Kumekuwa na usemi mmoja maarufu sana kwamba watanzania ni wavivu wa kusoma. Na ili kudhibitisha usemi huu watanzania wengi wanapohitimu masomo yao huwa wanafurahia sana kwa kuwa wanajua huo ndio mwisho wa mateso ya kutakiwa kusoma kila siku. Na wewe una fikra kama hizi? Unakosea sana na unakosa mengi sana kama huna tabia ya kujisomea.

Kujisomea ni muhimu sana na umuhimu wake ni namba mbili kwenye maisha yako ukishaweka kula. Katika ulimwengu wa sasa ambao mambo yanabadilika kwa kasi sana wale wenye ujuzi au uelewa mkubwa ndio wanaoweza kuponea, wengine wengi wanapotezwa na kasi hii.

Kama hujawahi kutafakari na kujua kwa nini ni muhimu sana kujisomea tena kila siku hapa nakupa sababu tano muhimu ambazo hutakiwi kuzikosa kwenye maisha yako.

READING

1. Kujisomea kunakuongezea ujuzi na utaalamu.

Hili halina ubishi kwa sababu wote tunakubaliana kwamba yule ambaye anasoma mambo mapya mara kwa mara yupo kwenye faida ya kujua mengi ukilinganisha na yule ambaye hajisomei. Hivyo kama unataka kuwa mtaalamu au kubobea kwenye kazi au biashara unayofanya ni muhimu sana uwe unajisomea. Unajua ili ufanikiwe kwenye kile unachofanya unahitaji nini? Kuwa bora zaidi ya yeyote anayefanya unachofanya wewe, na ili kuwa bora unahitaji kuwa na tabia ya kujisomea na kujiendeleza.

2. Kujisomea kunakusaidia kuongeza uelewa wako juu ya maisha yako na ya wanaokuzunguka.

Kuna vitu vingi kwenye maisha huwa hatuna majibu yake kwa sababu hakuna anayeweza kutufundisha moja kwa moja. Kwa kupenda kujisomea na kufuatilia mambo unajikuta unaelewa vitu hivyo na unafaidika navyo. Kwa mfano kuna baadhi ya tabia ambazo watu wengi kwenye jamii wanazo na zinawafanya washindwe kufanikiwa, pia kuna tabia ambazo watu wachache sana kwenye jamii wanazo na wanapata mafanikio makubwa. Kwa kupenda kufuatilia na kujifunza tabia hizi kwa kujisomea unajiweka kwenye nafasi nzuri ya kutengeneza tabia hizi za mafanikio kwako.

3. Kujisomea kunakusaidia kutatua matatizo na changamoto unazokutana nazo.

Maisha ya kila mtu yana changamoto na vikwazo. Huenda unapata msongo wa mawazo kutokana na kazi zako au familia yako, unaweza kujifunza jinsi ya kukabiliana na hali hiyo kwenye vitabu au hata kwenye mtandao. Huenda unapata tatizo la kuwa na matumizi mabaya ya fedha zako, unaweza kujifunza usimamizi mzuri wa fedha kwa kujisomea vitabu au mitandao mbalimbali. Hakuna tatizo ulilonalo sasa ambalo halijaandikiwa kitabu(kama unabisha niandikie tatizo lako kwenye email amakirita@gmail.com na nitakutumia kitabu au makala zaidi ya tano zinazoelezea unavyoweza kutatua tatizo hilo)

4. Kujisomea kunakujengea ujasiri kwenye kazi au biashara yako.

Kwa mfano unafanya kazi halafu unatakiwa kufanya ‘presentation’ au unafanya biashara ila kuna wadau ambao wanataka kuingia ubia kwenye biashara yako hivyo wanataka uwaelezee vizuri kuhusu biashara yako. Katika hali hizi mbili kama umejisomea na una uelewa wa kutosha utakuwa na ujasiri ambao utakufanya ukamilishe ‘presentation’ yako vizuri au kupata dili kubwa la kibiashara.

5. Kujisomea kunapunguza uchovu na msongo wa mawazo.

Tuseme labda umefanya kazi siku nzima na umechoka sana, badala ya kumalizia siku yako kwenye mitandao ya kijamii ambayo inazidi kukuongezea uchovu au kwenye tv ambapo unazidi kupata msongo ni vizuri sana ukajisomea kitabu kizuri cha hadithi. Kwa kujisomea kitabu cha aina hii utajikuta unahamisha mawazo yako kutoka kwenye uchovu na mihangaiko ya kila siku na kuyapeleka kwenye hadithi ya kitabu. Hii ni njia bora sana ya kujipumzisha hasa baada ya kazi inayochosha akili na mwili.

Nyongeza; Kujisomea kutakusaidia kupata kazi unayotaka.

Ni kweli kwamba nafasi za kazi ni chache sana siku hizi na wasiokuwa na kazi ni wengi sana. Usaili wa kazi siku hizi umebadilika sana, watu hawakazani sana kuuliza maswali ya kile ulichokisomea, wanajua unakijua na ndio maana umepewa mpaka cheti. Badala yake wanataka kujua uelewa wako kwenye maswala ya kawaida, uwezo wako kwenye uongozi na uwezo wako wa kukabiliana na changamoto za kila siku kwenye kazi zako. Kama wewe una tabia ya kujisomea utakuwa na uelewa mkubwa sana katika nyanja hizi muhimu za kazi ambapo yeyote atakayekusikiliza atakuwa na hamu ya kukuajiri kwa sababu anajua hutokuwa mzigo kwake. Ila kama huna uelewa wa ziada kuacha yale uliyosoma utasota kwenye usaili kila siku na kurudi kulalamika kwamba kazi hakuna. Hebu fikiri nafasi ya kazi imetangazwa moja, mmeomba watu 50, watano mmefikia vigezo vyote vinavyohitajika, kama hakuna upendeleo ni nani atakayepewa nafasi? Bila shaka ni yule mwenye vitu vingi vya ziada. Hivyo badala ya kulalamika kwamba wenzako wanapendelewa hebu anza kujifunza vitu vya ziada na uone kama utakosa kazi.

Kwa nini watu hawapendi kujisomea?

Pamoja na faida zote hizi ambazo wengi wetu tuinazijua bado wengi wetu hatupendi kujisomea. Tatizo ni nini?

Tatizo kubwa ni kwamba kujisomea ni tabia ambayo inatakiwa kujengwa kama unavyojenga tabia nyingine yoyote. Unapokuwa umeijenga tabia hii inakuwa sehemu ya maisha yako na haiwi tena vigumu kwako kuifanya.

Mwezi huu wa sita ndani ya KISIMA CHA MAARIFA tunajadili jinsi ya kujijengea tabia hii nzuri ya kujisomea. Kama umeona kuna umuhimu wa wewe kujisomea(upo hata kama hutaki) jiunge na kisima cha maarifa na ndani ya mwezi huu mmoja tutajenga tabia hii ambayo itakuwa sehemu kubwa ya mafanikio kwenye maisha yako.

Chukua hatua ya kujiunga na kisima cha maarifa mara moja kabla muda mfupi wa kujiunga haujaisha. Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma fedha tsh elfu kumi(10,000/=) kwa mpesa-0755953887 au tigo pesa-0717396253 na kisha tuma email yako kwa meseji kwenye moja ya namba hizo na utaunganishwa kwenye kisima cha maarifa.

Ndani ya KISIMA CHA MAARIFA utajifunza mambo mengi sana ikiwemo biashara na mafanikio.

Nakusihi sana uchukue hatua hii muhimu kwa kuboresha maisha yako, ukiikosa kuna siku utakuja kugundua ulifanya makosa sana kutofanya maamuzi haya muhimu. Sitaki uje uishi kwa manunguniko ndio maana nakusihi uchukue hatua hii.

Karibu sana, TUKO PAMOJA.