Unaweza kuwa na malengo na mipango mikubwa kwenye maisha yako. Ila kama afya yako haitokuwa nzuri ni vigumu sana kufika unakotarajia kufika. Hata kama unapenda kuwasaidia watu kwa kiasi gani kama afya yako sio nzuri wewe ndio utahitaji msaada mkubwa zaidi. Hivyo linapokuja swala la afya ni muhimu sana kuipa afya yako kipaumbele cha kwanza kabla ya mambo mengine yote. Tumekuwa tukichukulia swala la afya kwa urahisi sana kutokana na madhara yake kutoonekana mara moja.

afya3

  Kwa kipindi kirefu magonjwa ya kuambukiza yamekuwa tishio kwenye nchi zinazoendelea. Ila kwa kipindi cha hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukizwa. Magonjwa haya kama kisukari, kensa, shinikizo la damu, uzito uliozidi na magonjwa ya akili yameanza kuwa tishio kubwa kwa afya za watu.

  Magonjwa haya yasiyoambukizwa chanzo chake kikubwa ni aina au mifumo ya maisha tunayoishi. Leo tutaangalia mambo mawili unayopuuzia ambayo yanakusababisha kupata magonjwa haya yasiyoambukizwa.

1. Vitu unavyoingiza kwenye mwili wako.

  Mifumo ya sasa ya maisha inafanya watu wengi kuingiza sumu nyingi sana kwenye miili yao. Vitu unavyokula, kunywa au kuvuta vinaweza kuwa na sumu mbaya sana ambazo zitakusababishia magonjwa kama kensa.

  Kula vyakula vinavyotengenezwa haraka na vyenye kiwango kikubwa cha mafuta kunasababisha magonjwa kama presha na uzito uliozidi. Unywaji wa pombe na vinywaji vingine vinavyohifadhiwa kwa kemikali una sumu ambazo zinaathari kubwa kwenye mwili wako.

  Utumiaji wa madawa ya kulevya na uvutaji wa bangi umechangia kuleta watu wengi wenye magonjwa ya akili.

  Uvutaji sigara unasemekana kuchangia kwa asilimia kubwa sana kwenye magonjwa ya kensa.

afya4afya1

  Ili kuepukana na hili punguza au acha kabisa kutumia vyakula au vinywaji vinavyoweza kuwa na sumu. Kula mlo kamili. Kwa mtu mzima unatakiwa kula mlo wenye mafuta kidogo, chumvi kidogo, wanga na protini kwa wastani na mbogamboga, matunda na maji kwa wingi sana. Hii itakusaidia kuwa na uzito wa wastani na kukuepusha na maradhi yasiyoambukizwa.

  Pia jiepusha na utumiaji wa madawa ya kulevya na acha kabisa kuvuta sigara, kama unavuta.

2. Kutofanya mazoezi.

  Tatizo lingine kubwa linalochangia kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukizwa ni kutofanya mazoezi. Watu wengi hasa wanaokaa maeneo ya mjini na wanaofanya kazi za ofisini wanaongoza kwa kuwa na uzito uliozidi na kupata magonjwa kama presha na kisukari.

  Kama unafanya kazi ofisini kuna uwezekano unakaa zaidi ya masaa kumi na mbili kwa siku. Unaondoka nyumbani unakaa kwenye gari, unafika ofisini unakaa kufanya kazi, unarudi nyumbani ukiwa umekaa kwenye gari na unapofika nyumbani unakaa kupumzika au kuangalia tv. Kama unakwenda kujipumzisha sehemu nyingine kama baa nako unakaa. Kwa wastani unakaa muda mrefu sana hivyo vyakula unavyokula vinakuwa havitumiwi na hivyo kuhifadhiwa kwenye mwili. Hii inasababisha uzito uliozidi na kukuletea maradhi.

mazoezi

  Kuepukana na hili jiwekee utaratibu wa kufanya mazoezi. Inashauriwa kupata angalau masaa mawili kwa wiki ya kufanya mazoezi. Ukiweza kupata angalau nusu saa kila siku ya kufanya mazoezi inakuwa bora zaidi kwako.

  Kama unaona huna muda wa kufanya mazoezi anza kwa kuamka nusu saa kabla ya muda wako wa kawaida kuamka kisha tumia muda huo kufanya mazoezi. Unaweza kufanya mazoezi ya aina yoyote ambayo yatakutoa jasho. Unaweza kukimbia, kuruka kamba, kutembea na mazoezi mengineyo.

  Kuna mambo mengi yanaathiri afya zetu ila haya mawili yamekuwa yakipuuziwa na watu wengi. Anza kutilia mkazo mambo haya ili uweze kufikia malengo yako ya mafanikio uliyojiwekea.