3434; Gharama hazikwepeki.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Mafanikio ya aina yoyote ile huwa yana gharama ambayo lazima mtu uilipe ili uweze kuyapata.

Sehemu kubwa ya maisha ya watu imekuwa inatumika kukwepa kulipa gharama hizo za mafanikio.

Lakini kwa bahati mbaya sana, gharama hizo zimekuwa hazikwepeki.
Yale ambayo watu wanadanganyika yanaondoa gharama za mafanikio, yanakuwa yamezisogeza tu mbele.

Baadaye mtu anakuja kulipa gharama zote ambazo hakulipa huko nyuma.
Na anazilipa pamoja na riba kubwa sana, kwa sababu alizisogeza mbele kwa mkopo.

Kama kuna kitu ambacho unahitajika kununua ili kukamilisha baadhi ya majukumu yako muhimu, lakini ukaona huwezi kumudu kununua, kadiri unavyoendelea bila kuwa na kitu hicho, unakilipia gharama.
Kwa kukosa matokeo ambayo yangetokana na kitu hicho inakugharimu zaidi.

Kama upo tayari kulipa gharama upate kitu na kuna cha bei ndogo na bei kubwa, kama utachagua cha bei ndogo, utaishia kulipa gharama kubwa zaidi kwenye matokeo kuliko uliyookoa.
Tofauti inayokuwepo kwenye bei ni zaidi ya bei, kuna thamani tofauti kwenye bei hizo tofauti.
Unapochukua cha bei ndogo na kuacha cha bei kubwa, unalipa gharama kwa thamani unayoikosa.

Halafu kuna wale ambao wamekuwa wanakimbizana na njia za mkato za kufanikiwa haraka bila ya kuingia gharama yoyote.
Hawa ndiyo huwa wanalipa gharama kubwa zaidi, siyo tu kwenye fedha, bali kwenye kila kitu.
Wanaingia gharama ya muda, nguvu, umakini na sifa.

Kanuni kuu ya mafanikio ni ile ile na haijawahi kubadilika; JUA GHARAMA UNAZOPASWA KULIPA NA ZILIPE MAPEMA NA KWA UKAMILIFU.

Ukiona huwezi kumudu gharama, unaishia kulipa kwa kutokulipa gharama hizo.
Ukitaka kulipa rahisi, unaishia kulipa zaidi kwa thamani ndogo unayokuwa umechagua.
Na ukitaka kukwepa kabisa gharama hizo, unaharibu kila kitu.

JUA GHARAMA, LIPA GHARAMA. HAZIKWEPEKI KWENYE MAFANIKIO.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe