Kama kuna njia rahisi ya wewe kushindwa kwenye chochote unachofanya basi ni kukopi na kupesti. Hii ni njia rahisi na ya uhakika ya kwamba lazima utashindwa. Hata kama hutashindwa basi utateseka sana na hutoweza kufikia mafanikio uliyotarajia kufikia.

  Kukopi na kupesti ni pale ambapo unachukua kitu kinachofanywa na mtu mwingine na kwenda kukifanya vile vile na kwa mtindo ule ule anaofanya mtu uliyeiga kwake. Huku ni kuiga kwa asilimia mia moja bila ya kubadili chochote. Katika baadhi ya mambo ya kawaida kukopi na kupesti kunaweza kusiwe na madhara makubwa sana. Ila ukiweka kukopi na kupesti kwenye shughuli za kiuchumi unazofanya umechagua njia rahisi ya kufeli.

copy cat

 

  Huku mitaani kuna watu wengi wanasumbuka kwenye biashara kwa sababu ya kukopi na kupesti. Kwa mfano mtu mmoja anaweza kufungua biashara fulani kwenye eneo baada ya muda unakuta watu wengine nao wanakuja kufungua biashara ile ile kwenye eneo lile lile na wanatumia mbinu zile zile anazotumia aliyeanza biashara ile. Ikitokea mambo yamekuwa magumu kwenye biashara ile yule aliyeanzisha anaweza kustahimili ila wale waliokopi na kupesti wanaishia kupotea.

  Wanapopotezwa kwenye biashara hiyo huishia kufikiri kwamba aliyeanzisha biashara hiyo na ambae amestahimili huenda amewachezea mchezo mchafu. Kwa hiyo hawajifunzi kilichowafanya washindwe ni nini na wanakwenda kurudia makosa yale yale na kujikuta wanashindwa tena.

  Unapokopi na kupesti unaangalia juu juu tu na unaangalia upande wa mbele wa biashara. Unapoingia kufanya kuna changamoto nyingi sana utakutana nazo, kama ulikuwa hujajipanga vizuri hiki ndio kinakuwa kifo chako au yanakuwa mateso yako.

  Anayefikiri na kufanya utafiti kabla ya kuingia kwenye kazi ama biashara yoyote siku zote huwa anafanikiwa na kufurahia shughuli hiyo. Hii inatokana na kwamba anakuwa ameshajiandaa na changamoto zitakazotokea na wakati mwingine anakuwa na mpango mbadala wa kumtoa wakati anapokaribia kushindwa kabisa. Wewe unayekuja kukopi na kupesti kwa sababu unaona anayefanya hivyo anafanikiwa, unapokutana na changamoto kali inakuondoa kabisa kwenye mstari.

 Kwa nini watu wengi wanakopi na kupesti?

  Kukopi na kupesti kumeshakuwa kama ndio mtindo wa maisha hasa kwetu sisi watanzania. Kila sehemu ambapo itaanzishwa biashara mpya na ikaonekana ina mafanikio basi baada ya muda mfupi utakuta watu karibu kumi wamefungua biashara ya aina hiyo hiyo. Angalia mfano wa biashara ya boda boda, baada ya kuonekana ni biashara rahisi ya kufanya watu wengi walikimbilia kununua boda boda na mpaka sasa boda boda zimekuwa nyingi kushinda hata idadi ya abiria. Wengi walioingia kwenye biashara hii kwa kuiga tu wanajikuta katika hali mbaya.

  Mfano mwingine ni waendesha blog wa Tanzania. Baada ya kuona baadhi ya watu wanaoendesha blog za kuripoti matukio wanapata faida kubwa, wimbi kubwa la watu wamekimbilia kufungua blog za aina hiyo. Kutokana na kutojipanga wakati wa kuanzisha blog hizo wanapokosa habari za kuripoti wanajikuta wanakopi habari za watu wengine na kuweka kwenye blog zao. Mara nyingine wanajikuta wanaweka habari zisizo za uhakika na nyingine za udhalilishaji kabisa(kama picha za uchi). Hii inawafanya kushindwa kupata mafanikio waliyotarajia, kuteseka kwenye uendeshaji na kudharaulika pale wanapoweka habari zisizo na maadili.

  Sababu kubwa inayofanya watu wengi wakopi na kupesti ni uvivu wa kufikiri. Kama mtu akiamua kukaa chini na kufikiri kwa kina na kuangalia fursa anayotaka kuichukua kisha kuangalia uwezo na vipaji alivyonavyo basi anaweza kutoka na aina bora ya kazi ama biashara ambayo atafurahia kufanya na atapata mafanikio makubwa sana.

  Tatizo kubwa hutaki kufikiri, unataka majibu ya haraka haraka na unataka kuona mafanikio ya haraka haraka. Kitu chochote cha haraka haraka mwisho wake huwa sio mzuri. Una uwezo mkubwa sana ulioko ndani yako, una vipaji vya kipekee na una hazina kubwa sana ambayo ni akili yako. Tumia vitu hivi kuchambua fursa unayotaka kuingia kisha tengeneza mpango wako wa ushindi.

  Sijasema utafute kitu kipya kabisa cha kufanya, hutokipata. Nachokushauri ni uwe mbunifu kwenye kile unachofanya na ufanye kwa njia tofauti kulingana na uwezo wako wewe. Usiige kitu kwa asilimia mia moja, utashindwa vibaya sana.