Mwezi huu wa kumi na mbili ni mwezi ambao una mapumziko na sikukuu nyingi. Ni mwezi ambao kunakuwa na sherehe mbalimbali na pia watu wengi wanakuwa kwenye mapumziko ya kazi.

sikukuu

  Watu wengi wana taratibu mbalimbali unapofika mwezi huu wa mwisho wa mwaka. Wapo wanaofanya safari za mapumziko, wapo wanaorudi vijijini kwao na wapo wanaoendelea na shughuli zao kama kawaida.

  Mwezi huu kunakuwa na matumizi makubwa sana ya fedha na hivyo wengi hujikuta katika wakati mgumu mwanzoni mwa mwaka. Kila mwanzo wa mwaka fedha inakuwa ngumu kwa watu wengi kutokana na matumizi mabovu mwishoni mwa mwaka.

  Ili kuboresha maisha yako na kujiondolea nyakati ngumu zinazoweza kutokea mwanzoni mwa mwaka kuna mambo mengi unaweza kufanya. Hapa nitazungumzia mambo matano muhimu ambayo ukiyafanya wakati huu wa mwisho wa mwaka utauanza mwaka mwingine ukiwa na ari na nguvu za kutosha.

1. Tafakari mwaka unaokwenda kuisha. Katika mwaka huu kuna mambo mengi uliyopanga kufanya. Yapo uliyofanikiwa kufanya na kuna ambayo uliyoshindwa kufanya. Pia kuna vikwazo mbalimbali ulivyokutana navyo. Hivyo ni vyema kuchukua muda na kutafakari mwaka ulivyokwenda kwa upande wako.(soma; umefanya nini 2013?)

2. Tumia muda mwingi kukaa na familia na wale uwapendao. Kipindi hiki watoto wengi wapo likizo, na pia wazazi wengi wapo likizo pia. Huu ndio muda muhimu wa kuwa karibu na familia yako na kujifunza mengi ambayo unayakosa kutokana na majukumu ya kikazi. Tumia muda huu kuwa karibu na unaowapenda na wanaokupenda. Watembelee ndugu jamaa na marafiki na kubadilishana mambo mengi kuhusiana na maisha.

3. Pata muda wa kupumzika kweli. Japokuwa watu wengi wanakuwa na likizo kipindi hiki lakini wengi wanajikuta likizo zinaisha bila hata ya kupumzika. Wanajikuta wana majukumu mengi wakati huu wa likizo zaidi hata ya wakati wa kawaida wa kazi. Hata kama unavitu vingi vya kufanya bado unahitaji japo muda kidogo wa kupumzika. Kama shughuli zako hazikuruhusu kupumzika mwaka mzima basi unaweza kuwa na tatizo kubwa zaidi.

4. Kuwa mwangalifu katika matumizi. Kwa watu wengi wakati huu wanafanya matumizi yasiyo na mahesabu. Kwa sababu ni wakati wa sikukuu basi wananunua vitu ambavyo sio vya lazima, wanalewa sana na kufanya starehe nyingi. Kumbuka sikukuu sio mwisho wa dunia. Kuna maisha yataendelea baada ya msimu huu kupita, na kama usipokuwa makini utajuta sana mwanzoni mwa mwaka. Kuwa na bajeti ya matumizi, usisinunue kitu kwa sababu tu kila mtu ananunua, usinunue mti wa krismasi wa shilingi laki moja kwa sababu umeona unauzwa. Nunua vitu unavyohitaji na kulingana na uwezo wako.

5. Tumia muda huu wa mapumziko kuendeleza vipaji vyako ambavyo huvitumii wakati wa kazi. Una vipaji vingi ambavyo huwezi kuvionesha kwenye shughuli unazofanya. Wakati wa mapumziko unaweza kujifunza zaidi na kuendeleza kipaji chako. Inaweza kuwa uongozi, uandishi, uhamasishaji, uchoraji, uimbaji na mengine mengi. Pia tumia muda huu kujisomea vitabu mbalimbali vya kujifunza na kujihamasisha. Kama unataka vitabu vya kujisomea bonyeza hapa na kama unataka vitabu vya kusikiliza bonyeza hapa.

  Tumia msimu huu wa sikukuu tofauti na ulivyotumia misimu mingine. Tumia wakati huu kuyaboresha maisha yako na kuwa na mpango mzuri na maisha yako. Usifanye mambo ambayo hayana manufaa kwenye maisha yako na ya wanaokuzunguka.

  Nakutakia kila la kheri kwenye mapumziko yako na heri ya mwaka mpya wa 2014.