Ili uweze kufanikiwa kwenye uongozi kuna mambo muhimu unatakiwa kuwa unafanya na pia kuna mambo mengine unatakiwa kuepuka kufanya.

Katika makala zilizopita tumekuwa tukiangalia mambo muhimu ya kufanya ili kuweza kufanikiwa kwenye uongozi. Ili kuwa kiongozi mzuri ni muhimu kuwa na maono, ushawishi, ushirikiano na uadilifu. Kuwa na mpango mikubwa na kuweza kuwashawishi wengine kuifikia ili kuboresha maisha yako ni tabia moja inayoweza kukutengeneza kuwa kiongozi bora.

Pamoja na hayo kuna mambo ukiyafanya unaweza kuharibu sana uongozi wako bila ya kujali umeutengeneza kwa muda gani. Mambo haya yamekuwa yakifanywa na watu wengi na ndio sababu kubwa ya wao kushindwa kuwa viongozi wazuri. Kwa kuwa wewe unajifunza kuwa kiongozi bora, ni muhimu sana ukayajua mambo haya ili usije kuyafanya na ikakugharimu kwenye maisha yako na uongozi wako.

Hapa nitaongelea makosa kubwa matano unayoweza kufanya yakaharibu kabisa uongozi wako. Makosa hayo ni kama ifuatavyo.

1. Kutaka kupendwa badala ya kuheshimika.

Ni rahisi sana kwa kiongozi kutaka watu wampende yeye kutokana na uongozi wake. Ili kutimiza hilo anajikuta anafanya mambo ya kuwafurahisha watu badala ya kufanya mambo yatakayowasaidia watu. Katika uongozi kuna maamuzi unaweza kufanya watu wasikuelewe kwa sababu wewe una maono, baadae mafanikio yanapoonekana watu hukuheshimu sana kama kiongozi. Ila ukitaka kuwafurahisha watu hutoweza kufanya mambo ya kuwasaidia. Usitake kupendwa na watu bali jenga kuheshimiwa na watu kutokana na maamuzi unayofanya yenye manufaa kwenye maisha yao.

2. Kutochukua ushauri na msaada wa wengine.

Kuna wakati kiongozi anaweza kuona yeye yupo juu ya wengine hivyo ushauri wake ndio sahihi. Pia anafikiri hahitaji msaada wowote kutoka kwa anaowaongoza. Hili ni kosa kubwa sana unaloweza kufanya wewe kama kiongozi. Bila ya kujali ngazi yako ya uongozi ni muhimu sana kuchukua ushauri kwa unaowaongoza. Wakati mwingine kuna mawazo mazuri sana kutoka kwa unaowaongoza, pia unaweza kupata msaada mkubwa kutoka kwa unaowaongoza.

3. Kutokujali na kuendeleza vipaji vya wengine.

Watu unaowaongoza wana vipaji na uwezo mkubwa sana. Kazi yako kama kiongozi ni kuendeleza vipaji hivi ili kuwawezesha kufikia malengo makubwa kwenye maisha yao. Kama kiongozi hutothamini vipaji na uwezo wa watu wako itakuwa vigumu sana kwao kukufuata na hii itaathiri uongozi wako.

4. Kushindwa kupanga majukumu vizuri kwa unaowaongoza.

Kama wewe ni kiongozi wa timu au kikundi ambacho kinatakiwa kukamilisha jukumu fulani ni muhimu sana kila mtu kujua jukumu lake ni nini na anawezaje kulitimiza. Kushindwa kupanga na kueleza vizuri majukumu ya kila mtu ni chanzo kikubwa cha kupungua kwa uzalishaji kwenye maeneo mengi ya kazi. Wewe kama kiongozi hakikisha wafuasi wako wanajua majukumu yao na njia za kuyatimiza.

5. Kushindwa kutoa taarifa kwa watu.

Ni muhimu sana kutoa taarifa kwa wale unaowaongoza. Watu wanataka kujua ni mafanikio kiasi gani yamefikiwa na ni changamoto gani zinawarudisha nyuma. Wewe kama kiongozi unajukumu la kutoa taarifa sahihi na kwa muda sahihi kwa watu unaowaongoza. Hii itawafanya kuwa sehemu ya uongozi wako na kuufurahia.

Kama ukiweza kuepuka mambo haya matano, utafanikiwa sana kwenye uongozi wako. Kumbuka ni muhimu sana kwako kuwa kiongozi kwenye maisha yako. Na unaweza kujifunza kuwa kiongozi bora. Weka email yako hapo juu(kwenye blog) ili kupata makala hizi za mafunzo ya uongozi moja kwa moja kwenye email yako.

Karibu sana.