Kuna sheria moja muhimu ambayo inatawala kwenye maisha yetu binadamu. Sheria hii iko wazi ila ni wachache sana wanaojua umuhimu wake na kuitumia kufanikiwa. Ndio maana nimeiita siri muhimu kwenye maisha, kazi na hata biashara. Sheria hiyo ni kwamba kila kitu kinakufa. Huenda tayari unaijua sheria hii na unajiuliza kwa nini nasema ni siri kubwa. Kujua kwamba kila kitu kinakufa hakuwezi kukusaidia sana, ila kujua jinsi ya kutumia sheria hii ikakupelekea kufanikiwa kwenye kazi au biashara zako ni muhimu sana. Hapa tutaangalia jinsi ya kutumia sheria hii muhimu kwa mafanikio yako.

  Kabla hatujaizungumzia sheria hii muhimu hebu tuangalie mifano halisi inayotokea kwenye maisha yetu ya kila siku. Kama umewahi kuanza kazi mpya utakuwa umeshagundua kwamba mwanzoni unapata mafanikio makubwa ila siku zinavyozidi kwenda huone kama mafanikio yanaongezeka. Kama umewahi kufanya biashara au kuona biashara inayoendeshwa utagundua kwamba mwanzoni biashara inakuwa kwa kasi sana ila baadae inasimama na kunakuwa hakuna mabadiliko makubwa. Na kuna uwezekano ikafa muda unavyozidi kwenda.

  Biashara nyingi kubwa na ndogo ziko kwenye ukomo wa ukuaji. Unakuta biashara iko vile vile miaka miwili hata mitano. Unafikiri hali hii inatokana na nini? Hii inatokana na sheria kwamba kila kitu kinakufa, na kutokana na watu kushindwa kutumia sheria hii biashara zinakufa haraka kuliko walivyofikiri.

 

Kila biashara inakufa.

Biashara yoyote inapoanzishwa huwa inapitia vipindi vinne muhimu. Vipindi hivyo ni kama inavyooneshwa kwenye mchoro hapo chini.

 

ukuaji wa biashara

 

1. Kipindi cha kwanza; mwanzo wa biashara.

Kipindi hiki ndio mwanzo wa biashara. Katika kipindi hiki ndio biashara inakuwa inajijenga na bado haijapata wateja wengi. Ukuaji wa biashara na faida inakuwa kidogo sana kwenye biashara wakati huu.

2. Kipindi cha pili; ukuaji wa kasi wa biashara.

Katika kipindi hiki biashara inakuwa kwa kasi sana. Wateja ni wengi na faida ni kubwa kwenye kipindi hiki. Hapa ndipo watu wanaifurahia sana biashara na kunufaika.

3. Kipindi cha tatu; kusimama kwa ukuaji wa biashara.

Katika kipindi hiki ukuaji wa biashara unasimama. Faida haionekani kuongezeka kwa kasi kama mwanzo. Ni katika wakati huu ambapo watu wengi wameshaijua biashara hiyo na wengi wameanza kuifanya. Kwenye wakati huu unakuwa na washindani wengi kwenye biashara yako.

4. Kipindi cha nne; kuanza kuanguka kwa biashara.

Inapofika katika kipindi hiki biashara inaanza kuleta hasara badala ya faida. Ni katika kipindi hiki ambapo wateja wamepungua na faida ni kidogo na inashindwa kujiendesha yenyewe. Hii inatokana na soko kuwa na watu wengi wanaofanya biashara unayofanya na ushindani kuwa mkubwa sana.

 

Unawezaje kutumia hatua hizo nne kukuza biashara yako ili isife?

Biashara nyingi hushindwa kuendelea kwa kuwa wamiliki hawajui wafanye nini kwenye kila hatua ya maisha ya biashara. Biashara zilizodumu muda mrefu duniani na kufanikiwa sana wamiliki walijua na wanajua ni vitu gani vya kufanya ili biashara isife. Katika hatua ya tatu ya biashara ndipo penye changamoto kubwa sana kwa wafanyabiashara wengi hasa wa kitanzania.

  Hapa tutazungumza mambo matatu muhimu ya kufanya ili kuendelea kukua na kuepuka kufa kwenye hatua ya tatu na ya nne.

  Mambo matatu muhimu ya kufanya ili biashara idumu na kukua.

1. Kuendelea kujifunza kila mara.

Kwa kuwa mbinu za ufanyaji biashara zinabadilika kila siku ni muhimu kuwa na mbinu mpya za kufanya biashara yako. Ili uweze kupata mbinu hizi mpya ni lazima uwe unajifunza kila siku kuhusiana na biashara yako. Kama biashara yako umeajiri watu inakubidi uwe unatoa mafunzo ya mara kwa mara ili wafanyakazi wako wawe na uzalishaji wa hali ya juu.

  Kujua mbinu mbalimbali za kutatua changamoto za kila siku kwenye biashara itakusaidia kuweza kuvuka nyakati ngumu. Pia utapata mbinu mbalimbali za kuweza kupambana na ushindani wa soko.

  Unaweza kupata mafunzo wewe binafsi kwa kujisomea vitabu, kuhudhuria mafunzo na semina au kusoma kwenye mitandao. Mafunzo kwa wafanyakazi wako unaweza kutafuta watoaji wa mafunzo na wakaja kuwapa mafunzo wafanyakazi wako.

  Kiasi chochote cha fedha utakachotumia kwenye mafunzo yako binafsi na mafunzo ya wafanyakazi wako kitakuletea faida kubwa sana. Kama wewe pamoja na wafanyakazi wako mtakuwa na mafunzo sahihi juu ya biashara na maendeleo binafsi uzalishaji utakuwa mkubwa sana.

2. Kuwa mbunifu.

Hakuna kitu muhimu kwenye biashara kama ubunifu. Ubunifu ndio utakaokufanya uweze kupenyeza kwenye ushindani unaoletwa na watu wengine wanaofanya biashara unayofanya. Bila ya kuwa na ubunifu ni rahisi sana kwa biashara kushindwa kuhimili changamoto za soko na kuishia kufa.

  Katika ubunifu unaweza kuwa unatoa bidhaa za aina tofauti kwa wakati mmoja ili kuwa na faida zaidi ya wanaotoa bidhaa moja. Pia unaweza kuwa unatoa bidhaa na baadae kutoa bidhaa hiyo hiyo ila ikiwa imeongezewa sifa nyingi zaidi. Mfano mzuri ni makampuni makubwa ya simu Apple na Samsung. Makampuni haya yamekuwa yakitoa simu ambazo zinakwenda zikiongezeka kwa ubora. Kwa mfano Apple wametoa simu aina za Iphone 1, 2, 3, 4 na hata 5. Ukiangalia kwa makini hakuna tofauti kubwa sana kati ya toleo moja na toleo jingine. Ila uwepo wa toleo jipya hufanya hata wale wenye matoleo ya zamani kutaka kununua toleo hilo jipya. Na pia kama kulikuwa na watu wameiga toleo la kwanza hawawezi kuleta ushindani kwenye toleo jipya. Mbinu hii imekuwa ikitumika na wafanya biashara wakubwa na imewawezesha kufanikiwa sana.

  Angalia ni jinsi gani unaweza kutumia ubunifu kuboresha biashara yako ili kila siku iwe na mambo mapya. Biashara inapokuwa mpya kila mara inafanya wateja wasiichoke na washindani wasikusumbue.

3. Fanya utafiti endelevu.

Ni muhimu sana kuwa na utafiti endelevu kwenye biashara yako. Tafiti soko lako na masoko mengine ambayo bado hujayafikia. Fanya utafiti wa kujua soko linataka nini cha ziada kutoka kwenye biashara yako. Pia fanya utafiti wa jinsi gani biashara yako inaweza kukua zaidi na kufikia wateja wengi.

  Makampuni makubwa yanawekeza sana kwenye utafiti na maendeleo. Hii ndio inawafanya wanaendelea kutawala soko na kuwa na ubunifu mkubwa. Wafanyabiashara wengi wa Tanzania hawawekezi kwenye utafiti juu ya biashara zao.

  Ni katika utafiti ambapo utapata mbinu mbalimbali za kutawala soko na kuongeza wigo wa soko lako. Ni katika utafiti ambapo utajua ni kitu gani washindani wako wanafanya ila wewe hufanyi na inapelekea wewe kupoteza.

  Kama mpaka sasa hujawekeza kwenye utafiti kuhusu biashara yako anza kufanya hivyo ili uzuie biashara yako kufa kifo cha asili.

  Mbinu hizi tatu muhimu zinaweza kukusaidia sana kutengeneza biashara ambayo inakua kila siku. Kuna mbinu nyingi ambazo tutaendelea kujifunza kwenye mtandao huu, ila anza na hizo tatu za muhimu na uanze kupata mafanikio makubwa kwenye biashara yako.

 

Kama una swali lolote kuhusiana na mbinu hizo au jinsi ya kutatua changamoto nyingine za biashara yako weka maoni yako hapo chini au wasiliana na mimi kwa msaada zaidi.