Mpaka sasa umeshajua ya kwamba ili ufanikiwe ni muhimu ufanye kitu ambacho unakipenda. Na ili upende unachokipenda ni muhmu uwe unafanya kitu kinachotokana na kipaji chako.(soma; kama unataka kufanikiwa usifanye kazi) Je unakijua kipaji au vipaji vilivyopo ndani yako?

  Moja ya swali ambalo watu wengi huwa wanauliza ni jinsi ya kugundua wao wana vipaji gani. Kwa bahati mbaya sana huwa binadamu hazaliwi na msaada wa kutumia kama ilivyo kwenye uzalishaji wa mashine mbalimbali. Na pia wakati wa utoto unaweza kuwa ulionesha vipaji vyako ila wazazi au walezi wako hawakuweza kuvitambua.

kipaji

  Ulipoingia kwenye mfumo wa elimu ndio kabisa ulikwenda kuua vipaji vyako. Kwa sababu kwenye mfumo wa elimu haijalishi una vipaji gani, lengo kubwa ni kufaulu. Huenda umemaliza kusoma na hata kazi unafanya ila umegundua ulichosomea au kazi unayofanya huifurahii.

  Katika wakati kama huu unafikiri umeshapoteza muda wako mwingi na huwezi tena kujua kipaji chako. Hivyo unajilazimisha kukaa kwenye kazi ambayo huifurahii ili tu kusogeza siku. Hivyo ndivyo maisha yanavyotakiwa kwenda? Unatakiwa kuishi maisha yenye furaha na sio kusukuma siku ziende.

  Haijalishi umri wako umekwenda kiasi gani au umekaa kwenye kazi muda mrefu sana, ukitaka kubadilika hakuna kinachokuzuia. Katika wakati wowote kwenye maisha yako unaweza kubadili uelekeo wa maisha yako kama unaona unakoelekea hakuna matumaini yoyote. Unaweza kuvigundua vipaji vyako hata kama ulishavisahau kabisa au hukupata nafasi ya kuvijua.

  Kuna njia kuu tatu za kujua vipaji vyako. Njia hizo ni;

1. Kufanya mambo mengi.

Moja ya njia za kujua vipaji vyako ni kufanya mambo mengi na kujua ni yapi unayafurahia kufanya. Njia hii ni ya kujaribu na kukosea. Katika njia hii unajaribu kufanya mambo tofauti tofauti na katika hayo kuna machache utafurahia kuyafanya. Katika hayo machache utajua vipaji vyako ni nini.

  Njia hii ndiyo inatumika na watu wengi sana kujua vipaji vyao. Usione aibu kujaribu mambo mapya kwa kuogopa kushindwa. Fanya mambo mengi ambayo hujawahi kuyafanya, jaribu kucheza michezo mbalimbali, jaribu kuimba, jaribu kuandika, jaribu kujifunza kucheza vyombo, pia jaribu kuchora. Jaribu vitu vingi uwezavyo ili kujua ni kipi unafurahia kufanya.

  Kwa njia hii itakuchukua muda mrefu kidogo kufikia kile unachopenda kufanya. Usiogope kuhusu muda, maana muda huu ni muhimu kuliko ambao unaendelea kupoteza kwa kufanya kitu ambacho hufurahii.

2. Fikiri kama fedha isingekuwa tatizo.

Kwa asilimia kubwa unafanya unachofanya kwa sababu ya fedha. Unawezakuwa hufurahii kabisa unachofanya ila kwa vile ndio kinakupatia fedha za kuendesha maisha inakubidi uendelee kukifanya. Habari mbaya kwako ni kwamba huwezi kufanikiwa sana kwenye jambo lolote kama kinachokusukuma kufanya ni fedha(soma; kama unafanya ili upate fedha utateseka).

  Ili kugundua vipaji vyako na kuacha kutumikia tu fedha jiulize kama fedha isingekuwa tatizo kwako ungefanya shughuli gani? Yaani kama kila siku ungekuwa na uhakika wa kupata fedha unayohitaji ili kuendesha maisha yako hata kama hufanyi shughuli yoyote, ungetumia muda wako kufanya nini? Hicho kinachokujia kwenye mawazo yako ndio kipaji chako.

3. Ni shughuli au watu gani unawahusudu?

Unaweza kubisha mbele za watu ila unapokuwa mwenyewe kuna watu ukiwaona unavutiwa sana na shughuli wanazofanya. Wakati mwingine ukiona habari yoyote inayohusisha shughuli hiyo unavutiwa kuifuatilia. Shughuli hizi ambazo ukiziangalia unavutiwa kuzifuatilia au wakati mwingine unatamani kuzifanya ndipo kipaji chako kilipo. Unaweza kuwa unavutiwa na vitu fulani kwa muda mrefu ila kwa kuwa hujisikilizi wewe mwenyewe unashindwa kupata kujua vipaji vyako.

  Ni muhimu sana kujua kipaji au vipaji vyako ili kuweza kufanikiwa kwenye maisha yako. Ni rahisi kujua vipaji vyako kama kweli utakuwa na nia ya kuvijua. Acha kuteseka kwenye maisha yako kwa kujisukuma kufanya shughuli ambazo huzifurahii hata kidogo. Jua ni vipaji gani unavyo na anza kuviendeleza ili uweze kufurahia maisha yako.