Nilikuwa nasikia hili neno Meditation kwa muda mrefu ila sikuwahi kuchukua muda mwingi wa kufuatilia umuhimu wake kwenye maisha yangu. Na hata nilipofuatilia kwa juu juu nilishawishika kwamba ina uhusiano na dini ya Kibudha hivyo nikaona ni kitu ambacho hakinihusu.
Nilikuwa nakosea sana, na kama wewe una fikra kama hizi ama hujawahi kufuatilia basi jifunze hapa na ujue faida za Meditation.
Moja ya malengo niliyojiwekea kwa mwaka 2014 ni kufanya meditation. Kwa kuwa sikuwahi kufanya kabla na kwakuwa sikuwahi kupata taarifa za kutosha kuhusu meditation nilichukua hatua ya kujifunza kuhusu meditation. Hivyo nilitafuta kitabu kizuri kuhusu meditation. Katika kutafuta kwangu nilipitia vitabu kadhaa ila nilikutana na kitabu kimoja kilichonipa mwanga kuhusu meditation kwa njia rahisi sana.
Kitabu hicho kinaitwa Wherever You Go, There You Are kilichoandikwa na Jon Kabat-Zinn. Kitabu hiki kimeelezea meditation kwa njia rahisi na ambayo unaweza kuanza kuifanya muda mfupi baada ya kukisoma na ukaanza kupata manufaa ya meditation.
Nini faida ya kufanya meditation?
Kwa siku chache ambazo nimefanya meditation(simple) nimeweza kuona manufaa makubwa kwangu na kwa jinsi ninavyofanya shughuli zangu.
1. Meditation imenisaidia kuweza kuishi maisha ya sasa. Kwa kufanya meditation imekuwa rahisi kwangu kuweza kusahau yaliyopita, kuacha kufikiri yatakayokuja na kufurahia hali ya sasa(wakati unafanya meditation). Hii inapunguza majuto na hofu nyingi.
2. Meditation imenisaidia kuondoa takataka nyingi kwenye akili yangu. Akili zetu binadamu ni kama sumaku ambayo inavuta vitu vinavyoendana nayo bila kujali usafi au uchafu, faida au hasara ya vitu hivyo. Kuna mawazo mengi yanayopandikizwa kwenye kichwa chako kila siku na kila wakati. Ili kuweza kuchuja takataka na kuacha vyenye manufaa meditation ina msaada mkubwa sana.
3. Meditation imenisaidia kuweza kuweka mawazo yote kwenye jambo moja ya muhimu(kufocus). Dunia ya sasa imejaa makelele mengi sana. Ni vigumu sana kukaa sehemu moja kwa saa nzima ukifanya mambo yako bila ya kuwaza vitu vingine. Kuna miziki mizuri, kuna matangazo ya kibiashara, kuna mitandao ya kijamii, kuna simu za mkononi na vingine vingi ambavyo vinatushawishi tuvitumie. Ili kuweza kufanya kazi kubwa na nzuri inayohitaji kufikiri sana(kama kuandika au kusoma) meditation ina mchango mkubwa sana.
Jinsi ya kufanya meditation.
Sijabobea kwa kiasi cha kuweza kukufundisha jinsi ya kufanya meditation. Japo naweza kukueleza kwa urahisi ila hutopata ule mtiririko mzuri uliotolewa kwenye kitabu hicho. Hivyo nakushauri udownload kitabu hicho kwa kubonyeza maandishi ya jina la kitabu(Wherever You Go, There You Are by Jon Kabat-Zinn) ili uweze kujifunza vizuri na uanze kufaidika na meditation.
Meditation ni kitu ambacho unaweza kufanya kwa dakika 5 au 10 au 15 ila faida zake ukazipata kwa siku nzima. Ni kitu ambacho hakihitaji fedha wala nguvu nyingi kufanya. Ni wewe tu kuamua kuanza kufanya na uanze kufaidika.
Weka meditation kama sehemu ya maisha yako na uone jinsi utakavyonufaika.
Endelea kutembelea AMKA MTANZANIA ili unufaike zaidi na jiunge na mtandao huu wa kutumiwa vitabu kwa njia ya email kwa kubonyeza hapa na kuweka email yako. Waalike na wengine nao ili wapate mambo haya mazuri.