizochukuliwa baada ya kushindwa kulipa mikopo.

  Niliona watu wakifurahia kununua friji kwa shilingi elfu themanini na vingine vingi kwa bei rahisi. Kwa upande wangu niliona kuna mengi ya kujifunza kutokana na matukio haya na kuna haja ya watu kujua mambo muhimu kabla ya kuchukua mikopo ya biashara.

biashara7

  Kuna watu wengi mtaani huku wanajaribu kujikwamua kimaisha kwa kufanya biashara ndogo ndogo na hata biashara za kati. Lakini kutokana na ukosefu wa elimu sahihi juu ya mambo ya fedha na biashara kwa ujumla watu wengi wanajikuta wanatumbukia kwenye madeni yanayowagharimu mali zao binafsi.(soma; tatizo sio fedha, tatizo ni wewe)

  Kama unampango wa kufanya biashara ama tayari upo kwenye biashara kuna mambo muhimu matatu ambayo unatakiwa kuyajua kabla hujachukua mkopo wa biashara.

1. Usichukue mkopo kwenda kuanza biashara. Kama hujawahi kufanya biashara usichukue mkopo kwenda kuanzia biashara. Katika biashara kuna changamoto nyingi sana, na hata uandae business plan ya aina gani bado kuna changamoto ambazo huwezi kuzikadiria kwenye business plan. Ila unapokuwa kwenye biashara kwa muda fulani unaanza kuelewa jinsi ya kukabiliana na changamoto hizo. Kuna sababu nzuri sana kwa mabenki kutokopesha watu ambao hawajakaa kwenye biashara kwa miezi sita. Kwa sababu miezi sita ya mwanzo ya biashara ndio wakati mgumu na wa kujifunza. Hivyo kutumia fedha za mkopo kujifunzia biashara inaweza kukuingiza kwenye matatizo makubwa. Anza kidogo kidogo kwa akiba uliyojiwekea ukishaweza kuzimudu changamoto za biashara ndipo uchukue mkopo.

 

2. Ujue mkopo kabla hujauchukua. Hapa ndio kuna tatizo kubwa sana. Watu wengi wanakimbilia kuchukua mkopo kabla ya kupiga mahesabu ni kiasi gani watakacholipa mpaka mkopo utakapoisha. Kila siku tunasikia watu wakilalamika kulipishwa zidi ya asilimia mia ya mkopo waliochukua. Yani mtu anakopeshwa milioni mbili ila mpaka anapomaliza kuulipa anajikuta amelipa milioni nne. Jua vizuri mahesabu ya riba na pia mrundikano wa riba hiyo(compound interest), kama hesabu hizi huzielewi vizuri tafuta msaada wa wanaoelewa wakusaidie.

 

3. Usitumie fedha ya mkopo kwa chakula. Hapa nako kuna shida kubwa kidogo. Unaweza kuwa na fedha ya mkopo wa biashara, halafu huna hela ya kula, unafanya nini? Kwa fikra za haraka haraka utafikiria kumega mkopo kidogo upate chakula. Kumbuka fedha ya mkopo ina riba, na ukishakula hakuna njia yoyote unayoweza kupata riba kwa chakula ulichokula. Na mbaya zaidi tabia hii ya kutumia fedha hiyo kwa chakula inaendelea kidogo kidogo mwishowe mkopo unaisha. Unahitaji nidhamu kubwa sana ili kutokuitumia fedha ya mkopo kwa matumizi mengine. Inabidi uwe tayari hata kukaa njaa ili kutafuta njia nyingine ya kupata mahitaji hayo badala ya kukimbilia kutumia fedha ya mkopo.

  Mkopo ni mzuri sana katika biashara. Ila kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu matumizi ya fedha mkopo unaweza kuwa kisirani sana kwa biashara yako. Mipango mizuri ya fedha na malengo mazuri yatakuwezesha kukuza biashara yako na kufanikiwa kwenye maisha. Ili kuweza kuwa na mipango mizuri jua jinsi ya kutumia saa moja ya maajabu kwenye maisha yako.(soma; saa moja ya maajabu maishani mwako)