Rafiki yangu mpendwa,

Safari ya mafanikio kwenye maisha, haijawahi kuwa rahisi kwa mtu yeyote yule. Kila ambaye amefanikiwa, amepitia magumu na changamoto mbalimbali.

Wengi wanaoshindwa kufanikiwa, siyo kwa sababu hawawezi, bali kwa sababu hawakujua jinsi ya kuvuka yale magumu wanayokutana nayo.

Mtazamo wa kwanza ambao watu wanakuwa nao pale wanapokutana na magumu na changamoto ni mwisho wa safari. Yaani yale magumu na changamoto ambazo wanakutana nazo, wanachukulia ndiyo mwisho wa safari yao.

Hivyo hatua ya kwanza kwenye kuvuka magumu na changamoto ni kutokuyachukulia kama mwisho. Unapopitia magumu hupaswi kuona ndiyo mwisho, bali unapaswa kuona ndiyo mwanzo wa safari. Kile kinachokuzuia kwenye njia, inakuwa ndiyo njia yenyewe.

Watu wengi wanapoanza biashara, huwa wanakuwa na matumaini makubwa ya kufanikiwa. Kila mpango wa biashara huwa una faida na mafanikio. Lakini kwenye uhalisia, biashara zinaingiza hasara na kufa.

Watu wanapoingia kwenye biashara kwa uhalisia, ndiyo wanapokaribishwa na machungu ya dunia ambayo yanawasumbua sana. Hapo ndipo panapoamua kama mtu utafanikiwa au utashindwa.

Kwenye biashara, yale magumu unayokuwa unapitia ni zawadi nzuri sana ya mafanikio kwenye biashara. Kwa sababu magumu hayo yanakufanya uwe imara katika kujenga na kukuza biashara yenye mafanikio.

Chukulia mfano wa mtaji. Mtu anayeanza biashara kwa mtaji ambao ameupata kwa urahisi, huwa anaupoteza haraka kuliko yule ambaye amekusanya mtaji wake mwenyewe kwa muda mrefu. Ndiyo maana hata benki huwa hazitoi mikopo kwa mtu anayeenda kuanza biashara, kwa sababu zinajua kwa sehemu kubwa, mtaji wa mara ya kwanza unaenda kupotea.

Unapopitia ugumu kwenye kupata wateja, inakusukuma uwe na mfumo mzuri wa kupata wateja wa biashara yako. Kufanya hivyo kunakujengea kujiamini na kuwa na uhakika wa kupata wateja mara zote.

Kadhalika unapopitia ugumu wa kuajiri wafanyakazi kwenye biashara yako, inakusukuma utengeneze mfumo mzuri wa kupata na kujenga wafanyakazi wazuri kwenye biashara.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA, nimefafanua kwa undani zawadi hii ya magumu unayokuwa unapitia kwenye biashara na jinsi ya kuyatumia kujenga biashara yenye mafanikio. Karibu ujifunze hapo chini.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.